USIANZE kwa kuniuliza
umuhimu au walichokifanya wachezaji kama Edibily Lunyamila au Shadrack Nsajigwa
ni kipi katika soka hapa nchini, hakika utakuwa unajua mengi.
Ukitaka nikukumbushe, nitasema
walikuwa tegemeo katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars, lakini kwenye
kikosi cha Yanga, pia Simba. Walijituma, walionyesha kweli wanaifanya kazi yao
kwa juhudi kubwa.
Sasa nawatambua kama
wachambuzi wa masuala ya soka katika gazeti hili maarufu la michezo la
Championi. Maana yake maisha yao kwa asilimia 95 ni soka, pia utaona sasa
Nsajigwa ni kocha wa vijana wa Yanga, maana yake ataendelea kujifunza mengi na
kutokoma kutoa mchango wake katika mchezo huo nchini.
Si wao tu, wapo wengine
kama Madaraka Selemani, Selemani Matola, Bakari Malima na wengine wengi ambao
mchango wao kwa taifa letu katika mchezo wa soka ulikuwa ni mkubwa sana.
Inawezekana hatuwapi
thamani kubwa, lakini tunapaswa kufanya hivyo ingawa leo nina ushauri kwao
kwamba kuna jambo la kujifunza ambalo nimeliona, ningependa waige.
Ukweli sijui wachezaji hao
niliowataja au wenzao wa kariba yao wamejaaliwa watoto wa wanawake au wanaume,
yote ni mambo ya Mwenyezi Mungu lakini hili la kujifunza litakuwa linawahusu.
Wakati Kocha Patrick Phiri,
maarufu kama Big Phiri alipotua nchini kuja kumalizia mazungumzo na Simba kabla
ya mkataba mpya, aliongozana na mwanasheria wake. Pamoja na kwamba aliwahi
kuifundisha Simba kwa vipindi viwili tofauti, lakini hii ilikuwa ni mara ya
kwanza kufanya hivyo.
Yule mwanasheria
aliyeongozana naye, aliwaambia viongozi wa Simba kuwa ni meneja wake, lakini
baadaye akawatambulisha ni mwanasheria wake pia. Halafu mwisho ikagundulika ni
binti yake wa kumzaa.
Anaitwa Melesiana Patrick
Phiri, namkadiria kuwa na miaka kati ya 24-26. Alionekana ni mtulivu muda wote
na taarifa zinaeleza hata wakati wa kujadili mkataba huo na viongozi wa Simba,
yeye ndiye alikuwa mzungumzaji mkuu.
Taarifa zinaeleza Melesiana
aliwachachafya viongozi wa Simba kutokana na kuuliza maswali kibao kutaka
kupata uhakika wa mkataba wa mzee wake au ukipenda sema ‘mteja’ wake.
Hata alipoambiwa atapewa
nyumba, Melesiana alihakikisha kwanza anaiona ni ya kiwango kipi na mwisho
alipata fedha yake kama mwanasheria kutoka kwa Mr Phiri, halafu ndiyo akarejea
Zambia.
Tusizungushe mambo, suala
la elimu na soka barani Afrika limekuwa na walakini. Waliosoma hadi elimu ya
juu ni aghalabu, hili linajulikana kutokana na mfumo wa maisha yenyewe, si
Tanzania au Zambia pekee, sehemu nyingi za bara letu au hata Asia na Amerika
Kusini.
Phiri ameliona hilo,
amesisitiza elimu kwa wanaye na Melesiana sasa amekuwa msaada kwake na
anamsaidia baba sasa kupeleka mambo kitaalamu na katika mpangilio ulio sahihi.
Kwa kifupi Phiri sasa ana
msaada katika kazi zake, ndiyo maana leo nikakumbuka kuwakumbusha wachezaji
wakongwe wa hapa nyumbani kwamba hawajui mbele baadaye itakuwaje.
Hivyo wana jukumu la
kusimamia elimu za watoto wao ambao baadaye wanaweza kuwasaidia kama ambavyo
Melesiana anavyosimamia maslahi ya Phiri ambayo ndiyo maslahi ya familia yake.
Unaposimamiwa kimaslahi na
baba, mama au mtoto, uchungu kwa mwenye akili nzuri unakuwa juu na unaongeza
chachu ya utendaji. Hivyo Melesiana amemsaidia Phiri kuzungumza au kuongoza yale
ambayo angeshindwa kuyaongoza kwa kuwa kazi yake kubwa ni kufundisha mpira.
Wachezaji wakongwe,
wasimamieni watoto wenu wapate elimu zaidi, wajue umuhimu wake na wasiamini au
kuishia mlipoishia nyie kwa kuwa huko mbele, safari ni ndefu na ushindani
utakuwa juu zaidi.
0 COMMENTS:
Post a Comment