August 25, 2014

TANZANIA ELEVEN


KIKOSI cha Tanzania Eleven kilicheza mechi safi ya kirafiki dhidi ya wakongwe wa Real Madrid na kuishia kulala kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, juzi.
Mechi hiyo ilikuwa ni ya kuvutia na ilihudhuriwa na watu wengi sana waliotaka kuona burudani hiyo. Kweli wengi walijitokeza kuwaona nyota wa Real Madrid kama Luis Figo, Cristian Karembeu, Fabio Cannavaro na wengine.
Pia walijitokeza kwa wingi kwa kuwa walitaka kuwaona nyota kama Malota Soma, Mao Mkami, Clement Kahabuka, Abubakari Kombo, Kali Ongala, Iddi Moshi, Madaraka Selemani, Nassor Mwinyi Bwanga, Mtwa Kihwelo, John Mwansasu, Sabri Ramadhani ‘China’ na wengine wengi.

Mechi ilikuwa  nzuri lakini hakuna ubishi kwamba Madrid walicheza vizuri zaidi na kuonyesha kwamba wameishi katika maisha ya kufanya mambo yao katika mpangilio mzuri zaidi.
Bado unaweza kusema, wakongwe wetu wa Tanzania Eleven walijitahi na huenda bado wamo kisoka ingawa kisingizio kinaweza kuwa timu hiyo haikuwa na muda wa kutosha wa mazoezi pamoja. Kikubwa ambacho ninazungumzia leo ni mizengwe iliyokuwa imetawala kwenye kikosi hicho.
Mara baada ya kuteuliwa na hata kilipocheza. Kilijaa mizengwe lukuki huku tayari kukiwa na watu wasiowataka wachezaji fulani kuachwa kwa wachezaji ambao walionekana wangekuwa na msaada na wana uwezo wa juu zaidi.
Unaweza kujiuliza kwa timu ile kwa nini uwaache nje Malota Soma na Clement Kahabuka ambao wako fiti kuliko Emmanuel Gabriel ambaye alilazimishwa kucheza akiwa anajulikana ana tatizo la goti?
Kwa nini wengine warudi uwanjani mara mbili, mfano Kally na China ambao walitolewa na kuingia, halafu wengine wakabaki nje? Jiulize kama kocha aliamua kuwatoa, vipi akawarudisha tena.
Je, waliokuwa nje wote wasingeweza kucheza safu ya ushambuliaji kama Malota au Kahabuka halafu Kally narejea tena? Nimejaribu kufuatilia mengi hadi kufikia kuandika hii.
Lakini utaona kuna watu walisema hivi, wengine walijiita viongozi wakasema vile. Wako waliwasingizia makocha maneno haya au yale. Makocha pia wanaweza kukuambia nafasi za kucheza zisingetosha.
Utaona Real Madrid walikuwa na watu 11 kwenye benchi wakati Tanzania Eleven ilikuwa na watu 16 ambayo ni timu nyingine. Ndiyo maana nasisitiza, China na Kally hawakuwa na sababu ya kurejea mara mbili na kocha angeona wako safi, hakuwa na sababu ya kuwatoa.
na ninaamini kuna watu watakuwa hawazungumzi tena baada ya mechi hiyo kupita.

Hao ndiyo wakongwe, walichokifanya kwenye mechi hiyo achana na kile cha uwanjani, lakini mizengwe ambayo huenda kwa mashabiki ingekuwa si lahisi kuyajua, ndiyo majibu ya mpira wetu ulivyo.
Umejaza watu wasiopendana, watu wasiotaka fulani aujulikane, kuonekana au kufanikiwa. Sasa mpira wenyewe utapiga vipi hatua kwenda kwenye mafanikio wakati walio ndani yake hawataki watu wafanikiwe?
Wakongwe wameonyesha kuwa enzi zao pamoja ya kuwa na sifa nzuri kama kujituma licha ya kwamba walilipwa kidogo. Lakini wamethibitisha walikuwa na kasoro ya kutopendana na kutakiana mema, huenda ndiyo maana Tanzania haikufanikiwa sana kisoka.
Tujiulize, tabia hizo mbaya ndiyo vijana wetu wa sasa wamerithi kutoka kwa baba zao ndiyo maana mchezo wa soka umefunga breki na sasa umekuwa ni ule wa hadithi nyingi tu?
Kuna jambo kubwa la kujifunza kupitia kikosi hicho. Tuanzie uwanjani kwa tuliyoyaona kwa kuwa kama ni mazuri pia yapo. Lakini  niwasisitize vijana wanaocheza au wanaojiandaa baadaye kuwa wachezaji nyota kwamba zengwe, chuki, haliwezi kuusaidia mpira wa Tanzania, hilo msiige, waachieni hao wazee wenu wazee nalo, waende nalo. Upendo na kutakiana kheri ni sehemu ya nguzo za mafanikio. 

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic