November 8, 2014

MARSH (KULIA) WAKATI AKIWA KOCHA MSAIDIZI WA TAIFA STARS. KUSHOTO NI ALIYEKUWA BOSI WAKE, KIM POULSEN.

Baada ya hivi karibuni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kukumbwa na kashfa ya matumizi mabaya ya fedha zake kufuatia kuibuka kwa mvutano kati yake na klabu za ligi kuu, mapya yamezidi kuibuka katika shirikisho hilo.


Katika ripoti maalum ya ukaguzi wa mahesabu uliofanywa na kampuni binafsi kwenye shirikisho hilo (jina tunalo), TFF inadai kuwa ilitumia dola 667 ambazo ni zaidi ya shilingi 1,000,000 kwa ajili ya matibabu ya aliyewahi kuwa Kocha Msaidizi wa timu ya taifa, Taifa Stars, Sylvestre Marsh jambo ambalo siyo kweli.

Hali hiyo imeonyesha wazi ni jinsi gani TFF inavyochakachua fedha za udhamini wake na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na kuwanufaisha baadhi ya watu ndani ya shirikisho hilo na siyo zitumike kwa ajili na maendeleo ya soka la Tanzania.

Katika kipindi chote ambacho Marsh alikuwa hospitalini kwa ajili ya matibabu ya matatizo yaliyokuwa yakimsumbua, Championi ndilo lililokuwa la kwanza kuandika habari kuhusiana na kocha huyo na mara kwa mara lilikuwa likimtembelea hospitalini kwa ajili ya kumjulia hali, hivyo linajua kila kitu kilichokuwa kikiendelea juu yake.

Moja ya kazi kubwa ambazo gazeti hili liliifanya baada ya kufika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alikuwa amelazwa kocha huyo mara ya kwanza na kutoridhika na mazingira ya wodi aliyokuwemo, liliandika habari zake na kuuhamasisha umma wa Watanzania kujitokeza kumsaidia.
Hata hivyo, wadau na wapenzi wa soka hapa nchini ambao waliguswa na taarifa hiyo, walijitokeza na kumsaidia kocha huyo hospitalini tangu alipoanza kupata matibabu ya tatizo hilo lilokuwa likimsumbua mapema Februari mwaka huu, kisha akahamishiwa Hospitali ya Ocean Road na mpaka anaondoka hospitalini hapo, alikuwa anaendelea vizuri.

Kwa kipindi chote hicho ambacho Marsh alikuwa akipata matibabu katika hospitali hizo, alikuwa akihudumiwa na mfadhili mmoja ambaye jina lake tunalo na alilazimika kufanya hivyo kwa sababu TFF haikuonyesha dalili zozote za kumsaidia baada ya Rais wa TFF, Jamal Malinzi kumtoa Mwanza.

Baada ya Champoni kuiona ripoti hiyo ya TFF kuwa ilitumia dola 677 kwa ajili matibabu ya kocha huyo, lilimtafuta Marsh ili kujua zaidi ukweli wa jambo hilo ambalo linaonekana kuwa na ukakasi ndani yake.


“Kiukweli kwa sasa sipendi kuongelea mambo ya nyuma, kikubwa nashukuru Mungu nimepona lakini ninyi kama waandishi wa Gazeti la Championi ambao tulikuwa pamoja tangu naumwa mpaka sasa naamini mlikuwa mnajua na mliona kila kilichoendelea kwa kipindi chote hicho kuanzia Muhimbili mpaka Ocean Road, hivyo sina haja ya kuzungumza mengi,” alisema Marsh ambaye hivi sasa yupo jijini Mwanza akisimamia kituo chake cha soka cha Marsh Academy.

SOURCE: CHAMPIONI

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic