Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva,
ameendelea kuonyesha kuwa anaweza kuendelea kuwa hatari kwenye kikosi cha Yanga
baada ya kuonyesha uwezo katika mazoezi ya timu hiyo.
Msuva ambaye amekuwa gumzo katika mechi za hivi
karibuni, alikuwa nyota wa mechi ya mazoezini ya Yanga dhidi ya Abajalo FC,
juzi Jumatano kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola jijini Dar.
Winga huyo alifunga mabao mawili na
kuisawazishia timu yake ambayo ilikuwa nyuma kwa 2-0 dhidi ya wapinzani wao hao
ambao wanashiriki michezo ya Ligi Daraja la Pili Taifa.
Katika mchezo huo uliochezwa huku kukiwa na
manyunyu ya hapa na pale, Msuva alionyesha uwezo mkubwa wa ‘kulijua lango’
ambapo alifunga bao safi kwa kuwakusanya mabeki wa timu pinzani.
Kama hiyo haitoshi, baadaye Msuva alionyesha
kuwa hakubahatisha kwa kufunga bao lingine kwa kichwa akiwa karibu na lango,
akiitendea haki krosi iliyochongwa na mshambuliaji wa timu hiyo, Jerryson
Tegete ambaye naye alifunga bao moja katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya
mabao 3-3.
Hata hivyo, Abajalo ambayo haikupewa nafasi
kubwa ya ‘kufurukuta’ kabla ya mchezo huo, ilionyesha soka safi hasa kipindi
cha pili huku Yanga iliyokuwa chini ya nahodha wao, Nadir Haroub ‘Cannavaro’
ikiwapa nafasi ‘madogo’ hao kucheza wanavyotaka.
Mabao ya timu hiyo yenye
maskani yake Sinza jijini Dar, yaliwekwa wavuni na Bakari Mwinjuma aliyefunga
mawili, huku Yusuph Kinamuhama akifunga moja.







0 COMMENTS:
Post a Comment