Na Saleh Ally
MAFANIKIO ya mshambuliaji
mpya wa Chelsea, Diego Costa yanaonekana kwenda haraka sana kwa kasi ya
kimondo.
Costa, raia wa Hispania,
tayari amefanikiwa kufunga mabao saba katika mechi nne tu alizocheza za Ligi
Kuu England.
Wakati anaondoka Atletico
Madrid kwenda kujiunga na Chelsea, wengi waliamini hawezi kutamba kwa kuwa
alikuwa anatokea kwenye ligi laini.
Ilionekana La Liga ambako
aliwatoa jasho Cristian Ronaldo wa Real Madrid na Lionel Messi wa Barcelona ni
laini si kama England.
Lakini sasa tayari
kawashitua wengi, mechi nne bao saba tena England. Maswali yanaanza kuibuka na
moja ni kweli uwezo huo utaendelea au ni nguvu ya soda?
Maswali yanaweza kuwa mengi
lakini majibu yake yanataka subira kwa kuwa yatajibiwa na mechi zinavyoendelea.
Hakuna suala la utabiri wala
ubashiri lakini kila mechi inapochezwa, majibu yatapatikana.
Kizuri ambacho kinaonyesha
moto wa Costa hauwezi kuzimika kirahisi ni mambo matatu makubwa.
Ufundi mwilini:
Mabao saba aliyofunga, yanaonyesha
kuwa Costa ni mjuzi na si rahisi kupunguza kazi kwa kuwa amepata jumla ya
nafasi 12, kati ya hizo amefunga saba.
Huo ni wastani wa zaidi ya
asilimia 73 ya matumizi bora ya nafasi, maana yake ni mshambuliaji hatari zaidi
kuliko wote hadi sasa katika Premier League.
Kushusha wastani kama
atapata nafasi nyingi halafu akazipoteza, lakini hadi sasa, hakuna mjadala.
Silaha tatu:
Lakini bado inaonyesha ni
mchezaji bora sana kwa kuwa tayari ametumia silaha zote tatu kufunga mabao hayo
saba.
Mshambuliaji yeyote hatari,
lazima atakuwa na silaha tatu hatari na inategemea, kama ataweza kuzitumia
zote, basi atakuwa ni tishio.
Mguu wa kulia, wa kushoto
na kichwa. Costa anaonyesha za kwake zote zimefanyiwa ‘service’ ya uhakika na
ziko safi kufanya kazi kwa kuwa zote zimeishatumika katika hayo mabao saba.
Kukamilika:
Hakuna ubishi kweli Chelsea
imekamilika vilivyo kwenye kila idara, ukianza mabeki, viungo na washambuliaji.
Suala la kipa, halina ubishi wanao wa uhakika.
Ukizungumzia wachezeshaji
kwa maana ya viungo, Chelsea wako sawa sana na wanajumuisha vijana wengi na
wakongwe watundu.
Uhakika unapokuwa na mtu
kama Cesc Fabragas ambaye anacheza timu ya taifa na Costa, lakini Eden Hazard,
Oscar na Nemanja Matic, wote ni wale wanaoweza kutengeneza kitu kwa uwezo
binafsi na si maelekezo ya kocha pekee.
Yote haya yakiwa kwenye
kiwango cha juu, yataendelea kumfanya Costa afanye kazi yake vizuri ambayo
itakuwa ni kucheka tu na nyavu.
Ataendelea au la, vyote
vifanye kazi kwa pamoja na kuomba majeraha yasimkute lakini kikubwa cha
kujiuliza, mabeki ‘wakatili’ wa England, watakubali kirahisi?
Aina ya Costa ni watu
wasiokubali kushindwa kwa kujitahidi kila kukicha na hilo ndiyo linambeba.
Mabao yake pia yameonyesha
kuwa ni hatari zaidi kwa mabeki wa England kwa kuwa amefunga kwa kupiga chenga,
kuunganisha, kufunga mbele ya mabeki pia kwa shuti kali. Vyote ameweza.
Mwisho usisahau, kama
ataendelea kufunga ndani ya mechi kumi zijazo, huenda ikawa ndiyo tiketi ya
Mhispania mwenzake, Fernando Torres kupigwa bei kabisa kwa kuwa sasa anacheza
AC Milan kwa mkopo.
0 COMMENTS:
Post a Comment