Na Saleh Ally
SIFA kubwa ya kocha Zdravko Logarusic
ni uwezo wa kazi, kila sehemu utakayouliza, kila mmoja alisifia mipango na
alivyotaka timu yake icheze.
Sifa hizo, kila ulipouliza au kuona
ziliharibiwa na mwenendo mbaya, ukorofi, kukashifu wafanyakazi wenzake na
dharau za waziwazi, lakini kuendekeza starehe kupita kiasi.
Simba wanajua, kwamba Loga alikuwa
anaendekeza starehe lakini wao wakaamini kuficha maradhi ni kitu chema, mwisho
wameumbuka na kifo. Usisahau, “mficha maradhi, kifo humuumbua”.
Tayari kuna tofauti au watu wanaona si
sahihi, kwamba kwa nini Loga ameondolewa? Wengi wanahoji kwa nini ameachwa mara
baada ya kufungwa mechi ya kirafiki dhidi ya Zesco? Wana haki ya kuhoji kwa
kuwa hawajui lolote na hawana muda wa kuchunguza.
Ukweli ni kwamba Loga alikuwa na
matatizo mengi na uchunguzi wa gazezi hili umebainisha hilo. Moja, ni
kuendekeza starehe na kufikia kusahau hata kazi yake. Mfano wiki moja
iliyopita, uongozi ulilazimika kumkalisha na kumsisitiza lazima afike mazoezini
badala ya kubaki kwake huku akipikiwa ugali na mwanadada wa Bongo Muvi halafu
kazi anamuachia msaidizi wake, Selemani Matola.
Kabla ya hapo, uongozi ulimuweka chini
na kumuonya kuhusiana na suala la kutukana wachezaji na baadhi ya wafanyakazi
wenzake. Usisahau hata wakati wa uongozi wa Ismail Aden Rage aliitwa na kuwekwa
chini.
Kibongo, wapo watu ambao hawafanyi
kazi vizuri bila hofu, huenda Loga alifanikiwa kuwasaidia baadhi ya wachezaji
ndani ya Simba. Lakini wanadamu tunapishana, wapo wanaotaka kuaminiwa na
waachiwe wafanye kazi si kuchungwa au kutukanwa kama watoto.
Loga amekwenda kwa amani, sasa anakuja
nchini Patrick Phiri raia wa Zambia, kocha ambaye si mgeni hata kidogo kwa soka
hapa nchini na kazi yake inajulikana.
Hakuna anayeweza kusema Loga alikuwa
mtu mbaya, mchangamfu, mcheshi lakini mengi alikuwa anakosea anapokuwa kazini,
hasa ujeuri, dharau na kutowajali wachezaji wake.
Sifa za Phiri ambaye ni mshambuliaji
wa zamani wa Nkana na timu ya taifa ya Zambia ‘Chipolopolo’, ni tofauti na
Loga, vigumu kumkosoa akiwa kazini au nje ya kazi. Mtulivu, msikivu, mng’amuzi
wa mambo, mbunifu na asiyependa bugudha zisizokuwa na ulazima wowote.
Kabla, ukizungumzia sifa za mafanikio
wala si suala la kuhoji kwa maana ya rekodi maana akiwa Tanzania, ametwaa
ubingwa wa Tanzania Bara mara mbili (2004-05) na (2009-10), msimu mmoja bila ya
kufungwa hata mechi moja. Amebeba ubingwa wa Tusker mwaka 2005. Akiwa na Zambia
alibeba makombe ya Cosafa na Cecafa, pia kushiriki Kombe la Mataifa Afrika.
Hili ni deni kwa Rais wa Simba, Evans
Aveva ambaye pia si mara yake ya kwanza kufanya kazi na Phiri ambaye hata ujio
wake umechangiwa na heshima aliyonayo kwa rais huyo wa Simba.
Phiri aliyewahi kuipeleka timu ya
taifa ya vijana ya Zambia katika Kombe la Dunia mwaka 1997 nchini Nigeria,
anakuwa deni kwa Aveva kwa kuwa ni kocha mwenye msimamo na anayetaka mambo
yaende kwa mpangilio na si kubabaisha.
Iwapo Simba itafanya mambo kwa
kubahatisha, basi ijue itamkosa mara moja, maana yake Aveva na uongozi wake, wana
deni la kuhakikisha mambo yake yanakwenda kwa mpangilio wa juu.
Kikubwa cha kukumbuka, Phiri naye ni
bindamu, ana upungufu wake katika sehemu kadhaa na huenda linapaswa kukumbukwa.
Upole:
Kweli ni mkimya sana, ingawa ni
maumbile, lakini amekuwa hapendi kusema au kufoka mambo yake yanapoharibiwa.
Ameifundisha Simba kwa vipindi vitatu
tofauti, safari hii anarejea ni mara ya nne. Mara mbili aliondoka kimyakimya
baada ya uongozi kumkorofisha.
Huenda angeweza kutatua tatizo kwa
kusema kinachomkwaza, yeye hakufanya hivyo. Hilo ni tatizo na Simba wawe makini
kabla hajaondoka tena kimyakimya, maana yake, hasubiri kufukuzwa.
Kurudi nyumbani:
Amewahi kusema kwao ni kama chifu,
hivyo matatizo mengi ya familia yanamhusu. Ndiyo maana haishi kurudi nyumbani kwenda
kuyatatua hata kama timu iko katika kipindi kigumu.
Akirejea nyumbani, kurudi kwake kazini
pia kumekuwa mbinde. Kuna wakati Simba walimsubiri kwa mwezi mzima akiahidi
kesho, keshokutwa, wiki ijayo lakini hakurejea.
Hilo pia ni vizuri akapewa taarifa
kwamba halifai na sasa mambo yamebadilika, hivyo kwa kuwa kazi anaiweza na
hakuna ubishi ni kocha wa kiwango cha juu, basi aipige bila ya konakona. Karibu
tena Bongo ‘Fundi’ Patrick Phiri.
0 COMMENTS:
Post a Comment