Na Saleh Ally
KAULI ya Roberto Mancini kuhusiana na mchezaji wake wa
zamani, Mario Balotelli inaweza kuwa dawa au sumu kwa mshambuliaji huyo.
Mancini raia wa Italia ambaye amekuwa kimya
muda mrefu ameibuka na kusema, Balotelli anapaswa kutambua Liverpool itakuwa
nafasi yake ya mwisho.
Kocha huyo aliyeipa Man City ubingwa wa
England baada ya zaidi ya miaka 40 akiwa na Balotelli, amesema ni wakati wa
Balotelli kuonyesha alichonacho, la sivyo ataanza kuporomoka kwa kasi.
Mwendo wa Balotelli tokea atue Liverpool
umekuwa ni wa kusua, tofauti na wengi walivyokuwa wakitegemea kutokana na uwezo
wa kucheza alionao.
Mambo yamekuwa tofauti, ugumu wa mambo
umeongezeka na tayari ile presha ya Kingereza imeanza juu yake.
Hoja kubwa kwa kuwa hajafunga mabao, bora
Liverpool ingemtumia Rickie Lambert ambaye licha ya kutokea benchi amekuwa
akifanya vizuri zaidi.
Achana na hivyo, Waingereza wana uwezo
mkubwa wa kutengeneza presha, wamemhamishia Balotelli hadi kwenye suala la bei,
kwamba alinunuliwa kwa pauni milioni 16 kutoka AC Milan sawa na zile
alizonunuliwa Danny Welbeck akitua Arsenal kutoka Man United.
Wanasema Welbeck amekuwa akifunga mabao,
tayari ameonekana atakuwa hatari zaidi. Lakini Balotelli bado anasua na vituko
ndiyo vinachukua nafasi.
Kwenye mkataba wake na Liverpool, amebanwa
mambo mengi sana hasa kuhusiana na nidhamu. Inaonekana kulikuwa na mjadala
mkubwa kabla ya kufikia uamuzi wa kumsajili.
Lakini hakuna aliyeonyesha hofu kwake
kutokana na uwezo wake na hata upachikaji mabao. Lakini tokea ametua Liverpool,
kikubwa alichoonyesha ni uwezo mkubwa wa mashuti yaliyolenga bao akiwa sawa
sasa na Diego Costa ambaye anaongoza kwa mabao.
Balotelli anajulikana kwa uwezo mkubwa wa
kupuuza, uwezo wa juu wa kuendelea na anachotaka bila ya kujali. Lakini si
mgeni wa presha za Kingereza.
Kikubwa lazima afunge, hilo halina mjadala
kwa kuwa kila mmoja kwa mashabiki wa Liverpool kuanzia Tanzania, England na
kwingineko wanataka kumuona anafunga, hakuna mjadala.
Hadi sasa kinachoonekana ni kuwa takwimu
zinambana, hata ukiangalia wakati akiwa Inter Milan, Man City na AC Milan,
alikuwa na vitu vizuri zaidi ‘alivyotoa’.
Lakini tokea ametua Liverpool, bado haijakaa
vizuri kwake na hana ujanja, achague kufunga au kukubaliana na Mancini ambaye
walikuwa wakikwaruzana mara kwa mara kuwa ataporomoja haraka na ndiyo utakuwa
mwisho wake.
TAKWIMU:
INTER
MILAN:
Mechi 59
Kaanza 35
Dakika 3315
Mabao 20
Kuotea 26
MAN
CITY:
Mechi 54
Kaanza 33
Dakika 3000
Mabao 20
Kuotea 25
AC
MILAN:
Mechi 43
Kaanza 37
Dakika 3438
Mabao 26
Kuotea 23
0 COMMENTS:
Post a Comment