Kocha Mkuu wa Yanga Mbrazili, Marcio Maximo, kwa
ya kwanza ametoa ya moyoni baada ya kutamka kuwa, anataka kuona wachezaji wa
timu ya Yanga wanakwenda kucheza soka la kulipwa nchini Brazil.
Kauli hiyo, ameitoa kutokana na baadhi ya
watu kuhoji washambuliaji wake raia wa Brazil, Andrey Coutinho na Genilson
Santos Santana ‘Jaja’, kutua kuichezea Yanga katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara.
Maximo alisema
hakuna jambo la ajabu kwa wachezaji hao kucheza soka Tanzania na kuacha
kuendelea kukipiga Brazil kunapotambulika kuwepo na wachezaji wenye vipaji.
Maximo alisema, Brazil wapo wachezaji wengi
wa Afrika kutoka mataifa mbalimbali yakiwemo Angola na Msumbiji, wanacheza soka
kulipwa nchini huko.
Aliongeza kuwa, hakuna kitakachoshindikana
katika hilo, hivyo
amepanga kuyaboresha maisha ya wachezaji kwa kuwaandaa
kiprofesheno kwa kupata baadhi ya huduma muhimu kama kambi nzuri ya kisasa,
uwanja, gym na bwawa la kuogelea ili siku moja waende kucheza soka la kulipwa
Brazil.
“Ujio wa Coutinho na Jaja Tanzania umewashtua
watu wengi sana, lakini wanashindwa kutambua kuwa soka ni maslahi, wao wameona
yanafaa ndiyo maana wamesaini kuichezea Yanga.
“Klabu za hapa nchini zenyewe zimezoea
kusajili wachezaji kutoka Kenya, Uganda na baadhi za nchi Afrika Magharibi kitu
ambacho siyo sawa, lazima uchanganye wachezaji kutoka mataifa mbalimbali ili
uchanganye mifumo ya uchezaji.
“Wengi wanajua kwamba Brazil hakuna wachezaji
wa mataifa mengine kutoka Afrika, kitu ambacho siyo cha kweli, wapo wengi tu
wanacheza ligi huko, wapo kutoka Angola na Msumbiji, hivyo ninataka siku moja
kuona tunauza wachezaji Brazil,”alisema Maximo.
0 COMMENTS:
Post a Comment