SIMBA imeanza Ligi Kuu kwa kutoka sare mechi zake zote
mbili ilizocheza nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Hali
ambayo inaonekana kuwaudhi sana mashabiki na wanachama wa klabu hiyo.
Sare ya kwanza ya mabao 2-2 dhidi ya Wagosi wa Kaya,
Coastal Union ambao walisawazisha mabao mawili wakati Simba ilitangulia kufunga
mawili hadi mapumziko. Sare ya pili dhidi ya Polisi Moro.
Simba ilianza kufunga bao, ikaongoza hadi mapumziko
lakini kipindi cha pili, Polisi Moro wakasawazisha kupitia Danny Mrwanda na
kufanya matokeo ya mwisho kuwa bao 1-1.
Hizo ndiyo hasira za baadhi ya Wanasimba ambao
wameonyesha wazi hasira zao kuhusiana na timu yao kushindwa kufanya vizuri.
Kimahesabu hasi sasa Simba imepoteza pointi nne nyumbani.
Kila mechi imeacha pointi mbili zikipotelea hewani na
sasa ina kazi nyingine ngumu mbele yake Jumamosi, itakapokuwa na kazi ngumu ya
kupamabana na Stand United ambayo ilianza kwa kufungwa nyumbani, halafu
ikashinda ugenini.
Sare mbili za Simba zimeanza kuonekana kama ni jambo
kubwa sana, lakini sasa limeingia sehemu nyingine ambayo ninaweza kusema si
sahihi.
Kwa kuwa kuna watu leo wanaamini eti kutofanya vizuri
kwa kikosi hicho chini ya Patrick Phiri ni kutokana na kutokuwa na maelewano mazuri
na mashabiki na wanachama wengine wanaojulikana kama Simba Ukawa.
Awali nilidhani ni jambo la utani wa kimpira, lakini
kadiri siku zinavyosonga mbele limekuwa likizidi kuchukua nafasi na ikiwezekana
kuanza kuwashawishi baadhi ya watu kwamba hao Simba Ukawa ndiyo wanaoifanya
Simba isifanye vizuri.
Wako sasa wanaamini ambao nimewasikia wakizungumza hivyo
huku nikiwatazama na wengine nikawasikia wakihojiwa kwenye redio. Baada ya
hapo, kuna baadhi ya mashabiki wameanza kuushauri uongozi wa Simba kufanya
suluhu na wanachama hao wa Simba Ukawa.
Suala la suluhu ni jambo jema kwa ajili ya kuongeza
umoja ndani ya Simba maana umoja ni nguvu na hii ni kati ya misemo ya
utambulisho wa Simba. Kushirikiana ni jambo jema na msaada mkubwa kwa kundi la
watu linalotaka kufanya jambo moja kwa pamoja.
Lakini si kuweka hisia za kusema Simba ukawa ndiyo
chanzo cha Simba kutofanya vizuri. Hii itakuwa ni sehemu ya kuonyesha kiasi
gani bado watu wapo katika karne ya 21 wanaendelea kuishi na mawazo ya enzi za
karne za mawe.
Mawazo potofu, mawazo yasiyo na mwendo, hisia zisizo
sahihi, hisia pungufu zilizokuwa na mashiko na hazipaswi kupewa nafasi katika
kipindi chetu hiki, la sivyo tutaruhusu kuwa na watu ‘old model’ kwenye maisha
ya sasa!
Watu kama hao ni wale wanaoamini ushirikina ndiyo
unaocheza ni kosa kubwa, kuwapa watu nafasi waamini wanachosema ni kweli ni
kosa jingine kwa kuwa ni kuendelea kuidanganya jamii iishi na imani za zama za
mawe.
Si sahihi hata kidogo kuamini soka leo linaendeshwa na
ushirikina na kwamba timu haiwezi kufanya vizuri bila ya kuwa na mganga bora wa
kienyeji. Hapa ndiyo tumekuwa tukikwama, najua ni mradi watu fulani, lakini
vizuri kupima mnachofanya.
Msisitizo wangu, Simba inashindwa kufanya vizuri
kiufundi uwanjani. Ninamaanisha kukosa mabao, mabeki wao kutokuwa makini,
kiungo kupoteza ushirikiano katika kipindi cha pili ukilinganisha na
wanavyoanza kipindi cha kwanza.
Kocha Mkuu Patrick Phiri amesema wanayafanyia kazi mambo
hayo, wapeni nafasi na vizuri mambo hayo yashughulikiwe kwa kufuata utaratibu
badala ya papara au kutaka kuonyeshana, mwisho mtajichanganya zaidi na kuanza
kupokea vichapo na si sare tena.
0 COMMENTS:
Post a Comment