Na Saleh Ally
KUMEKUWA
na mambo mengi sana yanazungumzwa kuhusiana na kukatishwa kwa mkataba wa
makocha Hans van der Pluijm na msaidizi wake, Charles Boniface Mkwasa.
Pluijm na
Mkwasa kwa pamoja walikuwa wanainoa Yanga, lakini baadaye wakapata ‘pande’ la
kuifundisha Shaolla FC ya Saudi Arabia, hivyo wakaamua kwenda kuanza maisha
mapya katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati.
Mechi ya
Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly wakati wakiwa Yanga ndiyo ilimvutia
wakala wa soka nchini Misri, kumfanyia mpango Pluijm raia wa Uholanzi ambaye baada
ya kutua Saudi Arabia aliwashawishi mabosi wake wapya ‘wamvute’ Mkwasa, dili likakubalika.
Wakiwa huko
walifanikiwa kuanza kazi vizuri na mwanzo ilionekana kama mipango ilikuwa inakwenda
kama kila kitu kilivyopangwa, lakini wiki ya mwisho ikawa ngumu sana kwao.
Siku nne
zilizopita, gazeti hili lilipata taarifa ya mkataba wao kusitishwa, juhudi zikaanza
kufanyika kuwatafuta wao ili waweze kuelezea suala hilo na aliyekuwa wa kwanza
ni Mkwasa ambaye alifafanua.
Baadaye gazeti
hili pia lilifanikiwa kumpata Pluijm naye akafunguka lakini ombi likawa kama anaweza
kuandika barua inayoelezea kuhusiana na kilichotokea, hakuwa mbishi, akaandika.
Zifuatazo
ni barua za maelezo za Mkwasa na Pluijm kuhusiana na sakata hilo wakielezea A
to Z ya mambo yalivyokuwa.
BARUA YA
PLUIJM:
Hallow Saleh
Habari yako,
kuhusu hapa katika klabu tunayofanya kazi, mambo si mazuri. Nitafafanua, kabla ya
sisi kuanza kazi, klabu hii ilikuwa na wachezaji wengi nyota kutoka Mali na
Morocco, lakini waliondoka na tulipouliza kwa nini, hatukuelezwa sababu.
Tulipoanza kazi,
baadhi ya viongozi walitaka kutuletea wachezaji wa kiwango cha chini, wengine ni
wa daraja la chini na wale ambao tuliona kwa tulichotaka, wasingekuwa na msaada
kwa timu.
Tulikubaliana
kuwapa nafasi, tukafanya nao mazoezi kwa siku 3 halafu tukaamua kuwaondoa,
waende zao.
Wiki tatu ambazo
tulifanya kazi na timu, zilikuwa nzuri na wachezaji walifurahia namna tulivyofanya
nao kazi na muhimu zaidi, ilionekana kuna mabadiliko ya kiwango kuboreka. Wachezaji
hao walionyesha hali ya kutuamini zaidi kitu ambacho kilikuwa kizuri kwetu.
Pamoja na hivyo,
baadhi ya wachezaji hawakuwa wameanza mazoezi pamoja nasi na tulielezwa hawakuwa
wamelipwa tokea msimu uliopita, baadaye tukagundua kulikuwa na matatizo mengi ya
kifedha na kiuongozi!
Baada ya kuwa
tumewakata wachezaji kama 10 hivi walioletwa kwa ajili ya kufanya majaribio,
hapo ndiyo matatizo yalipoanzia.
Viongozi wakaja
kwangu na Charles (Mkwasa) na kutueleza kuwa mkataba wetu umesitishwa,
inashangaza sana, lakini ndivyo ilivyokuwa.
Sasa tuko kwenye
maandalizi ya kila mmoja kutaka kurejea kwao.
Salamu kwenu
Kocha wa zamani
wa Yanga
Hans.
BARUA YA MKWASA:
Salaam,
Nafikiri nyote
hamjambo hapo nyumbani, hapa hali imebadilika ghafla baada ya kocha na uongozi kushindwa
kuelewana kutokana na usajili wa wachezaji wapya kwa msimu ujao.
Viongozi waliwaleta
wachezaji kwa majaribio ambao kwa muono wa kawaida hawakuwa na uwezo mzuri, kwa
jumla tuliwakataa na pia walikuwa wanataka wachezaji kutoka madaraja ya chini pia
walikataliwa, wao hawakupendezewa nalo, hivyo wakaamua kusitisha mikataba yetu kwa
sababu kubwa wanasema hawana fedha.
Msimu uliopita
timu hii ilishika nafasi ya 12 ambayo ni timu ya mwisho kubaki daraja hivyo Kocha
Hans alitaka wasajili wachezaji wenye uwezo ili waweze kufanya uzuri, kama haitoshi
wachezaji wachache wazuri wa Shoulla wa msimu uliopita nao walihama, hivyo timu
ilikuwa inahitaji wachezaji wengine wa hali ya juu.
Habari ndiyo
hiyo, likiharibika lawama kwa kocha, lakini usajili wanataka wachee. Taratibu za
safari ya kurudi ma kwetu zinafanyika.
Asante sana kwa
ushirikiano wako na Mungu akipenda tutaonana.
Wako.
Charles B.
Mkwasa
0 COMMENTS:
Post a Comment