KILA mtu anaweza kuwa na hisia zake,
mawazo yake na hata uamuzi wake wa mambo. Lakini mwisho, ukweli wa mambo ndiyo
jawabu la mwisho.
Kuweka hisia zako hadharani ni jambo jema
na vizuri kama ukasimamia unachokiamini kuliko kuwa mwoga kwamba kuna watu
fulani wanaweza wasifurahie.
Si vibaya kusema viongozi wa Simba, watani
wao Yanga ni wale wasiotaka kutumia nguvu nyingi pia kuinua vipaji vya hapa
nyumbani.
Inawezekana wako wanaoamini kuwa wanapita,
hivyo hawana sababu kubwa ya kufanya juhudi kuinua vipaji, badala yake wanaweza
wakawa wananunua tu na kulahisiha mambo.
Wakati mwingine ni aibu, wakati mwingine
inakera na hasa suala la mzozo wa usajili ambalo linahusisha mchezaji mmoja tu
tena si raia wa Tanzania.
Ukiuliza anatokea wapi, jibu ni Uganda.
Tofauti yake na wachezaji wa Tanzania ni ipi, lazima majibu yatakuwa yanayumba.
Labda basi tuulize, Okwi ameipeleka wapi Uganda, yaani The Cranes, hakuna
tofauti na Tanzania!
Sasa ubora wa Okwi ni nini? Wakati
mwingine utaona Yanga walifanya kila linalowezekana kumpata lakini zaidi
ilikuwa ni siasa tu kwa kuwa walilenga kuwakomoa Simba.
Uliza Yanga, kwamba Okwi aliwasaidia nini.
Hakuna kwa kuwa hakucheza hata mechi saba za ligi, pia akafunga bao moja tu.
Yeye na Mrisho Ngassa au Hussein Javu, nani alikuwa na msaada utapata jibu.
Wakati Okwi hakuwa na msaada Yanga, vipi
leo Simba wanamchukua kwa mbwembwe na wanaonekana kufurahia sana. Jibu ni
lilelile kama la Yanga, kwamba wanataka kuwaudhi Yanga lakini ukweli hakuwa
kwenye mipango yao na sasa ni patapotea kama kweli atakuwa kwenye kiwango chake
au la.
Yote yanawezekana, huenda akacheza vizuri
na kuwa msaada kwa Simba, lakini kuna haja ya kujiuliza atakuwa msaada kwa
kipindi gani na ataisaidiaje Simba kufanya vizuri kwa kuwa amekuwa ana matatizo
yasiyobadilika kama kuomba ruhusa, kwenda kwao, baadaye akachelewa kurejea.
Tunajua utovu wa nidhamu kama kupata kadi
zisizokuwa na ulazima kama vile msimu mmoja kabla ya kuondoka kwenda Etoile du
Sahel ya Tunisia ambayo hadi leo inadai ni mchezaji wake na inadaiwa na Simba.
Okwi, Okwi, Okwi. Hivi ni nani hasa? Uwezo
wake ni kweli una tofauti kupindukia na wachezaji wa hapa nyumbani?
Vipi anawaendesha hivi viongozi wa klabu
kongwe za Tanzania ambazo zina umaarufu na uwezo mkubwa hata kuliko za kwao
Uganda. Au kwa kuwa viongozi hao wanataka sifa tu, wanataka kufurahisha
mashabiki wao bila ya kujali uzalendo au kufanya mambo kwa kuangalia maisha
marefu ya baadaye ya klabu zao?
Hawafanyi hivyo kwa kuwa wanajua baada ya
muda wataondoka? Je, Okwi ataendelea ‘kunyanyasa’ anavyotaka hadi lini au kwa
kuwa anajua hapa Tanzania ndiyo sehemu unaweza ‘kutesa’ unavyotaka!
Hii si sawa, kwa yoyote anayesoma makala
haya, akiondoa ushabiki na kutafakari atagundua Tanzania kupitia viongozi wa
Yanga na Simba wakiwa wamefungua macho wanaweza kubadili njia na kuepuka kupita
kwenye barabara ya kuwagombea akina Okwi kwa kuwa si lazima.
Tupeni fedha zenu nyingi kwenye timu za vijana na kwa asilimia
kubwa itawasaidia kuachana na mizozo na ‘vizogo’ vya akina Okwi ambao hawana
tofauti hata kidogo na wachezaji wa hapa nyumbani ambao hamuwapi vipaumbele!
0 COMMENTS:
Post a Comment