September 15, 2014




Na Saleh Ally
WAKATI Ryan Joseph Giggs anacheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu England mwaka 1990, Wayne Rooney alikuwa na miaka mitano tu, akiongozwa na wazazi wake.


Mwaka huo Gazeti la Championi lilikuwa halijaanzishwa, wahariri wake wote akiwemo Saleh Ally walikuwa hawajaanza uandishi hadi sasa ndiyo gazeti bora la michezo Tanzania!

Giggs amecheza Ligi Kuu England kwa miaka 24, tena timu moja tu ya Manchester United ambayo alijiunga nayo akiwa kinda akitokea Manchester City baada ya Alex Ferguson kufanya kazi ya ziada kumshawishi mama yake.

Asili ya Giggs ni Bara la Afrika katika nchi ya Sierra Leone, ndiye mchezaji mwenye rekodi lukuki za Ligi Kuu England pia kwa wanasoka kutoka Uingereza.

Yuko kwenye Muungano wa Uingereza (Great Britain) kwa kuwa anatokea Wales, nchi ya asili ya mama yake mzazi na ndiye mchezaji gwiji zaidi sasa tangu kuanzishwa kwa Man United.

Rekodi zake ni kubwa na za juu zaidi kuliko zile za wachezaji wengine wote wa enzi hizo na sasa ukijumlisha akina Bobby Charlton, Denis Law hadi kizazi cha kina Steve Bruce na baadaye Eric Cantona.


Kufikia alichokifanya inabidi uwe mtu kweli kwa kuwa Ligi Kuu England ina ushindani wa juu sana, hivyo si rahisi kufanya aliyoyafanya yeye kwa kipindi chote hicho na leo ukimtupia uwanjani, pamoja na kwamba ana miaka 40, kazi utaiona.

Giggs ni mchezaji mwenye vionjo vingi zaidi kwa maana ya kasi, mvuto wa pasi, chenga kuliko mwingine yeyote aliyewahi kutokea kwenye Ligi Kuu England.

Kawaida haihesabiwi lakini inaaminika, Giggs ndiye mchezaji aliyewapita mabeki wengi zaidi kwenye Ligi Kuu England kwa maana ya kumtoka mmoja, wawili au watatu na kupiga krosi iliyozaa bao au kufunga bao.

Makombe:
Hakuna mchezaji anayefikia rekodi yake ya kutwaa makombe, amebeba 13 ya Ligi Kuu England, si kitu kidogo. Mbali na hivyo ameshinda makombe matatu ya FA.

Pia Giggs amebeba makombe ya ligi mawili na mawili ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Usisahau amekuwa kwenye kikosi cha Manchester United kilichofanikiwa kushika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu England, mara tano.

Nahodha & kocha:
Anaingia kwenye listi ya waliowahi kuwa tegemeo kwenye kikosi cha Man United, baadaye nahodha halafu kocha. Hii hufanyika kwa wachezaji wachache sana na hasa katika timu moja.

Giggs amekuwa tegemeo kubwa la Man United lakini msimu wa 2007-08 alichukua nafasi ya nahodha baada ya Garry Neville kuondolewa kutokana na kuwa majeruhi.

Hali kama hiyo ni nadra sana kutokea kwa wachezaji wengi wa soka kwa kuwa ushindani unakuwa uko juu kwa mchezaji kupata nafasi hizo.

Binafsi:
Tuzo za timu, ndiye anashikilia rekodi ya juu, lakini bado unaweza kumuingiza kuwa bora na mwenye kiwango cha juu kwa zile binafsi.

Ana rekodi ya kutwaa mara mbili mfululizo tuzo ya PFA (wachezaji wa kulipwa) vijana.

Alifanya hivyo mwaka 1992 na 1993 na kuwa mchezaji wa kwanza kufanikiwa kuibeba tuzo hiyo mara mbili mfululizo. Baada ya hapo hakushinda tena tuzo hiyo hadi alipokuja kuibeba ya wakubwa mwaka 2009.

Nyavu zake:
Rekodi zake zinaonyesha Giggs ni mtu tofauti na wachezaji wengine wengi na anayetaka kumpata, lazima afanye kazi ya ziada.

Hadi kufikia msimu wa 2012−13, Giggs alishikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyecheza na kufunga kwenye kila msimu wa Ligi Kuu England tangu mwaka 1991.

