Baada ya kumuacha katika kikosi cha timu hiyo
kilichocheza dhidi ya URA ya Uganda hivi karibuni, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick
Phiri, amemtuliza mshambuliaji wake raia wa Burundi, Amissi Tambwe na
kumhakikishia kuwa atapata nafasi ya kucheza.
Hali hiyo imemsikitisha Tambwe na kuanza
kuyaona maisha yake klabuni hapo kuwa machungu kama shubiri huku furaha yote
aliyokuwanayo msimu uliopita ikitoweka.
Mmoja wa
viongozi wa Simba ambaye aliomba kutotajwa jina lake, alisema kuwa baada ya
Tambwe kuonyesha kutofurahia hali hiyo, kocha Phiri alimwita na kuzungumza naye
na kuhakikishia kuwa atapata nafasi ya kucheza katika kikosi chake cha kwanza,
hivyo anatakiwa kutulia.
“Hali hiyo pia ilitusikitisha baadhi ya viongozi
lakini hatukuwa na jinsi lakini pia, baada juzi kocha Phiri kufika Mtwara,
alimwita Tambwe na kuzungumza naye.
“Alimtaka asiwe na hofu na aendelee kufurahia
maisha katika kikosi hicho kama ilivyokuwa zamani na atapata nafasi ya kucheza
kwa sababu ni mmoja wa wachezaji anaowategemea kwa ajili ya kuiongoza Simba
kufanya vizuri msimu ujao,” alisema mtoa habari huyo.
Tambwe kwa sasa hana uhakika wa namba katika
kikosi cha kwanza cha Simba kutokana na washambuliaji, Emmanuel Okwi na Paul
Kiongera kuonekana kuwa chaguo la kwanza la Phiri.
0 COMMENTS:
Post a Comment