Na Saleh Ally
IKIWA ndiyo asilimia 15 ya msimu wa Ligi Kuu
England imechezwa, tayari kuna mambo mengi sana yamejitokeza ambayo yanaonyesha
utakuwa ni msimu wenye kila aina ya mapya yatakayojitokeza.
Tayari mechi 58 zimechezwa kati ya 380 ambazo
zinatakiwa kuchezwa kwa msimu mzima wa Premier League kwa 2014-15.
Msimu unaonyesha mabao yaliyofungwa ni mengi,
wafungaji waliofunga mabao mengi hadi sasa ni wapya na wachache sana waliofanya
vizuri msimu uliopita.
Lakini idadi ya mabao yaliyofungwa na mchezaji
mmojammoja pia iko juu, hali inayoashiria ushindani na utamu zaidi wa mabao
kupachikwa kwa wingi kwenye msimu.
Mshambuliaji Diego Costa wa Chelsea ndiye
anaonekana kuwa matata zaidi katika upachikaji mabao baada ya kufunga nane
katika mechi sita za Premier League ambayo ilionekana ni ngumu kwake kwa kuwa
anatokea La Liga.
Maana yake kwa asilimia, Costa amepanda juu ya
100% kiufungaji na suala hapa linaloangaliwa ni kama ataweza kuendelea na kasi
hiyo au baadaye mabeki watamtuliza.
Wageni:
Baada ya mechi sita, chati ya wanaoongoza kwa
kupachika mabao inashikiliwa na wageni zaidi ambao wanaongozwa na Costa mwenye
mabao hayo nane.
Unaweza kusema wageni wameiteka ‘nchi’. Hadi
sasa inaonekana wengi wao si wale waliofanya vizuri msimu uliopita au
hawakuwepo England.
Jose Ulloa wa Leicester ana matano, Graziano
Pelle wa Southampton ana manne sawa na Nacer Chadli wa Tottenham na Sergio
Aguero (Man City).
Hii inaonyesha hadi sasa wageni ndiyo wanashika
chati ya juu zaidi ya wafungaji bora huku wale wakali kama Wayne Rooney na
Robin van Persie wakiwa wanachechemea lakini hawako mbali kwa kuwa mmoja ana
mabao mawili na mwingine matatu.
Wastani:
Tayari mabao 164 yalikuwa yamefungwa kabla ya
mechi za jana Jumapili na leo. Hadi sasa wastani wa idadi ya mabao uko juu
sana, kwani unaonyesha kuna asilimia 2.83. Kimahesabu ni hivi, katika kila
mechi iliyochezwa, tayari wastani wake ni mabao matatu.
Kama ni mabao matatu kwa kila mechi na mechi
kawaida hupigwa ni 380, kuna uwezekano wa kufungwa mabao 1,140, lakini kwa
kawaida lazima yatapungua, kwa hali inavyokwenda, inaonekana hayatashuka chini
ya 1000.
Penalti:
Inaonekana hadi mechi sita kwa kila timu
zimechezwa na idadi ya penalti si nyingi sana kwani ni asilimia 4.3, idadi
ambayo ni ya chini.
Idadi ndogo ya mabao ya penalti na idadi kubwa
ya mabao ya kufunga inaonyesha kiasi gani uwezo wa kufunga mabao bila aina hiyo
ya adhabu uko juu.
Mwisho:
Ukitaka kujua ligi bado ni ngumu, angalia namna
mabao yanayofungwa katika dakika za mwisho. Kwamba kila upande unakuwa
haukubali hadi hatua za mwisho.
Tangu kuanzishwa kwa ligi hiyo inaonekana kuna
wastani mkubwa wa mabao yaliyofungwa baada ya dakika 80. Hadi sasa katika mechi
hizo chache, inaonyesha kuna wastani wa mabao asilimia 16 yamefungwa dakika 10
za mwisho.
Nyumbani & ugenini:
Idadi ya mabao kuwa juu pia imeongeza ugumu
katika mechi za nyumbani na ugenini. Inaonekana ushindi wa mechi za nyumbani
wastani wake ni 31%, ushindi wa ugenini ni 33% na sare ni 36%.
Hii inakuonyesha ligi hiyo haina mwenyewe kwa
kuwa ushindi wa ugenini unaonekana uko juu kuliko nyumbani. Maana yake timu
zimepoteza mfululizo nyumbani na hii inathibitisha ugumu wa ligi hiyo.
Hata hivyo, unaweza kusema ni mapema kwa kuwa
ligi inaweza kuwa na mabadiliko kutokana na makocha, makipa, mabeki, viungo na
washambuliaji wanavyobadilika na kutokana na makosa wanayoyafanya.
Inawezekana washambuliaji wakafunga mabao mengi
zaidi au mabeki wakawa imara na kupunguza idadi ya mabao yanayofungwa
wakishirikiana na makipa na viungo wakabaji.
Raha ya ligi hiyo ni kuendelea kuangalia,
lakini wiki hizo sita, tayari zimeonyesha kuwa kuna harufu ya ushindani wa juu
zaidi kuliko misimu mingine iliyopita.
0 COMMENTS:
Post a Comment