Na Saleh Ally
HATA kama itaonekana ni kazi lahisi lakini wiki moja ijayo ndiyo
itakuwa ngumu sana kwa Kocha Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic, kwa maana ya
kufanya uamuzi wa kitaalamu zaidi.
Uongozi wa Simba umeamua ‘kujilipua’, umewaleta washambuliaji watatu
kutoka nchi tatu na wote wanachezea timu za taifa, lakini anatakiwa mmoja tu.
Loga ndiye atakuwa na jukumu la mwisho la kuamua kuhusiana na
washambuliaji hao watatu ambao ni Modo Kiongera ni raia wa, Ousimanou Manneh kutoka Gambia ambaye
imeelezwa anakipiga nchini Senegal na Jerome
Ramatlhakwane maarufu kama Rama raia wa Botswana anayekipiga TP Mazembe
iliyomtoa kwa mkopo Don Bosco ya DR Congo.
Kwa maana ya takwimu, karibu wote wanaweza kuwa wachezaji wazuri
wakatoa msaada kwa Simba ingawa lazima waonyeshe kwa vitendo.
Ukiangalia takwimu, Rama ndiye anaonekana ana uwezo mkubwa zaidi
katika upachikaji mabao na changamoto ya mabadiliko ya soka la Botswana kupanda
haraka, unaweza kushawishika kumpa nafasi ya kwanza kuwa anastahili.
Kiongera, bado ni kati ya wachezaji bora na wenye kiwango bora na
anaichezea Harambee Stars kama mmoja wa washambuliaji wanaopewa nafasi ya pili
baada wale wanaocheza nje ya Kenya.
Manneh si mshambuliaji mzoefu sana, huenda uwezo wake atakapofanya
kazi mbele ya Loga kunaweza kukawa na majibu mazuri zaidi. Lakini suala la umri
wa miaka 19, linaweza likawa linambeba.
Kwa kuangalia walivyo, unaweza kusema nafasi ya kwanza ni kwa Rama,
pili Kiongera na Manneh abaki nafasi ya tatu.
Lakini kwa kuwaona kunaweza kukawa na jibu sahihi zaidi yupi atakuwa
msaada kwa Simba, ingawa bado Loga anatakiwa kukubali kuwapa muda zaidi Rama na
Manneh.
Kiongera na Loga wamewahi kufanya kazi pamoja wakiwa Gor Mahia.
Hivyo Rama na Manneh anatakiwa kuwaona na kutoa uamuzi ambao utakuwa
sahihi na si ule wa hisia kama ulivyoanza kuhisiwa kwamba yeye anaamini
Kiongera ni sahihi.
Ana haki ya kufikiri hivyo kwa kuwa anaijua kazi yake, lakini kuweka
uwanja wazi awaone na Rama na Manneh, litakuwa jambo zuri na uamuzi wake wa
mwisho utakuwa kwa manufaa ya Simba na hata usalama kwa kibarua chake.
Siku zote timu inakuwa ni mawazo ya wengi yanayoongozwa na wachache.
Mtihani kwa Loga unaweza ukawa mgumu au lahisi kutokana na uwezo utakaoonyeshwa
na washambuliaji wote.
Kama watakuwa wanatofautiana sana kiwango, kwake itakuwa lahisi kung’amua
mambo mapema na kwa ulahisi zaidi.
Lakini viwango vyao vikiwa vinakaribiana, basi bila shaka kila kitu
kitakuwa kigumu na umakini utalazimika kuongezeka.
Kwa uongozi wa Simba, pia unapaswa kumuamini Loga kutokana
atakayemchagua kwa kuwa mwisho mbeba lawama ni kocha. Na isitokee kukawa kuna
kiongozi anahitaji kufurahisha nafsi yake.
0 COMMENTS:
Post a Comment