Tambo zinaendelea kuelekea pambano
kali kati ya Azam na Mtibwa litakalopigwa Agosti 8 katika Tamasha la Usiku wa
Matumaini, Uwanja wa Taifa, Dar. Safari hii Kocha Mkuu wa Azam, Joseph Omog,
ametamba kwamba atahakikisha wanaisambaratisha Mtibwa siku hiyo.
Azam wameendelea kufanya mazoezi
makali chini ya kocha wake huyo raia wa Cameroon ambapo juzi Jumamosi walikuwa
kwenye Ufukwe wa Coco jijini Dar, wakisaka pumzi pamoja na stamina.
Omog amesema kikosi chake kinaendelea vizuri na maandalizi ya kuelekea kwenye
mchezo huo huku akiwatahadharisha wapinzani wake kuwa wajiandae kukutana na
kichapo kizito.
“Tunamshukuru Mungu maandalizi
yanakwenda vizuri kwa sababu tunahitaji ushindi katika mchezo huo ambao pia ni
sehemu ya kujiandaa na Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Mtibwa ni timu yenye wachezaji wazuri
lakini sitapenda kuona kikosi changu kinapoteza mchezo huo ambao utakuwa mgumu
kutokana na maandalizi jinsi yanavyoendelea kufanyika kwa timu zote mbili.
“Licha ya kuendelea kukipa mazoezi
makali kikosi change, leo (juzi) tupo hapa ufukweni kutafuta pumzi na stamina
kwa sababu ya kutaka kuendelea kuwa na timu imara yenye ushindani,” alisema
Omog, raia wa Cameroon.
0 COMMENTS:
Post a Comment