Kocha Mkuu wa Simba, Mzambia, Patrick
Phiri, ametoa wiki moja, kwa ajili ya kukiandaa vyema kikosi
chake ili kiwafunge wapinzani wao, Yanga.
Timu hizo zinatarajiwa kuvaana Oktoba
18, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi
Kuu Bara.
Simba hadi hivi sasa, imecheza michezo
mitatu ya ligi kuu na kutoka sare zote. Ni dhidi ya Coastal Union, Polisi
Morogoro na Stand United, zote zikichezwa kwenye Uwanja wa Taifa.
Phiri alisema kuwa, kutoka sare mechi
tatu siyo sababu ya kufungwa na wapinzani wao Yanga, hivyo yapo matarajio
makubwa ya ushindi kwa kuanza na Yanga.
Phiri alisema, ameona upungufu mdogo
kwenye kikosi chake ambao amepanga kuufanyia kazi na tayari ameanza kuifanyia
kazi safu ya ulinzi kwa kumtoa Mganda, Joseph Owino na kumuingiza Joram Mgeveke
kwenye mechi ya juzi dhidi ya Stand.
Mzambia huyo alisema, anashukuru kuona
mabadiliko makubwa kwenye safu hiyo iliyocheza dhidi ya Stand iloyoongozwa na Mgeveke
na Hassani Isihaka.
Phiri ana matumaini makubwa kwamba,
wiki moja inatosha kurekebisha makosa madogo kwenye kikosi hicho kabla ya mechi
ya watani.
“Ninaamini nina kikosi imara na chenye
wachezaji wazoefu kama Okwi (Emmanuel), Kiemba (Amri), Owino, Casillas (Husein
Sharifu), hivyo sioni sababu ya kupoteza mechi na Yanga.
“Nimepanga kutumia wiki moja kwa ajili
ya kufanyia marekebisho sehemu zenye upungufu, ninaamini siku hizo zinanitosha
kabisa kuwafunga hao Yanga, hizi sare tunazopata hazimaanishi timu yangu ni
mbovu,” alisema Phiri.
Phiri aliiongoza Simba kutwaa ubingwa
wa Tanzania Bara msimu wa 2011/12 kwa utamu wa kuifunga Yanga mabao 5-0.
0 COMMENTS:
Post a Comment