Familia za viongozi wa benchi la ufundi na
madereva wa timu ya taifa, Taifa Stars, wamelilalamikia Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) juu ya kutolipwa fedha zao wanazotakiwa kulipwa kutokana na
majukumu yao.
Taarifa kutoka ndani ya benchi la ufundi la
Stars zilizofika mezani katika gazeti hili ni kuwa hakuna kiongozi aliyelipwa
fedha za posho na malimbikizo mengine tangu timu hiyo ilipoanza ushiriki wa
kuwania kufuzu Afcon 2015, mpaka hatua ya kutolewa.
Mhusika mmoja kutoka kwenye benchi hilo amesema
kuwa uwezekano wa wao kulipwa haki zao unaonekana kuwa mdogo kwa kuwa Rais wa
TFF, Jamal Malinzi hajaonyesha mwelekeo wowote juu yao.
“Wao (TFF) waliwalipa wachezaji tu, lakini
benchi la ufundi na madereva wanadai hadi hivi sasa na haijulikani watatulipwa
lini. Mwambieni rais anatuua kwa njaa.
“Tumevumilia sana, lakini hivi sasa uvumilivu
tunaona umeanza kutushinda, kwa sababu familia zetu hazituelewi,” alisema mtoa
taarifa huyo akionyesha kuwa na uchungu.
Juhudi za kumpata Malinzi kulizungumzia suala hilo, zilikuwa ngumu kwani pamoja na kupokea simu mara ya kwanza na kuulizwa swali, alisema:
“Naomba unipigie baada ya dakika 20, kuna kazi
ninamalizia.”
Lakini baada ya hapo, simu yake ilikuwa ikiita bila ya kupokelewa hata kidogo.
0 COMMENTS:
Post a Comment