Na Saleh Ally
BURUDANI ya soka iko juu sana, inafurahisha kwa wakati husika lakini
mara nyingi haitoki katika moyo wa mhusika kwa kuwa atakuwa akikumbuka mara
kadhaa.
Ndiyo maana utafiti uliofanyika nchini Argentina hivi karibuni,
unaonyesha kuwa maumivu ya soka kwa kuwa yanajumuisha mapenzi, yanaumiza sana
ikiwezekana hata kuliko yale ya mtu kuachwa na mpenzi wake.
Wanaoachwa wakati mwingine huamini wanaweza kupata wapenzi wengine.
Wale wenye mapenzi makubwa na timu zao, wanajua kamwe hawawezi kuhama, hivyo
hawana cha kujipoza wanapoona timu wanazozipenda na kuziamini, zimeadhibiwa.
Kweli burudani yake ni nzuri na inabaki muda mwingi ukiikumbuka kama
ambavyo straika wa Manchester City, Sergio Aguero amekuwa akifunga mabao yake.
Ukijumlisha michuano yote msimu huu ana mabao 19, kati ya hayo
amefunga mabao manne mara moja, matatu mara moja, mawili mara mbili na
yaliyobaki mara moja. Hii inaonyesha Aguero yuko ‘level’ za kina Lionel Messi
na Cristiano Ronaldo.
Kwa sasa Aguero ndiye kinara wa mabao ya kufunga England baada ya
kupachika mabao 14 katika mechi 14. Takwimu zinaonyesha sasa Aguero raia wa
Argentina ana uwezo wa kufunga bao moja katika kila mechi anayocheza.
Anayemfuatia ni Diego Costa wa Chelsea ambaye alianza kwa kasi kabla
ya kupitwa na Aguero. Huyo anaonekana kuwa mpinzani mkubwa ingawa Alexis
Sanchez wa Arsenal raia wa Chile, si wa kumdharau pia, hadi sasa ana mabao
tisa.
Raha ya Aguero si idadi ya mabao ya kufunga pekee, lakini anaonyesha
ni kiwembe. Wakati wowote anaweza kusababisha madhara anapokuwa na mpira.
Katika mechi ya mwisho wakati Man City ilipoivaa Sunderland ugenini,
Aguero alifunga mabao mawili na kusaidia timu yake kushinda kwa mabao 4-1.
Gumzo zaidi ni moja ya bao lake siku hiyo.
Mshambuliaji wa Sunderland, Jozy Altidore raia wa Marekani aliyekuwa
benchi, anaonekana akipiga yowe na kusema: “Mungu wangu.”
Altdore alilazimika kufanya hivyo kwa kuwa Aguero alimpita beki
katika eneo ambalo wengi hawakutarajia, halafu akaachia mkwaju mkali wenye kasi
ya kilomita 78.5 kwa saa. Rekodi zinaonyesha kasi ya kutoka kwenye mguu wake
hadi anaupiga mpira ulikuwa ni sekunde 0.5.
Achana na hilo bao, katika mabao yake 14 ya Ligi Kuu England, 9
aliyofunga ni yale aliyowatoka mabeki kuanzia mmoja, wawili au watatu kabla ya
kufunga.
Maana yake ana uwezo wa kufunga kama mmaliziaji lakini ana sifa ya
kutengeneza bao mwenyewe tena katika wakati ambao wengi hawategemei.
Hii ni mara ya pili anaipa Man City ubingwa wa England, lakini
inaonekana kwa Chelsea wana hofu na kasi ya Man City wanaowakimbiza.
Tatizo kubwa kwa Chelsea linaonekana kuwa ni Aguero kwamba kama
atakuwa katika kiwango alichonacho sasa, halafu asiingie kwenye bahati mbaya ya
majeruhi, basi kazi wanayo.










0 COMMENTS:
Post a Comment