Uongozi wa Simba umeamua kuachana na harakati
za kutaka kumsajili kiungo mshambuliaji, Mgambia, Omar Mboob ambaye alikuwa
anafanya majaribio ya wiki mbili na kikosi hicho kwa kile kinachosemekana kuwa
uongozi wa timu hiyo kwa sasa hautaki kumuacha mchezaji yeyote.
Mboob ambaye alitua nchini wiki iliyopita
akitokea Semgar FC ya nchini Gambia, alifanikiwa kuitumikia timu hiyo katika
michezo kadhaa ukiwemo ule dhidi ya kikosi cha vijana.
“Viongozi wameamua kuachana na suala la
kumsajili Mboob ambaye alikuwa anafanya majaribio na kikosi hicho kwa kuangalia
kigezo cha kutotaka kuwaacha wachezaji wengine wa kigeni kutokana na umuhimu
wao kwa sasa ndani ya kikosi.
“Ila ameambiwa anaweza tena kurudi Simba kama
akitaka kusajiliwa katika kipindi cha usajili wa mwanzo wa msimu ambapo hapo
viongozi watakuwa wanajua nani wamuache ili yeye apate nafasi ya kusajiliwa,”
kilisema chanzo chetu.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa kamati ya
usajili wa timu hiyo, Zacharia Hans Poppe ambaye hakuwa tayari kukubali au
kukataa kuhusiana na ishu hiyo.
“Siwezi kusema lolote kuhusiana na jambo la
kuachwa kwa Mboob kwa kuwa bado sijapewa taarifa yoyote na viongozi wengine
kuhusiana na mchezaji huyo,” alisema Hans Poppe.
Lakini kabla, Hans Poppe alisema: "Mboob
si kwamba tulikuwa tunamhitaji, kuna wakala wake yuko huko Spain ndiyo aliomba
aje tumuangalie.
"Kama tukiona kiwango chake kiko juu sana
tofauti na wachezaji tulionao, basi tunaweza kumsajili. Vinginevyo tunaweza
kumuacha aende, halafu tutaangalia wakati wa usajili wa mwanzo wa msimu."
…







0 COMMENTS:
Post a Comment