Mwanzoni mwa miaka ya 2000, hadi kufikia 2010 Simba ilikuwa moja ya
klabu gumzo nchini, Afrika na kwingineko.
Jina lake lilijenga imani kwa timu nyingi za Ulaya na hata nchi za
Sweden, Norway na nyingine zilizo Kasikazini mwa bara hilo.
Ingawa kuna baadhi ya wachezaji wa Tanzania kama Yusuf Macho walipata
nafasi ya kunusa Afrika Kusini, Matola ndiye mchezaji pekee wa Simba
alisajiliwa na SuperSport United ya nchini huo bila ya kufanya majaribio hata
kidogo.
Kocha Pitso Mosimane wa SuperSport United ambaye baadaye alikuja kuwa wa
Bafana Bafana alimuona Matola wakati Simba ikiiadhibu Asante Kotoko ya Ghana
kwa mabao 4-2 katika mechi ya Kombe la Tusker mjini Nairobi, Kenya.
Moja kwa moja akanyoosha mkono na Matola akafunga safari kwenda Afrika
Kusini ambako alianza moja kwa moja. alikipiga kwa msimu wa 2005/2006 hadi
majeraha yalipoanza kumuanfama.
Kwa sasa ni kocha msaidizi katika timu ya wakubwa ya Simba hakika Matola
anaamini kuwa Simba inaweza kurudi kwenye enzi zake baada ya hivi karibuni
kupoteza mwelekeo.
Matola, aliyezaliwa mwaka 1978, alikuwa miongoni mwa viungo wakabaji makini
hususan miaka 2004 hadi na 2006, kiwango kilichoitoa udenda Super Sport United.
Matola, anasema ;
"Tuna kazi ngumu kuirudisha Simba yenye heshima yake".
Matola amesema hadhi ya timu hiyo imeshuka kwa kiasi kikubwa lakini hii
yote imesababishwa na uongozi mbovu pamoja na wachezaji kutokuwa na uzalendo na
timu yao, badala yake wapo kimaslahi zaidi, kitu ambacho enzi zao walikuwa
wakijituma kwa hali na mali kutetea heshima na hadhi ya klabu, ndiyo maana
Simba ilikuwa moto wa kuotea
mbali.
Lakini zaidi ya kujituma, mwisho wa siku inakuwa faida ya mchezaji
mwenyewe kwani, kufanya vema kwake ndiyo tiketi ya kujitanua zaidi katika soka
la kimataifa, ambalo limekuwa ni ndoto ya kila mchezaji hapa nchini.
“Ni dhahiri, Simba ya sasa
imepoteza muelekeo, hii sio kawaida ya Simba kumaliza misimu mitatu, minne bila
kushiriki michuano ya kimataifa. Ilikuwa ikikosa ni msimu mmoja tu, iwe klabu
bingwa ya Kombe la Caf, lakini si katika hali kama ya miaka hii.
“Tuna kazi ngumu ya kurudisha heshima ya timu yetu, kuanzia usajili hadi
uwanjani, tunapigana na mwalimu (kocha Loga ambaye ametimuliwa) kujaribu
kuibadilisha Simba ili iwe Simba ya kimataifa. Angalia ni msimu wa ngapi sasa, hatujashiriki michuano ya kimataifa. Lakini mwisho wa
yote tunataka kuhakikisha tunaijenga upya Simba yetu,” alisema kocha huyo
aliyeipa ubingwa Simba B mwaka 2012, katika michuano ya Benki ya ABC.
Mara ya mwisho Simba kushiriki michuano ya kimataifa ilikuwa 2012, baada
ya kutwaa ubingwa msimu 2011/12, ambapo misimu miwili mfululizo imeikosa michuano
hiyo, huku msimu 2013/14 ikimaliza nafasi ya nne, nafasi ambayo si rafiki na
heshima ya timu.
“Sikumbuki mara ya mwisho Simba kushika nafasi ya nne, lakini yote kwa
yote sababu kuu mbili zilihusika. Kwanza uongozi haukuwa ‘serious’ katika
kuimarisha kikosi, pili ni wachezaji kutokuwa na uzalendo na timu yao, badala
yake wapo kimaslahi zaidi. Enzi zetu, tulicheza kwa kujituma, kuifia timu maana
tulijua faida yake baadaye, ambayo ‘automatically’ ni kupata dili katika klabu
kubwa nje ya nchi.
“Kuna wachezaji waliokwenda kucheza soka la kulipwa, au kufanya
majaribio nje, hii yote ilitokana na juhudi zao uwanjani, hiyo ndiyo ilikuwa
siri ya mafanikio kwa Simba yetu pamoja na wachezaji.
Tofauti na sasa, wachezaji hawana moyo wa dhati wa kuitumikia timu, matokeo
yake ndio kama haya, ya kushika nafasi ya nne,” aliongea kwa uchungu Matola.
Matola, alisajiliwa na Super Sport msimu wa 2005/6 ambapo kabla ya hapo,
nyota wengine Ulimboka Mwakingwe na Shaaban Kisiga waliwahi kuhusika kutakiwa
na timu hiyo, lakini mwisho wa siku Matola ndiye alifanikiwa.
Matola anasema, mbali na kufanikiwa kwake, lakini alikumbana na
changamoto mbalimbali.: “Siri ya mafanikio ni kujituma mazoezini pamoja na
kujiamini, tofauti na hapo nisingeweza kucheza soka Afrika Kusini.
Kikosi chetu kilikuwa na
upinzani wa hali ya juu kutokana na kwamba, wenzetu wanaangalia zaidi wachezaji
wanaojituma uwanjani, hata wazawa pale walikuwa ni watu wa kupigana kufa kupona
mazoezini, maana walifahamu ushindani ulikuwa mkubwa. Hawakuangalia uzalendo
wala nini, ni juhudi binafsi za mchezaji uwanjani, ndiyo maana niliweza kucheza
soka pale,” alisema Matola.
0 COMMENTS:
Post a Comment