Kiungo mshambuliaji wa Simba, Mganda,
Emmanuel Okwi, hivi sasa ni mwenye mawazo mengi kila anapofikiria kasi ya
wachezaji wawili wa Yanga, Andrey
Coutinho na Simon Msuva kabla ya timu hizo mbili kuonyeshana ubabe Septemba 18,
mwaka huu.
Okwi amekumbwa na hali hiyo kutokana
na kukosa imani na safu ya ulinzi ya timu yake ambayo imeonyesha kutokuwa imara
katika mechi zake za Ligi Kuu Bara.
Okwi amesema bado hawajawa katika kiwango chao bora hali inayopelekea kuwa na mawazo mengi.
Alisema kama safu hiyo inashindwa
kukabiliana na wachezaji ambao kasi yao ni ya kawaida, vipi itakapokutana na
wachezaji wenye kasi kubwa kama ilivyo kwa wale ya Yanga?
“Tunatakiwa kubadilika sasa na kucheza
soka la uhakika, vinginevyo mambo yatakuwa magumu sana kwetu na tutashindwa
kufikia malengo tuliyojiwekea msimu huu.
“Tunakabiliwa na mechi ngumu zaidi
mbele yetu na ambazo zina upinzani mkubwa, hivyo kama tukiendelea kuwa katika
kiwango hiki na kufanya makosa ya ajabu mara kwa mara, itakuwa vigumu kwetu
kufanya vizuri katika mechi hiyo.
“Ni matumaini yangu kuwa kocha atakuwa
ameyaona makosa yote yaliyojitokeza, hivyo atayafanyia kazi haraka iwezekanavyo
kabla ya kukutana na Yanga ambayo ina wachezaji wengi wenye kasi kubwa kama
vile Msuva, Ngassa na Coutinho,” alisema
Okwi ambaye katika mechi ya juzi dhidi ya Stand United, alionekana
akiwafokea mabeki wa timu hiyo baada ya kufanya makosa yaliyowapatia wapinzani
wao hao bao la kusawazisha.
Okwi amejiunga na Simba hivi karibuni akitokea
Yanga ambayo alikuwa akiitumikia msimu uliopita, hata hivyo usajili wake huo
ulizua utata mkubwa kabla ya TFF kuamua acheze Simba.
0 COMMENTS:
Post a Comment