Na Saleh Ally
GARETH Bale ndiye mchezaji
ghali kuliko wote duniani katika kipindi hiki baada ya uhamisho wake wa pauni
milioni 86 kutoka Tottenham Hotspur kwenda Real Madrid kuweka rekodi mpya.
Pamoja na kuwa ghali, mwenye
fedha za kutosha, tokea kuanza kwa maandalizi ya msimu Bale amewashangaza wengi
baada ya kuwahi mazoezini kuliko wachezaji wote.
Achana na kuwahi mazoezini,
zaidi ya mara 15, wachezaji wa Madrid wameondoka mazoezini na kumuacha yeye
akijifua pekee.
Pia wamemkuta akiwa
mazoezini ameanza kujifua zaidi ya mara 10, hali inayoonyesha Braza amepania
vilivyo kung’ara na kuisaidia Madrid msimu uhao hata kuliko alivyofanya msimu
uliopita.
Mazoezi ambayo amekuwa
akifanya Bale yakiwemo yake ya kukimbia kasi yameonyesha kiasi gani wachezaji
wanaweza kuwa na hamu au tamaa ya kufanya vizuri hata baada ya kufanikiwa.
Wachezaji wengi wa Kiafrika,
wakiwemo wa hapa nyumbani Tanzania, mara baada ya mafanikio kidogo tu, basi
wanajiingiza kwenye starehe au wanavmba vichwa.
Bale ndiye ghali, ameonyesha
kweli ana uwezo lakini bado ndiye amekuwa wa kwanza kufika mazoezini, anawahi
na kuanza kabla ya wenzake, lakini anaendelea na mazoezini baada ya kumaliza na
wenzake.
Tamaa ya maendeleo haiwezi
kupatikana usingizini na hilo linaweza kuthibitishwa na vitendo vya Bale ambaye
anajiandaa na msimu mpya wa La Liga huku akiwa amepania kufanya vizuri zaidi ya
msimu uliopita.
Kung’ara:
Kabla ya hapo, rekodi
iliyokuwa juu ni ile ya Cristiano Ronaldo kutoka Man United na kutua Real
Madrid kwa pauni milioni 80.
Baada ya Bale kutua Madrid,
mengi yalizungumzwa na uchambuzi kwamba ilikuwa ni vigumu kwake kufanya vizuri
au angefunikwa kabisa na Ronaldo.
Wachezaji kadhaa nyota hasa
wale wakongwe nchini England walimshauri kubaki Spurs. Lakini raia huyo wa
Wales, alizidi kuwa jasiri akahakikisha anafikia alichokuwa nakitaka, kuichezea
Real Madrid na kutimiza ndoto yake.
Msimu uliopita, Bale
amefanya mengi makubwa ambayo yamethibitisha kuwa yeye ni bora, lakini ni mchezaji
anayejiamini na kutaka kufanya na kutimiza anachoona ni sahihi.
Alifanikiwa kucheza mechi 24
za La Liga na kufunga mabao 15, huku akitoa pasi 12 zilizozaa mabao, hilo
lilikuwa jibu kwa wote walioamini nyota huyo mwenye miaka 25 alikuwa hana nafasi ya kung’ara Hispania kwa
madai aina yake ya uchezaji haiendani na ile ya La Liga.
Bale ameng’ara, amefanya
mambo mawili makubwa ambayo ni furaha ya juu ya viongozi, wanachama na
mashabiki wa Real Madrid. Kuifunga Barcelona na kubeba makombe kwani alikuwa mchango
mkubwa hadi Madrid ilipobeba ubingwa wa Ulaya kwa mara ya kumi.
Msimu mmoja tayari ana
makombe mawili, Copa de Rey na Ligi ya Mabingwa, lakini jamaa bado hajaridhika,
anataka tena.
Mechi 10:
Katika mechi 10 za mwisho
msimu uliopita, Bale alicheza dakika 876, alikosa dakika 24 tu baada ya kucheza
dakika 86 wakati Madrid ikiitandika Sociedad kwa mabao 4-0, yeye akipachika
moja.
Mechi nyingine ambayo
alicheza 70 ilikuwa ni Madrid ilipoitwanga Almeria kwa mabao 4-0, Bale akafunga
moja. Katika mechi hizo kumi amefunga jumla ya mabao sita.
Katika mechi hizo kumi,
pamoja na kufunga mabao sita, Bale amekuwa nyota wa mchezo mara tatu, wakati
Madrid ilipoichapa Malaga 1-0, halafu dhidi ya Rayo Vallecano waliyoshinda 5-0
pia walipoitandika Barcelona 2-1.
Bale ameweka rekodi ya juu
zaidi katika mechi dhidi ya Rayo Vallecano ambayo Madrid ilishinda kwa mabao
5-0, yeye akafunga mawili, akawa nyota wa mchezo lakini akapata alama 10 za
ubora wa mechi. Kama ungekuwa ni mtihani, alipata mia kwa mia.
Inawezekana Bale anataka
bado kuonyesha ubora wake, lakini anajua bila ya mazoezi ya kutosha hataweza
kufanya vizuri wala kuuonyesha ubora huo. Funzo kwa wale wanaojiandaa na Ligi
Kuu Bara pia, kwamba kipaji au uwezo pekee bila mazoezi ya kutosha, haitoshi.
Mechi 24
Mabao 15
Asisti 12
Kilo 74
Urefu mita 1.83
0 COMMENTS:
Post a Comment