Na Saleh Ally
MECHI ya kirafiki
kati ya Yanga dhidi ya Simba, maarufu kama Nani Mtani Jembe, imepita lakini
imeacha makovu lukuki.
Kama ilivyo
kawaida, Yanga na Simba zinapokutana, anayepoteza basi habaki na amani. Utaona
msimu uliopita, Yanga walifungwa 3-1, wakamfukuza Ernie Brandts.
Msimu huu
wamefungwa tena mabao 2-0, Kocha Marcio Maximo, kiungo Emerson Roque safari
imewakuta, wanarejea kwao Brazil.
Haya ni baadhi ya
madhara ambayo timu zinakutana nayo kila zinapocheza mechi hiyo ya watani na
safari hii inajulikana kama Nani Mtani Jembe.
Nani Mtani Jembe ni
mechi inayoandaliwa na wadhamini wa klabu hizo mbili, Yanga na Simba. Kampuni
ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro.
Kwangu naona
wadhamini hao wamekuwa wakifaidika kupita kiasi na kuzinyonya klabu hizo
kupitia timu zao zinapocheza mchezo wa Nani Mtani Jembe, nisisitize si sahihi,
nitaeleza.
Katika mechi ya
Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, Simba walipata Sh milioni
15 za ushindi, Yanga waliopoteza wakapewa Sh milioni 5. Kabla ya mechi kila
timu hupewa Sh milioni 30 za maandalizi.
Kulikuwa na fedha
Sh milioni 100, hizi zinatokana na kura zinazopigwa na mashabiki. Simba
wakashinda na kupata Sh 77, 590,000, Yanga wakashindwa na kupata Sh 2,410,000.
Ukichukua jumla,
Simba ilipata Sh milioni 122.6 wakati Yanga iliambulia Sh milioni 37.4. Hapa
ndiyo kwenye hoja yangu ya msingi, kwamba wanaofaidika zaidi ni wadhamini
Kilimanjaro, kitu ambacho si sahihi, nafafanua.
Wadhamini hao
wanafaidika zaidi ya maradufu kwa kuwa ndiyo wanaochukua mapato ya mechi,
jiulize kwa nini iwe hivyo?
Umewahi kusikia
wapi, eti Chevloret wa Manchester, Emirates wa Real Madrid, Arsenal au T Mobile
wa Bayern Munich anakwenda kuchukua mapato ya mechi?
Jiulize, mapato ya
mechi ile kama ni chini kabisa, basi itakuwa ni Sh milioni 500. Sasa
Kilimanjaro walitoa Sh 190 kwa Yanga na Simba. Zote zinazobaki zinakwenda wapi?
Tena naweza kusema
hivi, hata ile Sh milioni 100 waliogawana Yanga na Simba, hawakupewa na
Kilimanjaro kwa kuwa ni fedha inayotokana na wanachama wa Yanga na Simba kwa
kuwa walikuwa wakituma SMS kupitia namba maalum na wanakatwa kwenye fedha zao.
Hivyo kama utaitoa
fedha hiyo ya upigaji kura kupitia SMS ambayo ni Sh milioni 100. Maana yake,
Kilimanjaro ilitoa Sh milioni 80 pekee kwa klabu hizo kongwe, zenye jina kubwa
lakini zinakubali kunyonywa fedha zao kirahisi na hakuna anayeamka.
Kwa mantiki hiyo ni
hivi; ile Sh milioni 100 waliyogawana ilitolewa na mashabiki na wanachama wa
klabu hizo kwa kukatwa kupitia SMS.
Sh milioni 20
ambayo waligawana, Simba Sh milioni 15 na Yanga Sh milioni 5 pamoja na Sh
milioni 60 iliyogawanywa kwa ajili ya maandalizi, ndiyo fedha pekee walizotoa
wadhamini hao.
Sasa jiulize kitu
kimoja, wadhamini hao matangazo yao waliyojaza uwanjani, promosheni rundo na
nguvu ya Simba kuwaletea watu zaidi ya 60,000 inalipwaje?
Utasema Simba
wanadhaminiwa na Kilimanjaro, sawa. Si unajua vifua vya wachezaji Simba na
Yanga ni ghali, ikiwezekana TBL wanaweza wakawa wanalipa kidogo.
Hilo linaweza
lisiwe jambo la kuzifanya Yanga na Simba ziwe watumwa kwa kukubali kuchukua kiasi
kidogo kabisa cha fedha kwa kuwa tu mdhamini ametaka au aliamua hivyo.
Wakati fulani,
uongozi wa Yanga uliwahi kuhoji kitita cha Sh milioni 100 kilichokuwa
kinatolewa na Azam TV kwamba ni kidogo. Kweli walikuwa na hoja, sasa huu ndiyo
wakati wa kuhoji fedha kiduchu za TBL zinavyowatumikisha.
Inawezekana hamkuwa
mmeamka, lakini kuna mengi ya kujiuliza, faida na hasara za Mtani Jembe na kama
mnachopata ni sahihi.
Mimi nimeamka, hizi
ni hoja chache. Nitarudi baada ya siku chache kuzijazia, ili tuchangie,
ikiwezekana nitaanzisha mjadala wa wazi, mashabiki na wanachama wa klabu hizo
wachangie, ili kuzisaidia kupata fedha zaidi kwa kuwa zinatumia fedha nyingi,
‘zinajiuza’ kama ulivyo msemo wa kibaya chajitembeza. Nitarudi.
You are great Saleh. Viva forever. Umeongea jambo la msingi ambalo lina ukweli mtupu. Wapo watakochukoa coz utakua umeugusa mrija wao wanaoutumia kunyonya but it z better ulaumiwe lakini sauti ya UKOMBOZI IPAE NA KISIKIKA...Pamoja daima.
ReplyDeleteMillanzi P.J
Wakukaya hapa umegusa kwenye mfupa, wengi hawatakuelewa lakini wachache wenye akili zinazochemka wataelewa nini unachomaanisha. TBL wanachokifanya hawakustahili kukifanya, wanaonesha hawana nia ya dhati kuzikomboa Simba na Yanga bali ni kujinufaisha matakwa yao kama wadhamini. Viongozi wa Simba na Yanga huu ndiyo wakati wa kustuka na kufumbua mambo kuona nyuma ya pazia ya mchezo huo kuna nini.
ReplyDelete