Wakati sasa ikiwa siyo siri tena juu ya wachezaji
wanaocheza soka kwenye Ligi Kuu ya Italia (Seria A) kulipwa pesa kiduchu, hali
ni tofauti nchini England.
England wachezaji wamekuwa wakilipwa kutokana
na uwezo wao, lakini kwa Italia hali ni tete na ndiyo sababu kubwa mastaa wengi
wanapakimbia kila kukicha.
Kutokana na hali hiyo, tuangalie wachezaji 10
kutoka England ambao wamekuwa wakivuta mkwanja mrefu msimu huu 2014/15.
10. John Terry
Nahodha wa Chelsea, John Terry, anakamata
namba 10 kwenye listi hii kutokana na kuingiza pauni 175,000 (sawa na Sh milioni
317 za Kitanzania) kwa wiki.
Ameitumikia klabu yake hiyo katika michezo 424
ikijumuisha michuano mbalimbali, huku katika kikosi cha Three Lions (England) akivaa
jezi ya nchi hiyo mara 78.
Nahodha huyo wa Blues anashikilia tuzo tatu za
kuwa beki bora wa mwaka wa EPL, vilevile ana Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa
ligi hiyo.
9. Mesut Özil
Mshika Bunduki huyu ambaye ameshinda Kombe la
Dunia 2014, ameingia katika orodha hii kwa kushika namba tisa kutokana na kuingiza
pauni 180,000 (sawa na Sh milioni 480 za Kitanzania) kwa wiki.
Özil ambaye alitua kikosini hapo mwanzoni mwa
msimu uliopita, pia ameweka rekodi ya uhamisho baada ya kutua kwa uhamisho wa
pauni 42.5 akitokea Madrid.
Japokuwa ameshindwa kufanya kama vile
ilivyotarajiwa na wengi, lakini huyu atabaki kuwa mmoja kati ya viungo makini
kwa sasa.
8. Eden Hazard
Kijana huyu mzaliwa wa Ubelgiji, ameshika namba
hii baada ya kuwa akikusanya pauni 185,000 (sawa na Sh milioni 499 za Kibongo) kwa
wiki.
Kiungo huyu aliyekuzwa na Klabu ya Lille ya
Ufaransa, ameaminiwa na Chelsea mpaka kupewa jezi namba 10 ambayo ilitumiwa na magwiji
kadhaa wa timu hiyo.
Kocha wake Jose Mourinho amemtabiria kinda
huyo kuwa atakuja kuwa mkali wa dunia kwa siku za baadaye.
7. Cesc Fabregas
Pasi zake murua ndizo zimemfanya arejeshwe
tena katika Jiji la London na timu ya Chelsea ambapo sasa anavuna pauni 200,000
(sawa na Sh milioni 540 za madafu).
Mchezaji huyo ambaye ni zao la akademi ya Barcelona,
La Masia, alitua jijini humo na katika umri wa 21 tu, akakabidhiwa unahodha wa
timu ya Arsenal.
Aliondoka klabuni hapo kwa shinikizo la kurudi
kwao ambapo licha ya kukaa kwa misimu kadhaa, hakuweza kung’aa kama mwanzo, lakini
kwa sasa swali lililopo ni kuwa, ataweza kupata mafanikio na timu yake mpya ya
Chelsea?
6. Sergio Aguero
Straika wa Manchester City, Sergio Aguero,
amekamata namba sita kutokana na kulipwa kiasi cha pauni 225,000 (Sh milioni
607 za Kitanzania).
Alipokuwa katika kikosi cha Atletico Madrid,
Agüero alitupia wavuni mara 74 katika michezo 175 kabla ya kutua City kwa pauni
milioni 38, sehemu ambayo amezidi kupata mafanikio na kushinda ubingwa mara
mbili.
Anakumbukwa kwa bao lake maridadi dhidi ya QPR
katika mchezo waliochukua ubingwa baada ya miaka 47 kupita, misimu miwili
iliyopita.
5. Robin van Persie
Kipaji chake kilianzia Feyenoord, pia ndiye
nahodha wa Uholanzi. Van Persie anaingiza kiasi cha pauni 225,000 kwa wiki
ambacho kinafanana na kile anachopata Sergio Aguero.
Straika huyo ilifikia wakati alikuwa roho ya
Arsenal kabla ya uhamisho wake kwenda Man United.
Sababu kubwa ya uhamisho huo ni kukimbia ukame
wa vikombe katika timu hiyo yenye maskani yake Kaskazini mwa London, hata hivyo
anabaki kama mmoja wa washambuliaji hatari duniani.
4. Yaya Toure
Huyu ndiye Mwafrika pekee katika listi hii
ambaye uwepo wake Man City unamfanya achukue pauni 240,000 (sawa na Sh milioni
648).
Yaya ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa katika
soka la Ulaya, alishacheza kwa mafanikio Barcelona, pia ameshacheza mara tatu michuano
ya Kombe la Dunia akiwa na kikosi cha Ivory Coast.
Kipaji chake cha kufunga, kupiga mipira ya
faulo na kukaba ndicho kinamfanya kuwa mmoja wa viungo hatari Premier League.
3. Radamel Falcao
Hapa kulikuwa na utata kidogo lakini ni rasmi
kuwa Falcao atakuwa akiingiza kiasi cha pauni 265,000 (sawa na Sh milioni 715)
kwa wiki.
Amesajiliwa kwa mkopo wa msimu mzima katika
dakika za lala salama na Manchester United kutoka AS Moncao, Falcao ni mmoja
kati ya wachezaji muhimu waliosajiliwa United.
Rekodi zake zinambeba baada ya kufanya vyema
huko nyuma na timu za Porto ya Ureno na Atletico Madrid ya Hispania.
2. Angel Di Maria
Huyu anakamata namba mbili baada ya kutua kwa Mashetani
Wekundu wa Manchester msimu huu, mchezaji huyo anaikamua klabu hiyo kiasi cha
pauni 280,000 (sawa na Sh milioni 756) kwa wiki.
Hakuna anayeweza kupinga Di Maria kulipwa
kiasi hicho kutokana na uwezo wake madhubuti wa kucheza soka ambapo aling’aa
mno msimu uliopita akiwa na kikosi cha Galaticos, Real Madrid.
Alishinda ubingwa wa La Liga na Ligi ya
Mabingwa. Ameshacheza zaidi ya michezo 100 katika kikosi cha Madrid, ndiyo
maana United wakakubali kutoa kiasi cha pauni milioni 59.7 kama ada ya uhamisho
wake.
1. Wayne Rooney
Nahodha wa England na Manchester United, Wayne
Rooney ndiye mchezaji anayelipwa zaidi Premier League, kwa wiki anaingiza mfukoni
pauni 300,000 (sawa na Sh milioni 810).
Amecheza mara 100 kwa kikosi cha England na
amefanikiwa kufunga mabao 41 kwa nchi yake na amecheza mara 300 kwa United na
kufunga 159.
Rooney ni kati ya wachezaji ambao wameweka
historia kwenye Premier League kutokana na kufunga bao bora la muda wote wakati
alipokuwa Everton walipocheza na Arsenal, ambalo mpaka kesho wakali hao wa Jiji
wa London hawawezi kulisahau.
Rooney ameshashinda ubingwa wa ligi, Ligi ya
Mabingwa na Mchezaji Bora wa Mwaka.
0 COMMENTS:
Post a Comment