Hatimaye lile sakata la kiungo mshambuliaji
wa Yanga, Mrisho Ngassa kwenda kufanya majaribio nchini Afrika Kusini katika
timu ya Free State Stars limepata majibu baada ya Meneja wa Taifa Stars,
Boniface Clement, kusema kuwa wao ndiyo walimruhusu.
Awali kulizuka utata ambapo Yanga
walitaka maelezo kuwa ni nani alimruhusu Ngassa kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Free State Stars bila ya ruhusa yao wakati wao walikuwa wanajua yuko kwenye kikosi cha Taifa Stars nchini Botswana.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupitia Katibu Mkuu wake, Selestine
Mwesigwa likieleza kuwa hawahusiki
na mchezaji huyo kwa kuwa hakuripoti katika kambi ya timu ya taifa alipoitwa.
Lakini Clement amesema kuwa, Ngassa aliomba ruhusa katika benchi la ufundi la timu
hiyo ili aweze kwenda kufanya majaribio na kudai kuwa TFF hawakuwa wakijua.
“Ngassa hana tatizo kabisa na Stars na
amejiunga na timu na anafanya mazoezi kama kawaida, kabla ya kuondoka alikuja
kuomba ruhusa katika benchi la ufundi na aliruhusiwa.
“Kwa upande wa TFF hawakuwa wakijua
suala hilo kwa kuwa wao ni watu wa ofisini, tutaendelea kuwa naye katika mechi
dhidi ya Msumbiji kwani taarifa zake tulikuwanazo na hana shida,” alisema
Clement.
Awali, Mwesigwa alisema Ngassa ameondolewa kwenye kikosi hicho kutokana na kocha kuchukizwa baada ya kuondoka bila ya kuaga.
Jana, Kocha Mart Nooij, akagoma kujibu swali hilo mbele ya waandishi wa habari na kuwataka wamfuate Ngassa hotelini na kumuuliza.
0 COMMENTS:
Post a Comment