Na Saleh Ally
WALIPOFIKIA Alex Ferguson
na Roy Keane sasa panatisha, maneno makali, ya kibabe hali inayoonyesha
wakizidi, hata heshima walizonazo zitaporomoka.
Wanasoka wa Tanzania
wanaweza hivi? Kuingia kwenye utamaduni wa vitabu na kueleza ukweli wa kila
walichonacho?
Tunajua wenzetu Wazungu
wanaweza hilo, lakini safari hii kwa mara ya kwanza, kitabu kinachohusiana na
masuala ya soka kinazua malumbano makubwa kati ya magwiji wawili.
Ferguson aliyekuwa kocha
wa Manchester United tokea mwaka 1986, ndiye mwenye mafanikio makubwa kuliko
mwingine yoyote kama ilivyo kwa Keane ambaye ni nahodha mwenye mafanikio
makubwa zaidi.
Wote wawili waliwahi
kutoa vitabu, Ferguson alifikisha hadi vitano. Lakini baada ya kustaafu vizuri
na kwa mafanikio makubwa, akatoa cha mwisho ambacho alieleza mambo mengi
yakiwemo yanayowahusu baadhi ya wachezaji wake akiwemo Keane.
Katika kipengele cha
Keane (kwa wiki nne sasa kimekuwa kikielezewa kwenye magazeti ya Championi
Jumatano&Ijumaa), kinaeleza mengi likiwemo suala la nahodha huyo kutopenda
mafanikio ya wachezaji vijana.
Ferguson ameeleza Keane
alivyojisahau baada ya kumpa madaraka makubwa, akaeleza alivyoanza kumdharau
msaidizi wake Carlos Quieroz raia wa Ureno, alivyomfokea Ronaldo, Ruud van
Nisterlooy.
Lakini akaenda mbali
zaidi kwa kueleza alivyowashambulia wachezaji wa Manchester United kwenye
runinga ya klabu hiyo ya MUTV kwamba ni legelege, hali iliyosababishwa wazomewe
wakiwa Ufaransa kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika kitabu chake hicho
amewagusa hadi van Nistelrooy na David Beckham, akieleza walibadilika mwishoni
kama ilivyokuwa kwa Keane.
Inaonekana nahodha huyo
wa zamani ndiye pekee ameshindwa kuvumilia, amejibu mapigo na katika uzinduzi
wa kitabu chake juzi, mambo yalikuwa mabaya zaidi alipotoa maneno makali kwa
Ferguson na sasa ndiyo gumzo kwenye mitandao ya England.
Keane amesema:
“Nashangazwa sana na Ferguson kutoa kitabu na kuanza kuwashambulia watu
waliomba mafanikio, angalia alivyoingiza mamilioni ya fedha.
“Hiyo haitoshi,
Manchester wamempa jukwaa (kwenye Uwanja wa Old Trafford), wamempa na sanamu.
Lakini bado anawadharau na kuwasema vibaya waliompa nafasi hiyo ya mafanikio.
“Kawaida alikuwa ni mtu
anayependa kutukuzwa, kuogopwa na watu, lakini mimi sikuwa kati ya waliofanya
hivyo, ndiyo maana nasema sikutaka kuandika kitabu, lazima niwe mkweli lakini
nimeshindwa kuvumilia lundo la uongo wa Ferguson, ndiyo maana nimeamua kumjibu
na kufafanua ukweli ni upi.”
Ukiambiwa Ferguson ni
muongo unaweza kukubali? Ukisoma yale ya kwenye kitabu chake (kupitia gazeti la
Championi), unaweza kuamini kocha huyo anaweza kudanganya?
Vitu vingi alivyovieleza
kama lile la Keane kuwadharaulisha wachezaji wa Man United kwenye runinga au
kumtukana van Nistelrooy wakiwa vyumbani, ni kweli anaweza kudanganya wakati
kulikuwa na wachezaji na makocha wengine vyumbani? Maana Keane vyote ameeleza
ni uzushi na kuvifafanua tofauti kwenye kitabu chake cha Second Half.
Majibu ya Keane kwa
Ferguson yanaonyesha mambo mengi sana ambayo pia unaweza kuyarudisha kwenye
soka ya hapa nyumbani.
Kwamba kunapokuwa na
kundi kubwa la watu mfano wa timu, lazima ndani yake kunakuwa na mengi ambayo yamejificha
lakini chuki huchukua nafasi kubwa sana.
Angalia ulivyokuwa
unawaona Keane na Ferguson wakishirikiana kuisadia Man United kupata mafanikio
makubwa, kumbe ndani yake kulikuwa na chuki kuu miongoni mwao na ndani kabisa
ya mioyo yao.
Leo wanaweza kutoa mengi
kama hayo, wanaonyesha kuwa kwenye soka, unafiki ni sehemu ya maisha, huenda
hata hapa nyumbani imekuwa ikitafuna mafanikio ya klabu zetu, ingawa wamekuwa
wakijitahidi kufanya kila kitu kiwe siri.
Kwani mara ngapi umesikia
klabu zikikanusha habari za ndani ambazo hutolewa na watu wake wanapokuwa
wamechoshwa na jambo fulani? Pia jiulize, bila unafiki, ugomvi, kuchukiana,
mchezo wa soka hauwezi ukaenda.
Angaliea kwenye kitabu
cha Zlatan Ibrahimovic ambaye sasa yuko PSG. Ndani yake anaeleza mengi kuhusiana
na Pep Guardiola akisema hajawahi kuona mtu mwenye roho mbaya kama kocha huyo
wa sasa wa Bayern Munich.
Wakati huo walifanya kazi
wote Barcelona, yeye anamuita ni myama, shetani mwenye ngozi ya kondoo huku
akisistiza alitaka kuua kipaji chake.
Soka ni mchezo mzuri,
lakini unafiki ni nguzo yake? Kama Wazungu wanasifiwa kwa upendo au kuwa
wakweli au kutokuwa na roho za kwanini. Vipi hapa nyumbani, ndani ya timu zetu
kukoje? Hebu watu nao wafunguke tujifunze, acheni uoga!
0 COMMENTS:
Post a Comment