Na Saleh Ally
ILE Simba ya
Patrick Phiri unayoijua, inaonekana imekaribia kurejea na ushindi wa mabao 2-0
dhidi ya Yanga unawaonyesha Simba kwamba wanastahili kuvuta subira.
Phiri amerejea
Simba wakiwa wamepita zaidi ya makocha wanne baada ya kuondoka nchini na
kuiacha timu hiyo.
Lakini kuna
mabadiliko ya mambo mengi, ukiacha makocha, hata wachezaji na viongozi,
wamepita wengi tofauti, hivyo mambo mengi yamebadilika.
Katika mechi ya
kirafiki, juzi Simba ilishinda kikombe cha Mtani Jembe kwa kuichapa Yanga kwa
mabao 2-0.
Phiri anaendelea
kuwa na rekodi ya kuinyanyasa Yanga kwa kuwa amepoteza mara moja tu dhidi ya
Yanga katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Aliyefunga bao
pekee siku hiyo alikuwa Jerry Tegete, Yanga ikiwa chini ya kocha Kosta Papic
iliutafuta mpira vibaya, lakini ikafanikiwa kuibuka na ushindi.
Ukiachana na
ushindi huo, zaidi Phiri amekuwa akipata sare au ushindi lakini kikubwa alichoonyesha
na kuthibitisha juzi ni kwamba yeye ni maestro tactician, yaani mwalimu
hodari na hasa katika mechi kubwa zinazohusisha Simba dhidi ya Yanga.
Kimahesabu, Phiri alimfunika kabisa Maximo.
Uchezaji:
Angalau sasa
unaweza kusema Simba inakwenda kwenye uchezaji wa ‘Kiphiri’, pasi fupifupi
lakini haraka.
Simba inaweza
kubadili uwanja, mpira kutoka kushoto kwenda kulia hata mara nne ndani ya
dakika moja. Kitaalamu wanasema “kuuondoa mpira kwenye matatizo.”
Lakini Simba
ndiyo timu iliyocheza pasi nyingi za kupenyeza, mojawapo ilisababisha faulo
baada ya Emmanuel Okwi kupenyezewa, akamtoka Juma Abdul aliyelazimika
kumkwatua. Yanga ilionekana ni juhudi binafsi za wachezaji, si timu
iliyounganishwa.
Katika kipindi
cha kwanza, Simba walipiga zaidi ya pasi 12 za kupenyeza (penetration passes)
na Jonas Mkude akionekana kuongoza kitengo hicho.
Angalia mabeki
wote wawili wa pembeni, Nassor Said ‘Chollo’ na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’
walipata nafasi ya kupiga krosi kwa kuwa viungo walifinya ndani na kuwapa
nafasi ya kupita. Wakati wachezaji wa Yanga, Oscar Joshua na Juma Abdul,
walilazimika kubaki nyuma muda mwingi na hakukuwa na nafasi ya kusaidia
mashambulizi.
Sub:
Mabadiliko yote
aliyofanya Phiri, yalionyesha kuwa na msaada mkubwa ukilinganisha na yale ya
Maximo.
Mwanzoni tu mwa
kipindi cha pili, Phiri alimtoa Juku Musheed na kumuingiza Joseph Owino baada
ya kuona kuwa Mliberia Kpah Sherman anawasumbua sana mabeki wake kwa kuwa
alionekana kwenye uzoefu na nguvu nyingi.
Dakika ya 65,
Simba ilimtoa Tshabalala baada ya kuumia akaingia Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, hii
huwezi kusifia.
Wengine waliotoka
ni Ramadhani Singano ‘Messi’ na kumuingiza Said Ndemla katika dakika ya 72,
halafu Maguli akaenda nje dakika ya 84, akaingia Danny Sserunkuma.
Wakati mabadiliko
hayo yanafanyika, tayari Phiri alibadili mfumo kutoka 4-4-2 aliyoitumia zaidi
kipindi cha kwanza na kwenda 4-5-1. Hapa akawa analinda zaidi, hivyo Ndemla
atasaidia katikati na Sserunkuma kubaki na mpira.
Wakati huo,
Maximo ndiyo alikuwa anaamka na kumuingiza Hussein Javu na Mrisho Ngassa baada
ya kuumia katika dakika ya 63. Usisahau alimuingiza Salum Telela katika dakika
ya 56 kuchukua nafasi ya Mbrazil, Emerson Roque ambaye hakupaswa kurudi kipindi
cha pili.
Phiri alimaliza
mchezo kwa kumuingiza Shabani Kisiga katika dakika ya 86 akimtoa Simon
Sserunkuma.
Maximo alichelewa
kubadili mambo, hali inayoonyesha Phiri ni mwepesi kujua nini cha kufanya.
Amekutana na
Maximo mara tatu, mara ya kwanza wakiwa na timu za taifa za Zambia na Tanzania,
ikawa sare ya bila mabao kama sare ya pili katika mechi ya Ligi Kuu Bara msimu
huu. Sasa amemmaliza.
0 COMMENTS:
Post a Comment