Msimu pekee aliofeli kufunga ni uliofuatia yaani uliopita na ndiyo aliostaafu. Hakuna mchezaji amefanya kama yeye.

Lakini usisahau, wakati anastaafu, Giggs alikuwa amebaki mchezaji pekee aliyekuwa anacheza Ligi Kuu England mpya wakati aliwahi kucheza ile ya zamani na mfumo wa kizamani. Ndiyo maana alichaguliwa kwenye timu ya karne ya PFA.

Asisti:
Asisti ni neno la Kiingereza, likiwa na maana iliyozaa bao au pasi ya mwisho kabla ya mfungaji kumalizia wavuni. Linatoholewa kuwa asisti, Giggs ndiye anayeongoza kwa kutoa asisti nyingi zaidi kwenye Ligi Kuu England tangu kuanzishwa kwake.

Giggs ametoa asisti 271 kwa timu yake ya Man United. Achana na kufunga mabao 114 katika mechi 672, ametengeneza kwa idadi hiyo ambayo hakuna kiungo mshambuliaji bora kila unayemjua anaifikia.

Sehemu moja:
Amekaa Man United tangu mwaka 1990, hakuna mchezaji aliyethubutu kufikia muda huo na mtu pekee ambaye anamzidi kwa kufanya kazi muda mwingi zaidi kwenye kikosi hicho ni Alex Ferguson tu.

Kocha huyo alitua Man United mwaka 1986 akitokea Aberdeen, maana yake anamzidi miaka minne tu. Kwa wachezaji hakuna anayefikia mziki wake wa kukaa muda mwingi kwenye timu moja, pia Man United.


Walimuacha:
Giggs ameachwa na wachezaji wengi sana na ambao walimkuta Manchester United.
Aliingia kama kinda, baadaye mkongwe na sasa ni kocha. Utaona hata kundi la akina David Beckham, Nick Butt, kina Neville ambalo lilijulikana kama Class of 1992, yeye ndiye mkongwe.

Giggs alikuwa ndiye kaka wa kundi hilo na wengi wao walimkuta, lakini mwisho wakaondoka na kumuacha. Wapo waliong’ara wengine wakapewa unahodha, lakini yeye akaendelea kubaki Man United, hadi leo.

Wapo ambao tangu wameondoka Man United wamecheza zaidi ya timu tano, lakini yeye ameendelea kuichezea timu hiyo kwa mafanikio makubwa.

Amecheza na wengi:
Ndiye anayeshikilia rekodi ya kukutana na wachezaji wengi zaidi kwenye sehemu mbili tofauti.

Kwanza akiwa Man United, kwa kuwa ameshindana namba na wachezaji wengi na pia wengi ameshirikiana nao akiwa klabuni hapo.

Pia kwenye Premier League, Giggs anashikilia rekodi nyingine ya kukutana na wachezaji wengi zaidi wa timu pinzani wakati akiwa na Man United.

Ikiwa na maana amekabwa mara nyingi zaidi na wachezaji wengi zaidi kuliko mchezaji mwingine wa Man United.


MAKOMBE 13 PREMIER LEAGUE:
1992-93, 1993-94, 1995-96, 1996-97, 1998-99, 1999-2000, 2000-01, 2002-03, 2006-07, 2007-08, 2008-09, 2010-11, 2012-13.


145 - Ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi za Ligi ya Mabingwa Ulaya.

632 - Ndiye aliyecheza mechi nyingi zaidi katika kikosi cha Manchester United kwenye Ligi Kuu England.

794 - Ndiye mchezaji aliyeanza mechi nyingi zaidi za kikosi cha Manchester United katika michuano yote.

100 - Ndiye mchezaji aliyefunga mabao 100 kwa mara ya kwanza kwa wachezaji wa Man United.

100 - Kiungo wa pili kuwa na mabao 100 katika Ligi Kuu England baada ya Matt Le Tissier wa Southampton.

1 - Ni mmoja wa wachezaji wanne tu wa Manchester United waliofanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, mara mbili. Wengine ni Paul Scholes, Gary Neville na Wes Brown.

WALIOCHEZA MECHI NYINGI PREMIER LEAGUE:

1. Ryan Giggs                  632
2. Frank Lampard             577
3. David James                 572
4. Gary Speed                   535
5. Gareth Barry                 529
6. Emile Heskey                516
7. Jamie Carragher            508
7. Mark Schwarzer            508
9. Phil Neville                    505
10. Sol Campbell                503


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic