Na Saleh Ally
KWA mujibu
wa waandaaji wa ziara ya Real Madrid nchini, kikosi hicho kitawasili nchini na
kucheza mechi yake Agosti 23 dhidi ya nyota wa Tanzania.
Kikosi cha
nyota wa Tanzania kitateuliwa ili kupambana na Madrid ambayo italeta kikosi cha
wakongwe au magwiji wake ambao wana majina makubwa.
Bado
waandaaji hawajaanza kuyaanika majina, lakini kikosi cha wakongwe wa Madrid
kinaundwa na nyota kibao, mfano Zinedine Zidane, Luis Figo, Roberto Carlos,
Michael Owen, Michel Salgado, Steve McManamann na wengine wengi.
Kunaweza
kukawa na maoni tofauti kuhusiana na ujio wa nyota hao ambao itakuwa ni mara yao
ya kwanza kuongozana pamoja na kucheza katika ardhi ya Bara la Afrika.
Kikosi cha
wakongwe wa Real Madrid kitatoa mafunzo katika mambo mengi sana baada ya kutua
na kucheza nchini. Huenda mazuri au mabaya yatajitokeza, vizuri yote yakawa ni
sehemu ya shule.
Kikubwa
ambacho uchunguzi wa gazeti hili umefanikiwa kupata ni namna ambavyo kikosi cha
Real Madrid upande wa wakongwe kimekuwa kikifanya mambo yake katika maisha ya
kila siku.
Awali,
wakati inaelezwa kuna mpango wa kukileta kikosi hicho, ilionekana ni kama timu
ambayo itakusanywa kwa ajili ya safari ya Tanzania na baada ya hapo, kila mmoja
anachukua ‘time’ yake.
Lakini
mahojiano kati ya Championi na Rayco Garcia aliyekuwa Madrid, Hispania
yanaonyesha mambo ni tofauti na Madrid imekuwa ikiwapa nafasi wakongwe wake
kuwa na ratiba nzuri ambazo zinaonyesha utofauti mkubwa na mwenendo wa klabu
zetu hapa nyumbani.
Katika
maisha ya kawaida, wakongwe wengi wa Madrid wamekuwa wakiishi pamoja kwa kuwa
kwa wiki, mara mbili wanakutana na kufanya mazoezi kwenye uwanja ambao hutumiwa
na timu ya sasa ambayo inaundwa na nyota kama Gareth Bale, Cristiano Ronaldo,
Pepe, Sergio Ramos, Iker Casillas na wengine.
Wakongwe
hao si wote wanaoishi Madrid, lakini wapo ambao wamekuwa wakisafiri kutoka miji
au nchi jirani kuungana na wenzao angalau mara moja kwa wiki na kufanya mazoezi
pamoja.
Kikosi chao
kimekuwa kikisafiri pamoja na kwenda kucheza na vikosi vya wakongwe wengine
kama Manchester United, Arsenal, Liverpool, Inter, AC Milan na vingine barani
Ulaya.
Kwa mujibu
wa Rayco, kikosi cha wakongwe wa Madrid ambacho kimekuwa kikicheza mechi za
ushindani kitakuwa tayari kucheza na timu yenye nyota hata wale wa Taifa Stars
kwa kuwa kiko fiti.
“Unapofikia
wakati kuna mechi, siku za mazoezi zinaongezeka na benchi la ufundi la Madrid
limekuwa likijumuika na kikosi hicho kwa ajili ya mazoezi zaidi ili kuwafanya
wawe fiti kwa ajili ya mchezo unaofuata.
“Ni mechi
ya kwanza Madrid kucheza barani Afrika kwa kikosi hiki cha wakongwe. Hakuna
atakayefanya mzaha na tutashughulikia vizuri sana,” anasema Rayco ambaye ni
kati ya wachezaji wa kikosi hicho.
Rayco pia
amewahi kucheza timu ya vijana ya Barcelona kabla ya kurejea Madrid ambako sasa
anakipiga kwenye timu hiyo ya wakongwe na anasisitiza mashabiki wa Tanzania
watashangazwa tofauti na wengi wanavyoamini kwamba ni wakongwe, hivyo
hawataweza kucheza.
Achana na
yote, lakini hata kabla Madrid haijafika nchini, tayari funzo limejitokeza.
Kwamba wakongwe wa Yanga na Simba ambao wengi wanaendelea kuwa hazina ya soka
hapa nyumbani, wangeweza kuendelea kuwa pamoja kwa kushirikiana.
Suala hili
linaweza kuanzishwa na klabu hizi mbili kongwe, zikawaandalia utaratibu mzuri,
zikawatafutia angalau udhamini mdogo ambao ungewasaidia kujiendesha na wao
wakaendelea kuwa karibu na klabu.
Inawezekana
wao kuendelea kuwa karibu na klabu na wakawa msaada. Lakini kuwa pamoja lazima
watazalisha mambo yanayoweza kuwa msaada kwenye soka katika klabu hizo na
nyumbani.
Kikubwa
kama hilo litawezekana, wachezaji hao wafuate utaratibu, wafanye mambo yao kwa
kuangalia mafanikio au kujenga na si majungu. Acha Madrid ije, kutakuwa na
mengi ya kujifunza.
0 COMMENTS:
Post a Comment