September 19, 2014


Na Saleh Ally
KWA watu wa Afrika Mashariki, Southampton ya England ni moja ya timu maarufu sana kutokana na jambo moja.

Mkenya, Victor Wanyama anakipiga katika kikosi hicho. Hivyo wengi wamekuwa wakipenda kukifuatilia kila kinapokuwa inacheza.
Kwenye vitongoji mbalimbali vya jiji la Nairobi, timu hiyo imekuwa ikijikusanyia mashabiki kwa haraka sana na hata kufikia kuonekana ni biashara kwa wale ambao hufanya biashara ya kuonyesha mpira.
Lakini kwa sasa Southampton imekuwa maarufu zaidi duniani kote. Si timu ya siku hizi, lakini msimu uliopita imezua gumzo baada ya kuuza wachezaji watano wa kikosi cha kwanza.

Southampton imeuza wachezaji wake watano wa kikosi cha kwanza kwenye timu za Liverpool, Manchester United na Arsenal. Kitendo hicho kilizua hofu kubwa mashabiki wake wakiamini watakuwa wamejivuruga.
Southampton imekuwa moja ya klabu zilizoingiza kiasi kikubwa cha fedha kutokana na mauzo ya wachezaji, imepata pauni milioni 97, hiki ndicho wanachotaka viongozi.
Hapa nyumbani kabisa linalosifika kwa mipango ya biashara ni Wachaga. Unaweza ukawaita Southampton ni Wachaga wa England kutokana na walichokifanya msimu uliopita.
Wamekuwa gumzo dunia nzima kutokana na kuwaza beki Luke Shaw aliyetua Man United kwa  (£30million) na Calum Chambers (£16milioni) aliyejiunga Arsenal.
Adam Lallana (£25milioni), Rickie Lambert (£4milioni) na Dejan Lovren (£20milioni), wote wamejiunga na Liverpool. 
Mashabiki walionekana kupania, kwamba timu imeuza nyota kadhaa wakiwemo watano wa kikosi cha kwanza, hivyo wakaingia hofu. Wako walijipanga kusema uongozi umekosea kwa ajili ya kuusema.
Lakini baada ya kuanza kwa Ligi England, katika mechi nne walizocheza wamekuwa na wastani mzuri hata kuliko baadhi ya timu walizoziuzia wachezaji.
Walianza na kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Liverpool wakiwa ugenini, baada ya hapo wakapata sare ya bila mabao dhidi Wes Brom, wakiwa nyumba na kelele zikaanza.
Wakatoka nje ya kuwatwanga West Ham 3-1, halafu wakarejea nyumbani na kushinda kwa mabao 4-0 dhidi ya Newcastle.
Kelele zimezimika, huenda wako wanaosubiri kulaumu lakini ukweli uongozi wa Southampton umeonyesha kile kilichoonekana hakiwezekani. Kwanza timu isiyo na jina kubwa kama Man United au Arsenal. Imetengeneza wachezaji, ikawategemea na kuwauza.
Halafu baada ya hapo imeendelea kufanya vizuri. Maana yake imefanya biashara na kuendelea kufanya vizuri kisoka.
Huo ndiyo uongozi sahihi, huenda hata hapa nyumbani viongozi wanapaswa kujifunza wao kuongoza na kuonyesha mifano ambayo haijategemewa, badala wao kufanya wanavyotaka mashabiki au wanachama.
Siku zote wanachama wanataka kuburudika tu, viongozi wanataka fedha ili kuendesha klabu kwa mafanikio.
Mapinduzi hutengenezwa na viongozi imara kama wale wa Southampton ambao hata kama timu yao haitafanya vizuri sana, bado wao ni mashujaa kwa kuwa walisimamia wanachokiamini na kimefanya kazi.
Nyumbani Tanzania kunaweza kuwa mfano au sehemu nzuri ya kujifunza hilo hasa kwa viongozi wengi wa Yanga na Simba hufanya maamuzi kuwafurahisha tu mashabiki.
Mabadiliko mara nyingi hayaanzi kwa kufurahisha kama walivyofanya Southampton. Lakini watu waumie na wanaoamua kuyaanzisha lazima wawe jasiri kama walivyofanya viongozi hao wa Southampton.

TIMU ZILIZOONGOZA KWA KUUZA WACHEZAJI:
1. Southampton FC £97m
2. Real Madrid CF £89.4m
3. Chelsea FC £81m
4. Liverpool FC £80m
5. AS Monaco £76m
6. FC Barcelona £68.7m
7. FC Porto £67m
8. Atlético Madrid £58.2m
9. Sevilla FC £43m
10. Bayern Munich £39m
11. Real Sociedad £36.7m
12. AS Roma £36.7m
13. Benfica £34.3m
14. Valencia C£32.7m
15. Udinese £31
16. Tottenham  £30.3m
17. Athletic Bilbao £28.7m
18. Man United £27m
19. Hellas Verona £23m
20. Cardiff City £22.3m

MECHI ZA EPL ILIZOCHEZA:
Liverpool 2-1Southampton
Southampton 0-0 Wes Brom
West Ham 1-3 Southampton
Southampton 4-0 Newcastle




0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic