Na Saleh Ally
UMESIKIA taarifa za England kuhusiana
na mauzo ya jezi? Mshambuliaji nyota wa Manchester United ndiye aliyemaliza
msimu akiongoza kwa mauzo.
Jezi yake namba 20, ndiyo iliyouzwa
zaidi kuliko nyingine ikiwa ni msimu mmoja tu baada ya kujiunga na Mashetani
Wekundu akitokea Arsenal.
Baada ya Gerrard, fowadi Luis Suarez
ameshika nafasi ya tatu akiwa na jezi namba 7 ya Liverpool, sasa ameiacha na
kutua Barcelona.
Nafasi ya nne imekwenda kwa Eden
Hazard wa Chelsea, halafu tano bora ikafungwa na Mesut Ozil aliyekuwa ametua
Arsenal akitokea kwa vigogo, Real Madrid.
Wengine wanaofunga 10 bora ya jezi
zinazouzwa zaidi katika Ligi Kuu England msimu uliopita ni Wayne Rooney
(Manchester United), Sergio Aguero (Manchester City), Juan Mata (Manchester United),
Shinji Kagawa (Manchester United) na Frank Lampard (Chelsea).
Hiyo ni 10 bora ya England, jiulize ya
Tanzania Bara iko wapi, si rahisi kuwa na jibu wala kupata takwimu kwa kuwa
klabu kubwa na zile maarufu za Tanzania wala hazijihusishi na biashara ya kuuza
jezi.
Si kwamba haziamini hiyo ni biashara,
lakini uvivu na kuridhika na viingilio vya milangoni na fedha kidogo za
wadhamini, kwao inatosha.
Ukiangalia katika 10 bora ya England,
utaona biashara imekuwa kubwa zaidi kwa wachezaji wanaosajiliwa kutoka klabu
moja kwenda nyingine na wale wakongwe wanaokubalika sana kama Gerrard na
Lampard, mauzo ya jezi zao yanaendelea kuwa juu.
Pia inategemea aina ya timu, kwani
Fernando Torres alikaa kileleni kwa misimu mitatu mfululizo, wakati huo akiwa
Liverpool, lakini baada ya kutua Chelsea, taratibu ameporomoka hadi kuondoka
kabisa 10 bora.
Hapa nyumbani, Yanga na Simba ndiyo
walikuwa na nafasi kubwa ya kufanya biashara kwa kutumia jezi za wachezaji
fulani, halafu Mbeya City, Azam FC, Mtibwa Sugar na nyingine zingefuatia.
Angalia wakati wa usajili wa Emmanuel
Okwi, Yanga wangeuza jezi kiasi gani na wangeingiza fedha kiasi kipi?
Hiyo haitoshi, usajili kwa ajili ya
msimu ujao, Jaja, Coutinho, lazima wangeiingizia Yanga fedha nyingi kama ilivyo
kwa Simba na Paul Kiongera, Pierre Kwizera, Amissi Tambwe na wengine.
Vipi sasa klabu hizo hazina hesabu ya
kutengeneza fedha wakati kuna soko? Angalia Barcelona baada ya kukubaliana tu
na Suarez, jezi zikaingia sokoni, mamilioni yakapatikana.
Klabu za Yanga, Simba na nyingine
hazina wabunifu, watu hawaelewi au wavivu wa kazi. Basi wana kila sababu ya
kujifunza, wakishindwa waombe ushauri.
10 YA JEZI ZINAZOUZA SANA ENGLAND:
1. Robin van Persie
2. Steven Gerrard
3. Luis Suarez
4. Eden Hazard
5. Mesut Ozil
6. Wayne Rooney
7. Sergio Aguero
8. Juan Mata
9. Shinji Kagawa
10. Frank Lampard
10 BORA BONGO KAMA WANGEKUWA MAKINI:
1. Coutinho
2. Paul Kiongera
3. Jaja
4. Amissi Tambwe
5. Mrisho Ngassa
6. Shabani Kisiga
7. Mwagane Yeya
8. Kipre Tchetche
9. Pierre Kwizera
10. John Bocco
0 COMMENTS:
Post a Comment