Na Saleh Ally
LIGI KUU England huwezi ukaiamua kwa mechi
moja hasa kama si mechi za mwisho za msimu. Utamu wake umegawanyika na hilo
linathibitika kila mwisho wa wiki zinapochezwa mechi za Premier League.
Ndiyo ligi inayotazamwa na mashabiki wengi
zaidi. Leo, kesho na keshokutwa utaona shughuli na namna mechi zitakavyokuwa na
upinzani. Usitazame mechi ya Liverpool dhidi ya Chelsea pekee, kwa kuwa kuna mengi
yatatokea.
Kila mechi ya Premier League inapochezwa,
huacha gumzo kwa wiki au mwezi mzima kwa kuwa huwa hazikaukiwi vituko.
Katika mechi za wikiendi hii, kuna mambo mengi
sana utayaona kutokana na kila timu inavyotaka kufanya lakini yote yanayokea,
lengo likiwa ni kufanya vizuri.
Anfield yenye hofu:
Chelsea imesafiri hadi Anfield, Liverpool
kucheza na wenyeji. Kumbuka haijafungwa hata mechi moja na ndiyo inaonekana ni ‘Top
Team’ katika Premier League.
Tatizo moja Liverpool imekuwa na mwendo wa kusua,
wanajua ilivyo kazi kuwazuia wakali kama Chelsea. Na kazi kubwa itakuwa ni
kuwazuia wasifunge mapema ili kuendana na kauli ya msimu uliopita ya
mshambuliaji wao wa zamani Luis Suarez aliyesema: “Raha ni kuitangulia Chelsea,
ukiacha wakufunge kwanza, ujue umekwisha kwa kuwa kusawazisha dhidi yao ni
karibu kabisa na kusema ni jambo lisilowezekana.”
Licha ya kuwa nyumbani, utawaona Liverpool
wakijilinda sana na kufanya mashambulizi ya kushitukiza. Lakini inawezekana
kabisa ukawaona watu usiowategemea kama Mario Balotelii na Didier Drogba waking’ara
kwa kuwa wana uzoefu na mechi kubwa.
Arsenal na marekebisho:
Arsenal wapo ugenini dhidi ya Swansea, timu
ambayo iliweka rekodi kwa misimu miwili sasa na kuchukua ile sifa ya Arsenal ya
kumiliki mpira kuliko timu nyingine.
Safari hii Arsenal inakwenda ikiwa na timu
nyingine ambayo ni tofauti na ile iliyokuwa ikiongozwa na Arsene Wenger, si
yule aliyekuwa akipewa sifa ya ubahili.
Unaweza kusema Arsenal imekamilika kwa kuwa
ina wachezaji wapya wazoefu na itaingia kuivaa Swansea ikiwa inataka
kurekebisha makosa ya kutoka sare ya bao 3-3 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa
Ulaya dhidi ya Anderlecht ya Ubelgiji baada ya kuwa imetangulia kwa mabao 3-0,
tena ikiwa nyumbani.
Licha ya kumuwekea ulinzi mkali Wilfried Bonny
kutoka Ivory Coast, utakachokiona, pamoja na kikosi cha Arsenal kuonekana kiko
imara, watafanya kazi ya ziada kuwazuia Swansea kumiliki mpira na watajaribu
kuwafunga mapema ili kuwachanganya. Wakichelewa kupata bao la mapema,
watakiona.
Ubabe wa Everton ugenini:
Everton haiko katika kiwango kizuri kama msimu
uliopita ambao ulikuwa wa kwanza kwa kocha wake, Roberto MartÃnez ambaye
alijiunga na timu hiyo akitokea Wigan Athletics ambayo iliteremka daraja.
Presha kwa kocha huyo iko juu licha ya kwamba
hata kama atafanya vibaya katika mechi dhidi ya Sunderland, kesho ugenini,
lakini ishu ni kupata nafasi za juu ili ashiriki tena michuano ya Ulaya.
Utaona mechi ya kasi iliyojaa ubabe kwa kuwa
Sunderland wanajua Everton wana kasi lakini kocha wao, Gus Poyet lazima atakuwa
amesisitiza Paka Weusi lazima waibuke na ushindi maana mwendo wao ni mbaya
zaidi ya bibi kizee mwenye mkongojo.
Ngumu sana:
West Brom wakati wanawakaribisha nyumbani
Newcastle, hii itakuwa kati ya mechi ngumu zaidi kwa wikiendi hii.
Kila timu ina pointi 13, Newcastle ndiyo
wameamka lakini West Brom chini ya Alan Irvine aliyewahi kuwa msaidizi wa David
Moyes kwa vipindi viwili tofauti, imekaa vizuri na utaona mtu kama Saido Berahino
mwenye asili ya Burundi amekuwa moto.
Kila moja itataka kushinda na utaona
mashambulizi mengi zaidi kwa maana ya takwimu na inawezekana kuwa na sare au
kipigo kutoka upande wowote ule.
Hisia za uadui:
QPR inawakaribisha mabingwa Manchester City
kwenye uwanja wa wake wa Loftus Road, ambao waliuachia majonzi katika msimu wa
2011/2012.
Sergio Aguero alifunga bao la dakika za
nyongeza na City ikabeba ubingwa na kuwaacha Manchester United wakiwa
wamezubaa.
QPR waligeuzwa ngazi ya ubingwa, mechi yao
dhidi ya City itakuwa ngumu kwa kuwa watataka kuwaonyesha kuwa wao si wale wa
kipindi kile, lakini usisahau kuwa hawana mwendo mzuri chini ya kocha wao
mkongwe, Harry Redknapp.
Hivyo ni mechi ya kuonyeshana nani zaidi, pia
ni mechi ya kila mmoja kutaka kurejea katika hali nzuri kwa kuwa hata Man City,
wameingia kwenye kundi la wanaosuasua.
0 COMMENTS:
Post a Comment