Na Saleh Ally
BILA ya kujali ni kwa saa
ngapi lakini ukweli ni kwamba, mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England msimu wa
2014-15, imeionjesha Manchester United utamu wa mkiani.
Baada ya kipigo cha mabao
2-1 kutoka kwa Swansea, Manchester United ikawa katika nafasi ya 20.
Haitafutika kwamba
Manchester United ilipoteza mechi yake ya kwanza ya ligi na kuvunja rekodi huku
ikiweka mpya kwa kuwa tangu mwaka 1972, haikuwahi kufungwa katika mechi ya
ufunguzi, tena nyumbani.
Swansea wameivuruga Man
United katika mechi ambayo imeonekana kuwavuruga sana mashabiki wa Man United
ambao wengi wameonyesha kuwa, tabia za mashabiki hazipishani sana bila ya
kujali wako Afrika au Ulaya.
Mashabiki wa Man United
hapa Bongo, walikuwa wakilalama na kuona kuwa kipigo hicho ni tatizo kubwa,
wengine wakitaka van Gaal aondoke. Lakini hata wale wa Ulaya na Asia, pia
waliungana na wenzao wa Bongo kwa kumshambulia van Gaal kupitia Mtandao wa
Twitter.
Kinachowauma ni kwamba hata
David Moyes aliyeonekana ni ‘boga’, alianza mechi yake dhidi ya Chelsea kwa
sare ya bila mabao. Vipi van Gaal, kocha wa ‘level’ ya Kombe la Dunia anafungwa
na Swansea, tena ndani ya Old Trafford?
Katika mahojiano na runinga
ya Sky ya Uingereza, van Gaal alizungumza kitu ambacho kama utatulia, utagundua
Man United ina nafasi ya kurejea tena na kufanya vizuri ndani ya mechi mbili
hadi tatu zijazo.
Ingawa kuna hofu kwamba kutokana
na kuanza vibaya kwa van Gaal, basi Man United itaboronga zaidi ya msimu
uliopita, lakini ukweli haitakuwa hivyo kama tayari kocha huyo ameliona hilo na
majibu aliyoyatoa ni ushahidi tosha.
Alisema haya: “Kweli
kipindi cha kwanza wachezaji walionekana kama waoga, wenye hofu na sielewi kwa
nini. Tatizo jingine katika kipindi hicho, nilifanya uchaguzi kuwapa nafasi
wachezaji ambao hawakuwa sahihi.
“Kipindi cha pili pamoja na
kufanya mabadiliko, bado timu haikucheza kitimu kabisa. Hili nalichukua mimi
kuwa ni tatizo langu, kwa kuwa ndiye ninayewajibika.”
Hii inaonyesha kweli van Gaal
ni mkomavu, hakwepi majukumu, yuko tayari kujifunza na anaweza kuleta
mabadiliko kama ataungwa mkono katika wakati huu mgumu badala ya kusakamwa.
Pre season:
Kipindi cha pre season ni
kile cha kujiandaa na ligi, Man United ilifanya vema ikiwa ni pamoja na kufunga
mabao hadi 7 katika mechi moja. Mashabiki wake wakachekelea sana huku wakiwa
wamesahau ligi na mechi za kirafiki kuna tofauti kubwa.
Kipigo cha Swansea kinaweza
kuwa somo kwa wale wanaoutabiri mpira kishabiki badala ya utalaamu, maana pre
season ni kutengeneza timu na wala si mashindano.
Subira:
Kwisha kwa msimu wa 2013-14
huku Man United ikiwa imebaki katika nafasi ya saba na kukosa nafasi ya
kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya, iliwaumiza sana mashabiki wa Man United,
wakaamini Moyes ndiye tatizo.
Asilimia 90 ya mashabiki wa
Man United waliamini baada ya kuondoka kwa ‘tatizo’ Moyes, basi mambo
yangekwenda vizuri na heshima ingerejea.
Hviyo mechi ya kwanza ya
ligi ndiyo ilikuwa imejaa jibu la subira waliyoihifadhi tangu mwishoni mwa
msimu uliopita.
Jibu limekuwa tofauti,
ingawa hakuna kitu kibaya sana lakini imeonekana kuwaumiza na wengi
wamezungumza kuwa bora Moyes, bila ya kujikumbusha kuwa walimzomea au
kumshambulia sana msimu uliopita.
Mfumo:
Mfumo wa 3-5-2 alioutumia van Gaal, unaweza kuwa kweli
una tatizo na hasa suala la kwenda taratibu kutokana na kasi ya Premier League.
Hata angekuwa nani
angechanganyikiwa, ndani ya miezi 10, wachezaji wa Man United hasa wale wa
zamani, wanakutana na mifumo ya makocha watatu tofauti, Alex Ferguson, Moyes na
van Gaal. Si rahisi.
Bado ana uwezo wa kuendelea
nao au kuacha, kila kitu bado ni chaguo lake. Lakini hana ujanja, lazima
aongeze kasi ili kuendana na ule mfumo wa Man United.
Beki wa kati:
Kwa mabeki wa kati
waliocheza, Chris Smalling na Phil Jones, Man United haina ujanja. Lazima
ihakikishe inapata beki mmoja wa kati kisiki na mzoefu kwa kuwa walivyocheza
katika mechi hiyo, bora hata Rio Ferdinand ambaye alionekana umri umemtupa
mkono na hafai kabisa!
Tatizo lilikuwa ni namna ya
kujipanga, kukaba hadi kuwanyima raha washambuliaji, haikufanyika hivyo
kuwafanya wacheze wanavyotaka kama lilivyopatikana bao la kwanza kwa kuwa
mfungaji alikuwa peke yake hadi akaamua wapi pa kupiga na haipishani sana na
bao la pili.
Lakini kiungo pia hawakuwa
wakikaba vilivyo, hii ilionyesha kiasi gani Man United inahitaji kubadilika katika
hilo kwa kuwa Swansea walipiga pasi 28 bila ya kuguswa hadi walipofunga bao la
kwanza.
Kuinuka:
Nani anasema Manchester
United haiwezi kuinuka baada ya kipigo katika mechi ya kwanza au ufunguzi wa
Ligi Kuu England, tena ikiwa nyumbani?
Van Gaal alifundisha
Barcelona akachukua makombe, hali kadhalika Bayern Munich. Anajua harufu ya La
Liga na Bundesliga, sasa ameonja chumvi ya Premier League.
Kwa uzoefu wake ana uwezo
wa kubadilisha mambo ingawa bado uongozi wa Man United una kazi ya kumuunga
mkono kama alivyofanya mwenyekiti, Edward Martin aliyemuunga mkono Ferguson
kuanzia mwaka 1986 hadi 1990 alipotwaa Kombe la FA kwa mara ya kwanza.
Kila mmoja kwenye uongozi
hadi mashabiki waliokuwa wanaingia na mabango uwanjani, walitaka aondoke. Yeye
akashikilia msimamo kwa kuwa aliamini ni kocha bora. Nani atakataa van Gaal si
kocha bora? Basi wamlinde ili aweze kufanya mabadiliko na kutengeneza mfumo ili
kazi iende anavyotaka.
0 COMMENTS:
Post a Comment