Mashabiki wa Simba walioonekana na machungu, walimvaa mshambuliaji Mganda wa
timu hiyo, Emmanuel Okwi, huku wakimhoji kwa nini timu haifanyi vizuri, juzi.
Lakini shabiki mmoja, yeye alienda
mbali, kwani alijitokeza mbele akitaka kumfanyia fujo, jambo ambalo lilizua
fujo na polisi kulazimika kuingilia kati na kuwatawanya mashabiki hao. Ilikuwa
ni baada ya mechi dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Taifa, Simba ilimaliza mechi hiyo kwa sare ya bao 1-1- ikiwa ni tatu mfululizo msimu huu.
Juzi, tafrani ilikuwa kubwa kwenye
basi la Simba, mashabiki walilizingira na kuanza kuwatolea maneno makali
wachezaji, wakilalamika kwa nini wanashindwa kufanya vizuri.
Lakini Okwi ndiye aliyeonekana
kuzongwa zaidi na mashabiki hao waliokuwa wamepandwa na jazba.
Kama siyo polisi waliokuwa karibu na
eneo hilo kuingilia kati, pengine hali ingekuwa mbaya zaidi.
Okwi bado hajafanya kile
kilichotarajiwa na mashabiki wa Simba, baada ya kutua msimu huu kwa usajili
uliozua utata akitokea Yanga ambayo ilikuwa na mgogoro naye.
0 COMMENTS:
Post a Comment