SIKU mbili zilizopita,
Kocha Mkuu wa Manchester United, Louis van Gaal aliamua kufanya kitu ambacho
huenda kimewashtua watu wengi sana, lakini unaweza ukawa ni msimu wa kuinuka
kwa kikosi hicho.
Manchester United imefanya
usajili mzuri hadi dirisha linafungwa, imeibua idadi ya washambuliaji na viungo
bora kama Angel di Maria na Radamel Falcao ambao hakuna shaka watatoa msaada
mkubwa.
Bado pamoja na hayo, Kocha
van Gaal ametangaza amri mpya ambayo haikuwahi kufanyika hapo awali. Kwamba
kila siku moja kabla ya mechi, wachezaji watakabidhisha simu zao zote kwa
uongozi.
Hiyo itakuwa ikifanyika usiku
wa kuamkia kwenye mechi! mastaa wote watalazimika kukabidhisha simu zao kwa
uongozi na kingine amesisitiza chakula cha mchana ambacho wamekuwa wakila saa 7
mchana, kitajumuisha timu yote, yaani timu kubwa na zile za vijana, full stop!
Inawezekana katika hali ya
kawaida, mtu anaweza kufikiria kwamba jambo hilo lingependeza zaidi kufanyika
katika vikosi vya timu za Tanzania ambako wengi wamekuwa wakililia uhuru kama
wa Ulaya.
Wachezaji wa Tanzania
hawapendi kubanwa wakiamini Ulaya hawabanwi na bado wanafanya vizuri. Wanaamini
ni watu wazima na kubanwa kunawafanya wasiwe huru badala yake wanataka wapewe
uhuru kwa kuwa wanayajua majukumu yao.
Makocha kadhaa hasa wale
kutoka Ulaya wamekuwa wakikwama Tanzania kutokana na kuwaacha wachezaji wawe
huru kabisa na mwisho wanawaangusha wao kwa kuwa wanautumia vibaya uhuru
wanaopewa.
Mara ngapi tumewalaumu
makocha wanaowawapa wachezaji uhuru kupindukia, kweli wanakuwa na nia nzuri
lakini wachezaji ndiyo wanashindwa kuwa waelewa kutokana na wanachopewa. Timu
ikianguka, anayepewa lawama zote, inakuwa ni kocha.
Wachezaji walio Manchester
United hauwezi kusema hawajui suala la kuwa ‘professional’, lakini van Gaal pia
hawezi kuwa mwendawazimu, maana yake ameona jambo na anataka mabadiliko ndiyo
maana ameamua kutikisa.
Alichokifanya huenda kisiwe
cha kudumu, lakini ametuma salamu kwa wachezaji kwamba yeye ndiye ‘mwenye nchi’
na ameamua kufanya hivyo akitaka kila mmoja wao kuweka akili na nguvu zake
kwenye kila mchezo ulio mbele yake.
Maana yake hivi, van Gaal
anataka Manchester United ianze kushinda na si hadithi kama ambavyo mambo
yamekuwa yakitokea. Anajua presha kubwa iko mbele yake kwa kuwa Man United ndiyo
iliyofanya usajili ghali zaidi kuliko klabu nyingine yoyote msimu huu.
Pia imempata kila
iliyemtaka kuanzia katika beki, kiungo hadi washambuliaji. Hivyo van Gaal
hawezi kuwa na lolote la kujitetea zaidi ya kuwaridhisha mabosi wake wa
Manchester United na ushindi.
Uwezo wa wachezaji alionao
hauna maswali, ni bora na unakubalika duniani kote. Kwa nini ushindi ni tatizo?
Ndiyo ameona suala la kuweka nguvu na akili nyingi kwenye mchezo zimepungua na
inawezekana ameona ushiriki wa wachezaji wake kwenye mitandao ya kijamii kama
Twitter, Facebook na Instagram unavyokuwa juu licha ya wao kutofanya vizuri.
Uamuzi wa ujasiri wa van
Gaal unatufunza kwamba kocha anaweza kuwa na mbinu nyingi za ushindi na kocha
huyo Mholanzi anataka kuwaonyesha wachezaji yeye ndiye bosi, mwenye uwezo wa
kuongoza mapambano ya timu kupata ushindi, hivyo hakuna mjadala kwenye
kumsikiliza.
Maana yake hivi,
itakapotokea mwalimu anapambana na wachezaji wasio na nidhamu, si kwa lengo
binafsi na badala yake ili kukisaidia kikosi chake, viongozi wanapaswa kuungana
naye.
Hapa nyumbani imekuwa
tofauti kidogo na kunapotokea kocha anapanga mikakati fulani ambayo inawaudhi
wachezaji, viongozi hutengana na wengine wakawaunga mkono wachezaji kwa kuwa ni
washkaji au vipenzi vyao bila ya kujali maslahi ya timu na klabu.
Van Gaal ametoka Ulaya na
kurudi Afrika, kwamba kumbe bado tabia za wachezaji hazipishani sana na
ikiwezekana wakati mwingine wanapaswa kuchungwa. Angalia, Ulaya nao
wanachungwa, vipi nyumbani kwetu!
0 COMMENTS:
Post a Comment