YANGA wamefunga usajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, watani
wao Simba watakuwa bado wanahangaika katika nafasi moja, nao watafunga.
TP Mazembe inaonekana ipo tayari kumtoa Ramatlhakwane kwa Simba, lakini
mazungumzo hayajakamilika. Simba watakapomalizana na hilo, hakuna shaka nao
watafunga usajili na baada ya hapo ni kambi.
Kambi kwa timu zote zimeanza, wataalamu wanaziita off camp. Wachezaji
wanakwenda uwanjani na kufanya mazoezi, baada ya hapo kila mmoja anarejea
nyumbani kwake. Hakuna ubishi
baada ya hapo, Yanga, Simba watabadilisha mfumo na kuanza kambi ya wachezaji
kuishi pamoja.
Ukitaka kufanya tathmini ya usajili, angalau Sh milioni 200 au zaidi
kutoka kila upande zitakuwa zimetumika. Maana yake kwa msimu huu pekee, Yanga
na Simba zitakuwa zimetumia zaidi ya Sh milioni 400 kwa ajili ya usajili tu.
Kwa wachezaji iliyowasajili na makocha wawili kutoka Brazil, hapana
shaka Yanga wanaweza wakawa wametumia fedha nyingi zaidi. Pengine milioni 300
au zaidi ya hapo. Hayo yote yanaweza yakawa yamepita.
Sasa kinachofuatia ni maandalizi ambayo yatatoa majibu ya kile
walichotoa, fedha walizomwaga kufanya usajili. Lazima kuwe na kambi za uhakika
ambazo zinaendana na mfumo wa kisasa.
Kwa Azam FC, wao hilo linaweza lisiwe tatizo. Wana kambi nzuri na kila
kitu kinapatikana kwa ajili ya maandalizi na huenda makocha au wachezaji wao
wanaweza wasiwe na sababu kuhusiana na mazingira mazuri.
Wale wa Yanga na Simba, vipi? Uongozi wa klabu hizo kongwe unalitambua
hilo, kwamba umepoteza fedha nyingi kwa ajili ya usajili kama utajumlisha ada
ya usajili, kuwalipa wachezaji na mishahara minono itakayokuwa inamwagwa kila
mwezi, bila ya kusahau posho?
Kambi wanazozitegemea zitakuwa ni za kukodi kwa kuwa hawana sehemu au
vifaa kama ilivyo kwa Azam FC. Ndiyo maana siku chache zilizopita nikaandika
makala na kuelezea kuhusiana na “soka la kutembeza”.
Niwakumbushe, usajili mzuri au wa majina pekee bila ya maandalizi bora
itakuwa ni kazi bure. Mwisho wake hata akina Jaja, Coutinho na wengine
waliosajiliwa Simba hawatakuwa na lolote.
Kuna taarifa Yanga watakwenda kujichimbia Pemba na maandalizi yako
katika hatua za mwisho, Simba pia wana mpango wa kwenda Afrika Kusini kwa kambi
ya siku takribani kumi. Ni jambo zuri, lakini kuna jambo pia nitakumbusha.
Timu kusafiri na kwenda kuweka kambi nje ya Dar es Salaam, mara nyingi
limekuwa likitumika kama jambo la uhamasishaji na si ufundi. Uongozi unaamini
kuwa kama timu itakuwa nje ya Mkoa wa Dar, basi mashabiki na wanachama au
wachezaji wenyewe watahamasika na kujituma.
Lakini wakati mwingine hata kambi hizo za mikoani au nje ya Tanzania
zimekuwa zikijaa kasoro kibao na wachezaji badala ya kujituma baada ya
kuhamasika, wanatumia muda mwingi kulaumu kutokana na kuwepo kwa kasoro lukuki.
Hivyo ni jambo jema, uongozi wa Simba na Yanga ukazipima kambi hizo kwa
kuangalia uhakika. Kwamba kama kweli zimelazimika kupeleka vikosi vyao nje,
basi iwe kwa sababu hasa za msingi na kambi zina ubora sahihi.
Mwisho ni katika suala la mechi za kirafiki ambazo Simba na Yanga
zitacheza wakati wa kujiandaa. Lazima ziwe ni zile kwa ajili ya kujenga kikosi
na kumpa nafasi kocha kukitathmini kikosi chake na si ilimradi kwa kuwa
viongozi ndiyo wameamua na hakuna la kufanya. Msipokuwa makini, mwisho mtaishia
kuwa gumzo wakati wa usajili, mwisho wanaobeba ubingwa wanakuwa wengine.
0 COMMENTS:
Post a Comment