December 17, 2014

TAMBWE  AKIWA AMEJIPUMZISHA KWAKE AKISOMA GAZETI LA MICHEZO NA BURUDANI LA CHAMPIONI AKIWA KWENYE JEZI YA NJANO NA KIJANI AMBAYO SASA ATAKUWA AKIITUMIKIA.

Na Saleh Ally
MUNGU ndiye anayeona kila kitu kilicho mbele, kwani upande mmoja ukifunga, yeye anafungua mwingine.


Hicho ndicho anachoamini mshambuliaji mpya wa Simba, Amissi Tambwe ambaye amejiunga Yanga kwa dau la dola 20,000 (Sh milioni 34).

Tambwe ambaye alikuwa akilipwa mshahara wa dola 1,000  (Sh milioni 1.7) kwa mwezi, sasa atakuwa akipokea mara mbili ya hizo, Sh milioni 3.4 au dola 2,000.

Mrundi huyo ametemwa Simba, ilionekana safari yake imeishia hapo, akiwa katika harakati za kujiandaa kurejea kwao akaichezee timu yake ya zamani ya Vital’O, Yanga wakamwita na kutaka saini yake.

Tambwe anaamini ni nguvu ya Mwenyezi Mungu, halafu anasisitiza kwamba anachotaka ni kuona anapata mafanikio makubwa akiwa na Yanga lakini kamwe, hatawasahau mashabiki wa Simba.

Kwani haikuchukua saa tano tangu Simba imuache kabla ya Yanga kusema inamhitaji. Mazungumzo yao hayakuchukua zaidi ya saa moja, kabla ya Yanga kukubali kumsajili. Ndiyo maana anasema hayo ni mambo ya Mungu.

Simba imemuacha bila ya kuangalia rekodi yake nzuri ya msimu uliopita, nafasi yake amepewa kiungo machachari Simon Sserunkuma kutoka Uganda.

Mashabiki mbalimbali wa Simba walimpigia simu Tambwe na kumueleza wazi kuhusiana na mapenzi yao kwake, kwamba bado wanampenda, anawavutia na hata kama kaenda Yanga, bado wako pamoja.

Hali hiyo imeonyesha kumsikitisha lakini akasisitiza kwamba huu ndiyo wakati mwafaka kwake kusonga mbele kimaisha na atakachofanya ni juhudi kubwa akiwa na Yanga.

Katika mahojiano mafupi na gazeti hili baada ya kuingia mkataba na Yanga, Tambwe amesema anachotaka sasa ni mafanikio makubwa na Yanga.

“Nimesaini mwaka mmoja, kikubwa kwangu ninataka mafanikio. Kawaida mafanikio hayawezi kupatikana kirahisi hivyo.

“Najua natakiwa kupambana, najua natakiwa kugombea namba Yanga na ili niaminiwe lazima nifunge au niisaidie timu.

“Kwa kuwa ni mgeni, huenda nikahitaji muda kidogo. Lakini nitakachofanya ni kufunga ili niweze kuaminiwa na kuungwa mkono.

“Kwa mchezaji kuungwa mkono na mashabiki wa klabu unayoichezea ni jambo jema sana. Niseme siwezi kuwasahau mashabiki wa Simba kwa kuwa waliniunga mkono wakati wote, hata pale nilipokuwa na wakati mgumu.

“Angalia nimeachwa, lakini walipiga simu kunieleza bado wako na mimi. Wakasema uongozi ndiyo umeniacha, lakini bado wananipenda kama mchezaji wao, kweli inatia moyo sana,” anasema Tambwe.

Anapoulizwa siku ikiwadia, atahofia kuifunga Simba kwa kuwa mashabiki wake walionyesha mapenzi makubwa kwake kabla na hata baada ya kuondoka, anasema:

“(Kicheko), hilo halitawezekana, nimekuambia ninataka mafanikio. Sasa nimehamia Yanga, mimi ni mwajiriwa wa Yanga, ninataka kufunga.

“Siku tukikutana na Simba, nitaongeza juhudi zaidi niweze kufunga kwa sababu ya mambo mawili. Yanga ndiyo kazi yangu, lazima niifanye kwa mafanikio.

“Lakini lazima nifute zile hisia kuwa kwa kuwa nilikuwa Simba, basi siwezi kuifunga.”

Tambwe aliifungia Simba mabao 19 katika msimu uliopita na kuibuka Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara.

Mambo yalianza kuharibika ikielezwa kwamba haendani na mfumo wa kocha Patrick Phiri, kwani hadi Simba inafikisha mechi saba, alikuwa amefunga bao moja.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic