Na Saleh Ally
MICHUANO ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon),
inaanza kutimua vumbi Januari 17 hadi Februari 8, mwakani.
Gumzo lake lilipunguzwa kasi baada ya
waliotakiwa kuwa wenyeji, Morocco kujitoa katika hatua za mwisho wakieleza
kuhofia suala la ugonjwa hatari wa Ebola.
Sasa mzigo umesogezwa Equatorial Guinea ambayo
mwaka 2012 kwa kushirikiana na jirani zao Gabon iliandaa michuano hiyo na
wenyeji wote wakafanikiwa kutinga robo fainali.
Kuna makundi manne katika michuano hiyo, kila
moja likiwa na timu nne. Kinachoumiza ni kwamba hakuna hata timu moja kutoka
ukanda wa Afrika Mashariki!
Kusini wana Zambia na Afrika Kusini, Kati wana
DR Congo na Congo BR. zilizobaki ni timu za Kaskazini na Magharibi ambazo
unaweza kusema ni michuano yao.
Ugumu wa hatua ya makundi katika michuano
hiyo, umefanya ule msisimko urudi tena, kwani timu kama Nigeria ambao walikuwa
mabingwa watetezi, wametolewa kwenye hatua za kufuzu.
Maana yake, mwali hana mwenyewe na timu zote
16 zitakazoenda Equatorial Guinea zitakuwa sawa na hakuna cha kuangalia mkongwe
au ubora kwa majina.
Lazima mpira upigwe, kama ingekuwa ukongwe,
Nigeria ingefuzu. Lakini umeona timu kama Afrika Kusini ambayo hadi mwisho wa
mechi za hatua ya kufuzu, haikupoteza hata moja na ndiyo iliyoibania Nigeria,
haikusonga!
Cape Verde imerejea, Ivory Coast imerudishwa
kundi moja tena na Cameroon ambao walikuwa kundi moja kuwania kufuzu. Maana
yake Kundi D litawaka moto.
Lakini Kundi C ndilo hatari zaidi unapoziona
Algeria, Senegal, Ghana na Afrika Kusini zikiwa pamoja. Zote zimewahi kushiriki
Kombe la Dunia.
Lakini ubishi wa Afrika Kusini na Senegal,
ubora wa Ghana na Algeria na zinatakiwa timu mbili tu, haitakuwa kazi ndogo.
Kwa kifupi itakuwa michuano migumu
itakayovutia na vigumu sana kutabiri nani atakuwa bingwa licha ya kwamba kuna
timu zenye uzoefu mkubwa kama Cameroon, Ivory Coast, Ghana, Algeria na Senegal.
KUNDI A:
Equatorial Guinea, Gabon, Congo BR na Burkina
Faso
KUNDI B:
Zambia, DR Congo, Cape Verde na Tunisia
KUNDI C:
Algeria, Senegal, Ghana na Afrika Kusini
KUNDI D:
Ivory Coast, Guinea, Cameroon na Mali








0 COMMENTS:
Post a Comment