FELLAINI |
Na Saleh Ally
WAKATI mwingine inakuwa ni vigumu
sana kukubali, lakini mambo yanapozidi kuwa magumu, kunakuwa hakuna mjadala
tena.
Soka linakwenda na bahati au aina
ya uchezaji katika timu fulani kutokana na kocha anataka nini, ndiyo maana
mchezaji anaweza kung’ara hapa, akashindwa kule.
Kuna wale wanaoshindwa kule, lakini
wakaenda sehemu fulani na kufanya vema kuliko ilivyotarajiwa.
Kwa misimu miwili, wachezaji wengi
wameishindwa Manchester United ambayo wanaonekana hawana bahati nayo na si
uwezo.
Wachezaji hao wamekuwa gumzo si
England tu, hata Tanzania na duniani kote, kwamba ni mizigo, hivyo waondoke.
Kocha Louis van Gaal, mara tu baada
ya kuchukua ‘job’, sasa ameruhusu wachezaji kadhaa waende zao.
Hawezi kusema ni mizigo, lakini
ukweli ndiyo huo kwa kuwa wanaonekana hawana faida licha ya kuwa na uwezo wa
juu na rekodi nzuri nyuma. Hivyo wanatakiwa waende zao, ili Man United iingize
fedha na kujiongeza.
Marouane Fellaini
Alitua Man United msimu uliopita
akitokea Everton baada ya Kocha David Moyes kumvuta kwa kuwa anajua ni ‘jembe’
lake.
Man United ilimwaga pauni milioni
27.5, lakini sasa iko tayari kumuuza kwa pauni milioni 20, ingawa inaonekana
watapata si zaidi ya pauni milioni 15 tu.
Javier Hernandez 'Chicharito'
Idadi ya mabao na dakika alizocheza
Man United zinamfanya kuwa mmoja wa wachezaji bora kabisa wa United. Lakini
hapati nafasi ya kutosha ya kucheza mbele ya Wayne Rooney na Robin van Persie,
hilo ndiyo tatizo lake na ajabu, Man United huwa haitaki kumpa nafasi kwa
kuendelea kutafuta mastraika wengine.
Jiulize akiingia ‘sub’ anapiga
mabao, vipi hapewi nafasi ya kutosha ili ajiamini zaidi na kuendelea kuwa
hatari zaidi? Huenda hana bahati.
Man United inataka kumuuza kwa
pauni milioni 12, lakini bila shaka itapata angalau pauni milioni 10 tu.
Jamaa ni mkali na tayari timu kibao
kubwa kama Juventus na Inter Milan (Serie A), Atletico Madrid (La Liga),
Tottenham na Southampton (Premier League), zinamhitaji.
Anderson
Ni kati ya wachezaji wenye uwezo
mkubwa, lakini inaonekana majeraha kila mara limekuwa ni tatizo kwake.
Kocha Alex Ferguson hakukubali
aondoke hadi mwisho alipokaribia kustaafu akamtoa kwa mkopo Fiorentina.
Lakini sasa mambo yanaonekana ni
magumu na van Gaal amemuonyesha mlango aende zake.
Nani anaweza kusema Anderson si
kiungo mzuri? Ana kila kitu, lakini Man United inaonekana si kwake.
Nani
Misimu miwili iliyopita amekuwa
ndiye chachu ya aina ya mashambulizi ya Manchester United. Kasi kubwa, krosi za
hatari na mashuti ya kushtukiza.
Lakini mambo yamebadilika, amekuwa
kama ‘amerogwa’ na kila anapopewa nafasi, anaboronga.
Man United imeonyesha uvumilivu wa
juu, lakini wapi na sasa bosi mpya ameamua kumpa nafasi akajaribu kwingine.
United iko tayari kumuachia kwa
pauni milioni 15.
Shinji Kagawa
Mjapani ambaye Ferguson alimnunua
kutoka Borussia Dortmund, lengo likiwa ni kuimarisha kiungo cha Mashetani
Wekundu.
Kagawa kajitahidi kupiga gia ili
ainuke, lakini wapi na ukweli huenda staili ya Man United imemshinda.
Ujio wa Juan Mata kutoka Chelsea
ndiyo unazidi kutia mchanga kitumbua chake na sasa United iko tayari kumuuza
kwa pauni milioni 10, ila zikipatikana 8 hamna noma, biashara inafanyika.
Kocha wake wa zamani, Jurgen Klopp
anaonyesha bado anamkubali na huenda akarejea Dortmund lakini wabishi Atletico
Madrid, wanaona anawafaa.
Wilfried Zaha
Akiwa Crystal Palace alionyesha
uwezo mkubwa na wengi wakaamini ndiye Pele wa England, Ferguson akajipinda na
kumuwahi kabla bei haijaenda juu.
Hakumtumia sana, alipoingia Moyes,
kukawa na mgogoro kwamba dogo anakula raha na binti yake bosi ndiyo maana
hapangwi.
Sasa van Gaal amesema acha dogo
aende zake na United iko tayari kulamba pauni milioni 10 ili impige bei.
Timu kibao zinamkubali na zinaamini
atafanya vizuri na West Ham, QPR, Crystal Palace na Newcastle, mojawapo inaweza
kumpata.
0 COMMENTS:
Post a Comment