November 8, 2014



Na Saleh Ally
SARE sita mfululizo za Simba zimekuwa gumzo kupita kiasi hali ambayo inaonekana kuwavuruga mashabiki, wanachama, wachezaji, makocha na hata viongozi wa klabu hiyo.


Tatizo kubwa kila mmoja amekuwa akisema lake, kila mmoja anaamini tofauti na wengine wanaamini tu wanavyoambiwa bila ya kufanya uchunguzi kama lile suala la kuwa wanachama Simba Ukawa ndiyo wanafanya timu ipate sare!

Simba inabanwa na masuala ya kiufundi kwa maana ya uchezaji, Kocha Patrick Phiri inabidi abadilike na kwenda tofauti kwa maana ya kuwa na kikosi chenye uchezaji wa kasi.

Hakuna ubishi kuwa kadri siku zinavyokwenda, kumekuwa na mabadiliko na unaweza kusema huenda Phiri raia wa Zambia akawa anapiga hatua na mambo mawili ndiyo makubwa zaidi, kuongeza nguvu kwenye ushambuliaji na kuongeza ugumu katika ulinzi.

Katika sare zote sita, sare tano ni za mabao na zote Simba imetangulia kufunga, jiulize siku wapinzani wakianza kufunga, itasawazisha? Lakini safu yake ya ulinzi haina uwezo wa kulinda mabao yanayoanza kufungwa.

Lazima Simba iongeze wachezaji wenye uzoefu katika nafasi kadhaa ili kuimarisha kikosi bila ya kujali kuwa kocha aliyepo ni Phiri au Kim Poulsen ambaye uongozi umeishafanya naye mazungumzo.

Beki ya kulia:
Simba imekuwa ikimtumia Miraji Adam, huyu bado ni kinda na anahitaji muda. Taratibu anaweza akawa anacheza lakini kwa ligi yenye ushindani kama hii ya sasa ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2014-15, kuna tatizo.

Mifumo ya timu nyingi inashambulia kutumia viungo wa pembeni pia mabeki wa pembeni. Usisahau mabeki na viungo hao wanakuwa na kasi kubwa na wengi wana uzoefu.

Kwa hapa Simba inaweza kuwasajili kati ya mabeki wawili kujiimarisha. Shomari Kapombe wa Azam FC ambaye uongozi wa klabu yake umeishatangaza kumuweka sokoni. Pia Hassan Ramadhani ‘Kessy’ ili kuwa na watu wanaoweza kukaba kwa ajili ya ulinzi lakini kusaidia mashambulizi.

Beki wa kati:
Joseph Owino safi, Hassan Isihaka si vibaya sana na anajitahidi, lakini Simba inahitaji beki mwingine wa kati mzoefu sababu ya mambo mawili. Kwanza ina namba sita Jonas Mkude ambaye ni kinda, hivyo lazima kuwe na wazoefu wawili au wenye nguvu na kujiamini zaidi.

Kawaida namba nne anatakiwa kuwa ‘mkatili’ mwenye uwezo wa kuvuruga mambo, halafu anayemaliza kazi kama Owino yeye ndiye anatuliza mambo kwa kumalizia kazi. Isihaka si mchezaji wa aina hiyo na hata uchezaji wake anakuwa kama namba tano ambayo ni aina ya uchezaji wa Owino pia.

Said Morad wa Azam FC au ‘patna’ wake Aggrey Morris, pia Salim Mbonde wa Mtibwa Sugar ni kati ya watu wanaotakiwa au wengine wa aina hiyo. Simba haina beki wa kati anayeweza kuwatisha washambuliaji kutokana na ugumu au uimara wake, hiyo haiwezi kuwa safu imara.

Kiungo mchezeshaji:
Nani anachezesha Simba, nani anakimbia na mpira katikati, nani anatoa pasi za haraka, karibu na mbali katika kikosi cha Simba.

Angalia Phiri alivyolazimika kujaribu, mechi dhidi ya Coastal alicheza Kisiga, alilazimika kumtoa, baadaye akanza kumtumia Awadhi Juma.

Utagundua aina ya wote wawili si wale wenye kasi au uchezeshaji wa kutembeza timu. Ndiyo maana Mtibwa Sugar, zaidi walimtumia Kisiga kama namba kumi. Bado kiungo huyo anaweza kucheza vizuri, lakini anahitajika anayeweza kushika dimba kweli kama ilivyokuwa kwa marehemu Mutesa Mafisango.

Straika:
Kuna Ame Ali wa Mtibwa Sugar ambaye alipelekwa Simba wakaona hana kitu, Kipre Tchetche ambaye Azam FC imemuweka sokoni na Itubu Imbeni raia wa Kenya mwenye asili ya DR Congo ambaye anakipiga Coastal.

Amissi Tambwe bado anahitajika Simba, watajidanganya kutaka kumuacha. Lakini anahitaji msaada kutoka kwa mabeki wenye uwezo wa kupiga krosi nzuri, viungo wenye pasi nzuri za mwisho lakini mfanya vurugu mmoja.

Yaani mshambuliaji anayewapa mabeki wakati mgumu kama ilivyo kwa Kipre au Imbem ambaye ndiye alikuwa chachu ya Coastal kusawazisha mabao yote mawili ilipocheza na Simba katika mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Bara.

Ukimtoa Emmanuel Okwi katika safu ya ushambuliaji. Hakuna mshambuliaji mwingine tishio ambaye mabeki kabla ya kukutana na Simba wanakuwa wanamuombea augue homa ili wapishane naye.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic