IKANGAA ENZI ZAKE. |
WAZIRI wa
mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ameonyesha kushangazwa
kuhusiana na maandalizi waliyopata timu ya Tanzania katika michuano ya Jumuiya
ya Madola na matokeo ya mwisho yaliyopatikana.
Wakati
akizungumzia kuboronga kwa timu iliyokwenda Jumuiya ya Madola, Membe
alizungumza vizuri kama mzazi ambaye anaonekana hataki kuharibu mambo, lakini
maneno yake yalikuwa yanaashiria maswali mengi.
Alisisitiza
timu ikirejea, basi angependa kupata maelezo kuhusiana na kilichotokea lakini
aliumia sana na timu hiyo kufanya vibaya.
Membe kwa
niaba ya serikali, alifanya juhudi za kufanikisha kambi za wachezaji wengine
walikwenda Ethiopia, China na kwingineko, hiyo ilikuwa ni sehemu tu ya
maandalizi.
Wakati
Membe anasubiri timu ikirudi ajue kipi kilikuwa tatizo, pumba zimeanza kuzagaa
baada ya baadhi ya viongozi walioongozana na timu hiyo kuanza kutoa sababu
‘biskuti’, yaani zisizokuwa na msingi hata kidogo.
Meneja
aliyeongozana na timu hiyo, Muharami Mchume alikaririwa na vyombo vya habari
jana akisema, eti walishindwa kufanya vizuri kutokana na waamuzi kuwabania.
Haya ndiyo
maneno ambayo tumekuwa tukielezwa tokea miaka ya 1990 wakati Tanzania ilipoanza
kuboromoka kwa kasi kubwa kwenye mashindano ya kimataifa. Huenda viongozi wa
sasa bado wanaishi enzi hizo, hawajui lolote.
Nasema
hawajui lolote kwa kuwa sasa kila kitu kinaonekana, watu wameona kila
kinachoendelea na sijui kama kweli kwenye riadha kunaweza kuwa na mwamuzi
ambaye atakuonea. Pia kwenye ngumi, tuliona nahodha Selemani Kidunda akipigwa
hadi kuchanika puani. Bado kocha akasema ameonewa, meneja naye ameungana naye,
hawa watu wa aina gani?
Katika hali
ya kawaida, tayari wameunda sera ambayo watarudi nayo nyumbani, kwamba
wameonewa. Maana yake watakuja na mabegi ya nguo na viatu vya “mitumba” na “sale”
walivyonunua, pamoja na mizigo rundo ya sababu za kijinga.
Membe
anachosubiri, hatakipata. Hilo ninaweza nikamhakikishia kwa kuwa kufanya kwetu
vibaya katika michezo ya kimataifa, pia huchangiwa na uongo na watu kutoamini
kwamba kiwango chetu kiko chini. Kwanza tukubali, halafu tuanze kujiboresha ili
kukipandisha, hivyo tutaweza.
Mimi naweza
kuwa nina ushauri kwa Membe, nimueleze kwamba kwa hali ilivyo ya migogoro
katika vyama vya ngumi na riadha, nadra kuwa mafanikio hata kama timu
zitasafirishwa China, Marekani na kwingineko.
Kuna migogoro
mingi, hata wale magwiji wa michezo hiyo hawana ushirikiano mzuri. Najua
wataficha, wengine watakasirika kwa maandishi haya, lakini ukweli shujaa wa
nchi hii kwenye riadha kama Juma Ikangaa na Filbert Bayi, hawako karibu na
wanahitaji kukutanishwa.
Bayi ana
sifa zake, atakuwa na mchango wake na huenda anafaidika na michezo hiyo kwa
sasa kwa kuwa timu zikiweka kambi zinaweka kwenye shule yake, anasaidia kidogo
na yeye anapata kidogo na mambo yanakwenda, shukrani.
Vipi kuhusu
Ikangaa, shujaa wa Tanzania katika riadha, ikiwezekana mwanariadha mwenye
medali nyingi kuliko mwingine katika historia ya nchi hii. Mbona hatumuoni,
vipi hashirikishwi na maneno mengi na ninaweza kusema hapewi heshima yake.
Kweli Ikangaa, Bayi wakiungana hatuwezi kuwa na mafanikio?
Siwezi
kusema kuna hofu ya kufunikwa, mfano Ikangaa akionekana sana, wengine
hawataonekana. Ninacholenga ni kuonyesha ushirikiano kuwa ni duni na sasa ndiyo
wakati mwafaka mjue kuwa inapofikia timu ya Tanzania inakwenda Jumuiya ya
Madola au Olimpiki, tambueni ni suala la utaifa.
Hivyo
mashujaa wa taifa wapewe nafasi na viongozi wafanye kazi zao kwa kuangalia
maslahi ya taifa letu na si nafsi na matumbo yao. Tumechoka kuabishwa,
angalieni mlilia maandalizi hakuna
sasa mmehamia kwa waamuzi. Oneni haya,
mnatuumiza wajomba!
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment