Na
Saleh Ally
KUPITIA
runinga ya Msumbiji iliyoonyesha mechi ya Tanzania dhidi ya Msumbiji waliokuwa
kwao, nilimuona beki Shomari Kapombe akiangua kilio mara baada ya mechi.
Sura
ya Kapombe iliashiria uchungu au uzalendo kwa kuwa alitaka kushinda mechi hiyo
na kuiona Tanzania inafuzu kwenye hatua ya makundi kuwania kucheza Kombe la
Mataifa Afrika.
Mjadala
umekuwa kuhusiana na kilio hicho cha Kapombe, kitu ambacho naona hakiwezi kuwa cha
msingi katika mjadala huu wa kwa nini Tanzania imekuwa ni timu ya “ilibaki
kidogo tu.”
Sidhani
kama ni kipindi sahihi kujadili eti Kapombe alimwaga chozi, unaweza kuichukulia
kama ni sababu binafsi ya uzalendo wake kwa taifa. Lakini bado Kapombe na wenzake
ni sehemu inayohusiana na suala la kufeli kwa Stars.
Mchezaji
gani wa Taifa Stars anaweza kujitoa kwenye timu na kusema mimi tu ndiyo
nilifanya vizuri zaidi? Lakini kama maandalizi waliyopewa na TFF hayatoshi au
hayakuwa sahihi, wanapaswa kusema pia.
Kwa
hiyo wachezaji pia ni sehemu ya kufeli kwa timu yetu. Safari hii inabidi
wawajibike kwamba wametufelisha na hakuna zaidi ya hilo. Hivyo acha Kapombe
alie lakini ukweli ni hivi, wachezaji ni sehemu ya kufeli kwetu.
Mjadala
mwingine ni kuhusiana na mwamuzi wa mechi hiyo, Dennis Bate kutoka Uganda
pamoja na msaidizi wake kwamba ‘waliiuma’ Taifa Stars na ‘kuibeba’ Mambas
ambayo iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kusonga kwenye hatua ya makundi.
Sababu nyingine ya Taifa Stars kutolewa
imekuwa ikielezwa ni mwamuzi huyo Mganda kwamba aliiuma Stars kupita kiasi na
kusababisha kutolewa. Tena mwamuzi wa pembeni ndiye amekuwa akituhumiwa zaidi.
Katika
hali ya kawaida kuwalaumu waamuzi hao ni kupoteza muda, tena bila sababu za
msingi. Waamuzi hao Waganda hawakuwepo wakati Taifa Stars chini Marcio Maximo
ikishindwa kuifunga Msumbiji nyumbani Dar es Salaam na baadaye kwao Maputo.
Waamuzi
hao hawakuwepo wakati Taifa Stars ya Kim Poulsen ilipong’olewa na Msumbiji
baada ya sare Dar es Salaam na Maputo. Mikwaju ya penalti ikatumika, pamoja na
Juma Kaseja kuokoa mara mbili, Stars ikang’olewa!
Mara
zote mbili, waamuzi hao wa Uganda hawakuwepo. Hivyo kuwafanya wao ndiyo hoja ya
Stars kufeli ni kupoteza muda. Ndiyo maana lile la machozi ya Kapombe, waamuzi
hao naona si suala la msingi kujadili kwa sasa.
Mwisho
wa Watanzania kusema “ilibaki kidogo tu” utakuwa ni lini? Hakika ni kitu
kinachokera na huu ndiyo wakati wa kufanya maamuzi magumu. Nani anawajibika?
TFF
ilifanya maandalizi kuanzia Tukuyu, Dar es Salaam, Afrika Kusini na mwisho
ikapaa hadi Msumbiji. Kitaalamu kuna cha kujifunza, kwamba mazoezi hayo
yalikuwa na tija au ndiyo yaliwachosha wachezaji!
Tuangalie
mambo yaliyofanyika kisiasa zaidi kwa TFF kutaka kujivua gamba la aibu ya
kufanya vibaya kama ikitokea timu ikatolewa. Kwamba inaonekana imefanya mazoezi
sehemu nyingi lakini mwisho hayakuwa na msaada!
Je,
kocha Mart Nooij anasemaje kuhusu wachezaji wetu, vipi kuhusu uwezo wake na huu
ndiyo uwe mwisho wake au tuendelee naye? Wachezaji tulionao, wote wanastahili
kuichezea Stars au ni kikosi kinachoitwa kwa kufuata mazoea?
Kama
ni kikosi kinachoitwa kwa kufuata mazoea, vipi tunaoneana haya? Au kwa kuwa
wachezaji ni rafiki na ndugu zetu tunaona haya kuwaambia ukweli? Haya ndiyo
mambo ya kujadili sasa na si nani amelia au kujigaragaza uwanjani!
Kama
ni mjadala uanze sasa na nini cha kufanyia kazi kwa kuwa visingizio pumba kama
hivyo vya mwamuzi Mganda na mwenzake haviwezi kuwa msaada kwetu hata kidogo.
Badala yake tutaendelea kujiangusha zaidi.
Nani
tunamuweza, Tanzania inaweza kushinda au kufanya vizuri zaidi mbele ya nani
kama Msumbiji wamekuwa wakifanya wanachotaka kila wanapokutana na sisi?
Wakisikia wanakutana na Tanzania, wanajua kutakuwa na ugumu lakini kusonga
mbele ni uhakika kwao!
Mjadala
ndiyo umeanza sasa, lakini vizuri twende kwenye pointi za msingi na tuondoe
ushabiki wa Yanga na Simba, upinzani wa nani anamtaka au hamtaki nani TFF.
Badala yake tuangalie utaifa kwa kuwa sisi ni Watanzania, timu yetu
inapoharibu, hatuwezi kubadili utaifa tukashangilie kwingine.
0 COMMENTS:
Post a Comment