August 8, 2014

RAMA


Na Mwandishi Wetu
MTIHANI mkubwa kwa Kocha Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic, baada ya uongozi wa klabu hiyo kukamilisha mazungumzo na washambuliaji watatu wa kimataifa.


Washambuliaji hao watatu, wote wanachezea timu zao za taifa na Loga anatakiwa kuchagua mmoja tu ndani ya wiki moja.
 
KIONGERA (KULIA) AKIWA NA KIONGOZI WA SIMBA, IDDI KAJUNA MARA BAADA YA KUTUA DAR MARA YA KWANZA
Modo Kiongera ni raia wa Kenya ambaye kocha huyo hatapata shida kuhusiana na uwezo wake, Ousimanou Manneh raia wa Gambia ambaye imeelezwa anakipiga nchini Senegal na Jerome Ramatlhakwane raia wa Botswana anayekipiga TP Mazembe iliyomtoa kwa mkopo Don Bosco ya DR Congo.

Makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, amethibitisha ujio wa washambuliaji wote watatu ndani ya siku mbili.

“Baada ya kufika nchini, hiyo kazi tutaiacha kwa kocha na benchi lake la ufundi waamue mmoja ni yupi,” alisema Kaburu.

Nafasi za wachezaji wa kimataifa ni tano na tayari nne zimejazwa na Amissi Tambwe na Pierre Kwizerra (Burundi), Donald Musoti (Kenya) na Joseph Owino (Uganda).
 
MANNEH
Loga amesema kwake unaweza kuwa mtihani kweli, lakini atahitaji muda mchache kupata jibu.

“Waache waje, wakiwa hapa itakuwa ni rahisi kuamua kuhusiana na uwezo wao,” alisema kocha huyo raia wa Croatia na alipoulizwa kama hakutakuwa na upendeleo kwa Kiongera ambaye ndiye chaguo lake, alijibu:

“Hizo ni hisia za watu, lakini mimi nataka mshambuliaji mwenye uwezo wa kunifungia mabao, hivyo nitaangalia mwenye uwezo wa juu zaidi.”

Kiongera:
Ametimiza miaka 22, anachezea KCB na Harambee Stars, ana uwezo wa kupiga mashuti na mzuri wa mipira ya vichwa.

Loga amefanya naye kazi Gor Mahia ya Kenya na inaonekana ndiye chaguo lake namba moja, hata hivyo si tegemeo namba moja katika upachikaji mabao kwenye kikosi cha Harambee Stars.

Rama:
Umri ni miaka 19, Mazembe iliamua kumpeleka Don Bosco kwa mkopo, timu hiyo inamilikiwa na mtoto wa Moise Katumbi, mmiliki wa TP Mazembe.

Kaichezea timu ya taifa ya Botswana mechi 37, kafunga mabao 20, moja likiwa dhidi ya Taifa Stars, Julai Mosi, mwaka huu, Deo Munishi ‘Dida’ akiwa langoni na Stars ikalala 4-2.

Pamoja na kucheza kwao Botswana, amecheza pia Afrika Kusini katika timu za Santos, Vasco da Gama na Thanda Royal Zulu.

 Manneh:
Ana miaka 19, sifa yake ni vichwa na mashuti ya mbali, anatokea katika familia maarufu ya soka nchini Gambia ya Manneh.

Kaka zake wote watatu (Jerreh, Musa na Abdou Karim) ni wanasoka na walicheza katika timu moja ya Real de Banjul.

Manneh anayevutiwa zaidi na Cristiano Ronaldo wa Real Madrid, ni kati ya wachezaji makinda wanaokipiga timu ya taifa ya Gambia, hadi sasa bado hajawa tegemeo kwenye kikosi hicho cha taifa ingawa ana nafasi ya kucheza.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic