Na Saleh Ally
PAMOJA na Manchester United kufanya usajili ghali zaidi kwenye Ligi
Kuu England ikiwemo kumsajili mshambuliaji nyota Ramadel Falcao, bado gumzo
kubwa la usajili limeangukia kwa Danny Welbeck.
Welbeck, 23, ametua Arsenal akitokea Manchester United kwa uhamisho
wa pauni milioni 16 na ndiye anaonekana kujadiliwa zaidi.
England kunaweza kuwa mbali zaidi, mashabiki wa soka hapa nyumbani
Tanzania wamekuwa wakijadili kama kweli Welbeck anastahili kucheza Arsenal.
Wako wanaoona kama Wenger hakuwa na sababu ya kumtwaa kwa kuwa kuna
Olivier Giroud na Yaya Sanogo.
Hata hivyo kwa Wenger, Giroud ndiye atakuwa mshindani mkubwa wa
Welbeck, lakini sasa ni majeruhi.
Kama wote wakiwa fiti, unaweza kujiuliza Wenger atakuwa katika
nafasi ipi na yupi hasa atampa nafasi ya kuanza.
Usisahau, wakati Giroud anaumia na kulazimika kukaa nje hadi
mwakani, aliipa Arsenal bonge la bao la kusawazisha dhidi ya Everton.
Pamoja na yote kila mmoja ana aina ya uchezaji wake, kiasi Giroud ni
mgumu anayeweza kucheza kama mshambuliaji wa kati tu, lakini Welbeck kidogo
atakimbia na mpira kama kiungo, ingawa hatatakiwa kufanya hivyo sana kwa kuwa
Arsenal ina watu kama Santi Cazorla, Theo Walcott, Alex Oxlade-Chamberlain,
Alexis Sanchez na Mesut Ozil.
Takwimu zao zilizopita, zinaweza kuchangia Wenger aamue nini, ingawa
ufanisi wao kila watakapopewa nafasi linaweza kuwa jibu sahihi,
Mechi & mabao:
Tokea alipotua England akitokea Montpellier ya Ufaransa, msimu wake
wa kwanza Giroud alipiga mabao 11 katika mechi 34. Msimu uliofuatia akaongeza
kwa kupiga 16 katika mechi 36.
Maana yake mabao yake 27 katika dakika 5,477 alizoichezea Arsenal ni
wastani wa bao moja katika kila dakika 195.6.
Rekodi ya Welbeck ni mechi chache na dakika chache zaidi, kwa kuwa
misimu miwili amecheza mechi 54, aikiwa ameanza kwa asilimia 50 ya mechi hizo
na amefunga mabao 10.
Amefanikiwa kucheza jumla ya dakika 2,791 ukiwa ni wastani wa dakika
279.1 kwa bao.
GIROUD
WELBECK
Mechi 72 mabao 28
Mechi 54 mabao10
MASHUTI:
Kwa umaliziaji, wote si wabaya sana ingawa si wa kiwango cha juu
hadi kuwaita hatari.
Katika suala la kupiga mashuti na kulenga lango, kwa misimu miwili
iliyopita, Welbeck akiwa na Man United amepiga mashuti 60 yaliyolenga lango,
huku akiwa nafasi chache ya kucheza kwa kuwa kuna Wayne Rooney na Robin van
Persie.
Giroud aliyekuwa na nafasi ya kutosha kucheza, amepiga mashuti 182
ambayo ni mara tatu ya Welbeck
Ukiweka wastani wa mechi alizocheza kila mmoja na mashuti aliyopiga,
inaonekana Welbeck ana ubora zaidi kwa kuwa wastani wake ni 16.7, wakati Giroud
ana 15.4.
NAFASI:
Giroud ni mkali zaidi katika utengenezaji wa nafasi, akiwa na
Arsenal ametengeneza nafasi 72 kwa wachezaji wengine wa Arsenal na 11 kati ya
hizo zimezaa mabao.
Welbeck ametengeza pasi 36 ambazo ni nusu ya Giroud na kusababisha
mabao matano.
Kwa umri wake na mechi alizocheza, Welbeck ana nafasi ya kufanya
vizuri Arsenal hasa kulingana na aina ya uchezaji wao.
Safari hii hatalazimika kukimbia zaidi na mpira, badala yake kutafuta
nafasi tu ili afunge kwa kuwa mafundi wamejazana, mfano Ozil, Cazorla na
wafanya ‘fujo’ kama Chamberlain na Sanchez.
Wakati Giroud anasubiri hadi mwakani kurejea dimbani, hii ni nafasi
kwake kwamba anaweza na Mfaransa akirejea dimbani, aanze kazi ya kusaka namba.
SOURCE:
CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment