Kocha Mkuu wa Simba,
Mzambia, Patrick Phiri, ametamka kwa kujiamini kuwa, kiungo wake mkabaji, Jonas
Mkude, amesaini Simba mkataba wa miaka miwili na Yanga wasahau nyota huyo
kusaini huko.
Kauli hiyo inaonekana kupishana
na ya kiungo mwenyewe ambaye anadai yeye hadi hivi sasa hajasaini Simba huku akitoa
nafasi kwa klabu zinazomhitaji kumfuata kwa ajili ya kufanya mazungumzo ili
asaini kwenye msimu ujao.
Kwa mujibu wa kanuni za
Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), kiungo huyo anaruhusiwa kufanya mazungumzo
na klabu inayomhitaji kutokana na kubakiza miezi sita kwenye mkataba wake.
Phiri alisema kuwa
ana uhakika mkubwa wa Mkude kusaini Simba, hivyo amewaondoa hofu mashabiki
kuhusiana na mchezaji huyo kwenda Yanga.
Phiri alisema, ni ngumu kwa
kiungo huyo kuondoka Simba hata kama bado hajasaini kutokana na umuhimu mkubwa
alionao kwenye kikosi chake hicho.
Mzambia huyo aliongeza,
tayari amewaonya viongozi wa timu hiyo kwa kuhakikisha wanawabakiza wote
anaowahitaji ambao mikataba yao inaelekea ukingoni kumalizika.
“Nikupe siri moja, Mkude
amesaini Simba na hizo taarifa za kwenda huko Yanga ni uongo, mimi ninakuthibitishia
hilo, kama unabisha tusubiri tuone kwenye usajili ujao.
“Ni ngumu kumuachia
mchezaji mwenye umuhimu ambaye anapata nafasi kwenye kikosi cha kwanza kwenda
kuichezea timu nyingine tena kwa wapinzani wetu wakubwa Yanga.”
0 COMMENTS:
Post a Comment