Kumekuwa na taarifa zinazotofautiana
kuhusiana na kuchelewa kwa mshambuliaji Emmanuel Okwi aliye kwao Uganda, lakini
ukweli sasa suala la ndoa, ndilo lililomchelewesha.
Uchunguzi umeonyesha Okwi yuko katika mipango ya
kutaka kufunga ndoa.
Lakini ikawa vigumu kupata uhakika kwa kuwa
vyanzo vyetu havikuweza kumpata Okwi jijini humo.
Lakini Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya
Simba, Zacharia Hans Poppe, akakata mzizi wa fitina kwa kulitolea ufafanuzi
suala hilo.
Hans Poppe amesema Okwi amepewa ruhusa ya
kushughulikia masuala yake na hasa hilo la ndoa.
“Anatarajia kufunga ndoa mwezi huu, nafikiri
itakuwa tarehe ishirini, ndiyo maana tumempa ruhusa.
“Ila atarudi kuungana na wenzake kwa ajili
ya mechi ya Nani Mtani Jembe dhidi ya Yanga. Baada ya hapo, tutamruhusu tena,”
alisema Hans Poppe.
Taarifa za kutoka Kampala zinaeleza, Okwi
anamuoa mpenzi wake wa siku nyingi na maandalizi yako katika hatua za mwisho
kabisa.
“Kila kitu kiko vizuri, mambo yako katika
hatua za mwisho kabisa,” kilieleza chanzo kutoka Kampala.
Tayari Simba imeanza maandalizi kwa ajili ya Ligi Kuu Bara na Okwi na Joseph Owino
ambaye amepata msiba ndiyo walikuwa hawajajiunga na wenzao.
SOURCE: CHAMPIONI







0 COMMENTS:
Post a Comment