December 8, 2014


Kwenye michezo suala la thamani ya kitu au jambo, inapewa kipaumbele sana. Kwamba nani analipwa mshahara zaidi, timu ipi ina fedha zaidi au mdhamini yupi anamwaga fedha nyingi zaidi.


Kwa upande wa wadhamini wanaomwaga fedha nyingi kwenye timu kubwa za Ulaya ni pamoja na Fly Emirates wa Real Madrid na Arsenal. Usiwasahau Qatar Foundation wa Barcelona, Chevloret wa Man United , Samsung wa Chelsea, Deutche Telekom wa Bayern Munich na wengine.

Makampuni hayo yanakubali kutoa mamilioni ya fedha kwa kuwa yanajua yatafaidika na matangazo wakati timu hizo zikicheza. Wachezaji wa timu husika huvaa matangazo hayo vifuani mwao.

Wachezaji wanaweza kuvaa matangazo karibu kila sehemu ya jezi au bukta zao. Lakini kifua ndiyo ghali zaidi kwa kuwa anawekwa mdhamini mkuu.

Hilo ndilo lililonivutia kuandika Metodo ya leo baada ya kumuona Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete akiwa amevaa jezi ya zamani ya Real Madrid akifanya mazoezi.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari jana, Kikwete ameshauriwa na madaktari kufanya hivyo baada ya ule upasuaji aliofanyiwa nchini Marekani. Hivyo akiwa na wasaidizi wake, picha zilionekana akiwa amevaa jezi hiyo ya zamani ya Real Madrid ikiwa na tangazo la Beanq-Siemens yenye asili yake nchini Ujerumani.

Kama unakumbuka ile Madrid ya enzi ya akina Ronaldo di Lima, David Beckham, Figo na Zinedine Zidane waliokuwa wakivaa jezi hiyo na Siemens ambayo ni kampuni ya masuala ya umeme na mitambo mkubwa ikawa inalazimika kumwaga hadi dola milioni 118 (zaidi ya Sh bilioni 200) ili itangazwe na Real Madrid kwa misimu mitatu.

Mara baada ya kuiona picha hiyo, nikajiuliza vipi rais wetu avae jezi hiyo na kuitangaza kampuni hiyo ambayo ilipotaka kutangazwa na Beckham au Zidane ililazimika kutoa mamilioni ya fedha?

Nikajijibu, Rais Kikwete ni shabiki wa Real Madrid. Lakini swali jingine likaibuka, hivi ni sahihi yeye kuvaa jezi yenye tangazo na kutokea hadharani? Kwani nini isiwe na ujumbe mwingine kama “ukimwi ni hatari”, “pambana na malaria” au “pambana na unyanyasaji wa wanawake na watoto”?

Naweza nikapishana na wengine, lakini ninaamini kifua cha Rais Kikwete ni ghali zaidi kwa Watanzania kuliko hata cha akina Beckham. Hivyo kama ni shabiki wa Madrid, basi angeweza kuivaa jezi hiyo kwa wakati wake na si pale anapotokea hadharani.

Akiivaa Saleh Ally ambaye naye ni shabiki wa Madrid, wala haina shida, nani anamjua? Tena ilifikia wakati nikasema bora Rais Kikwete angevaa jezi ya Taifa Stars, au hata Yanga, si wote tunajua ni Mwanajangwani. Najua ya Myama hawezi kutinga.

Kwa kifupi, iko haja ya kudhamini kifua cha kiongozi wetu mkubwa na kuangalia kwa umakini sana anavaa nini.

Ikitokea siku kampuni fulani ya mitambo, utengenezaji simu au masuala ya umeme, ikagombea tenda na Siemens halafu ikashindwa, inaweza kuona tofauti.
Huenda inaweza isiuchukulie ushindani ule kama wa kitaalamu na kawaida. Badala yake ikaanza kuwaza kuna upendeleo kwa kuwa Rais Kikwete aliwahi kuonyesha wazi anaiunga mkono kampuni hiyo.

Katika ushindani, kawaida wengi hasa wale wenye tabia ya kutaka kushinda kwa dhati, huwa hawakubali kilahisi na hasa kama wanajiamini kutokana na ubora wao.

Hivyo ni lahisi sana kwa serikali yetu kuingia kwenye mitego au hisia za kujaribu kufikiri ni hivyo kwa kuhakikisha rais wetu havai nguo za matangazo ya makampuni fulani.

Najua yeye kwa England ni shabiki wa Newcastle, fumba macho ujaribu kufikiria hili. Mfano angekuwa shabiki wa Liverpool, halafu akavaa jezi yenye mdhamini wao wa sasa, siku chache baadaye ishu ya Escrow imeibuka na benki hiyo inahusishwa kutokuwa makini. Unafikiri mngesemaje? Mgefikiraje?




2 COMMENTS:

  1. Kumbe kuna wakati Saleh akili yako inafanya kazi vizuri,hongera kwa kuwafumbua macho watanzania maana waandishi wengine wamakalia kuitangaza picha tuu bila kujali matokeo yake

    ReplyDelete
  2. Very informative post! There is a lot of information here that can help any business get started with a successful social networking campaign. metodo fanart 2.0

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic