Na Saleh Ally
MICHUANO ya Kombe la Dunia inakwenda ukingoni lakini
burudani inazidi kunoga na kila mechi inayofuatia inakuwa tamu zaidi, mfano
mzuri leo.
Nusu fainali ya pili ya Uholanzi dhidi ya Argentina,
ubashiri, kila mtu ana wake hakuna anayejua nani atashinda, lakini gumzo zaidi
ni washambuliaji wawili ambao asili yao ni winga.
Winga ni mchezaji anayecheza pembeni lakini timu zao
zinawatumia kama washambuliaji, Arjen Robben wa Uholanzi na Lionel Messi wa
Argentina na raha zaidi wote wawili, kila mmoja ni hatari zaidi kwa kutumia
mguu wake wa kushoto ‘mashoto’.
Robben ambaye alicheza fainali ya Kombe la Dunia mwaka
2010, nchini Afrika Kusini, ndiye mchezaji mwenye kasi zaidi kuliko wengine
walio katika michuano hiyo nchini Brazil.
Hiyo haizuii kasi ya Messi ingawa mshambuliaji huyo wa
Barcelona, bado hajaonyesha makali kama ilivyotarajiwa zaidi ya kufunga mabao
muhimu na pasi moja iliyobadilisha mambo na kuivusha Argentina.
Wachezaji ghali zaidi duniani ni Messi na Cristiano
Ronaldo, ambaye amesharudi kwao Ureno. Lakini Robben anaonekana kuwa bora zaidi
hata zaidi ya wawili hao na Messi atakuwa na kazi kubwa ya kuwaonyesha
wachambuzi wamekosea kutokana na wanavyochambua kwamba Robben ndiye hakamatiki.
Wawili hao ambao wanapiga mashuti makali mguu wa
kushoto, ndiyo silaha kubwa wanapokuwa wanamiliki au kukimbia na mpira watakuwa
na kazi kubwa leo saa 5 usiku kwa saa za Afrika Mashariki kuionyesha dunia
ubora wao.
Kila mmoja ana rekodi zake, huenda mmoja anamzidi
mwingine pale, lakini mwisho mechi hiyo ina rekodi zake ambazo zitapatikana
baada ya kuwa imekwisha na anayekwenda fainali kujulikana.
Messi:
Unaweza kusisitiza kwamba kikosi cha Argentina hakiko
vizuri sana kama ilivyo Uholanzi, lakini soka linabadilika katika kila mechi.
Lakini hata umahiri, Robben ameonyesha ni mshambuliaji
tishio zaidi kuliko Messi katika michuano hiyo ya Kombe la Dunia inayoendelea.
Messi ana mabao manne, moja zaidi ya Mholanzi huyo.
Mfano utaona kiwango chake cha kupiga mashuti sahihi,
kiko chini ukilinganisha na Robben, amepiga mashuti 15, lakini amelenga mara
saba tu na kuambulia asilimia 47 za ubora wa kulenga lango.
Messi amecheza dakika 453 na kufanikiwa kutoa pasi
moja tu iliyozaa bao. Bado inaonyesha hayuko kwenye kiwango chake sahihi, labda
kama atajirekebisha katika mechi ya leo na kuwa msaada zaidi kwa Argentina
kuliko ilivyo sasa.
Takwimu: KOMBE LA DUNIA MECHI SHINDA SARE POTEZA
2006, 2010, 2014
12
10
1 1
Robben:
Katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu, Mholanzi
huyo mwenye sifa mbili ‘mbaya’ za lawama, uchoyo na kujiangusha, ameonekana
kuwa bora zaidi na ndiye anayeonekana kuwa mchezaji hatari kuliko wote katika
michuano hiyo.
Tayari Robben amepachika mabao matatu na kutoa pasi
moja iliyozaa bao sawa na Messi, lakini amepiga mashuti tisa katika magoli ya
timu pinzani, kati ya hayo, nane yamelenga lango hivyo amepata asilimia 89 za
ubora katika hilo.
Katika dakika 480 alizocheza, Robben ameonekana ndiye
mshambuliaji msumbufu zaidi kwa mabeki wa timu zilizokutana na Uholanzi na
huenda Argentina wakawa katika wakati mgumu kama atakuwa katika kiwango chake.
Takwimu: KOMBE LA DUNIA MECHI SHINDA SARE POTEZA
2006, 2010, 2014
11
9
1
1
0 COMMENTS:
Post a Comment