| RAIS WA TFF, JAMAL MALINZI |
UNAWEZA ukafika mbali zaidi kwa kujiuliza kwamba, hivi
ni kweli mpira wa Tanzania bila ya fitina tena zile zisizokuwa na mashiko
hauwezi kabisa kusonga mbele? Mimi ninaweza nikawa ninaamini tofauti na wewe.
Kila mdau wa soka nchini anajua kwamba mwanasheria Dk
Damas Daniel Ndumbaro amefungiwa miaka saba kushiriki katika masuala ya soka
kwa kuwa tu alisimama imara kuzitetea klabu zisikatwe fedha zao za udhamini
kibabe.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupitia barua
iliyoandikwa na Katibu wake Mkuu, Mwesigwa Celestine, liliagiza klabu zikatwe
asilimia 5 ya fedha zao za udhamini kutoka wadhamini Vodacom na Azam TV.
Hakikuwa kitu rahisi kukubali, TFF haikuwa imekutana na
klabu kujadili hilo kabla ya kuamua tu. Dk Ndumbaro akasimama kidete na
kuzitetea klabu, serikali ikasikia, kupitia Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni
na Michezo, Juma Nkamia ikaungana na Dk Ndumbaro na kupinga hilo.
Serikali ikaagiza, pande hizo mbili zikae na kulijadili
hilo. baadaye Rais wa TFF, Jamal Malinzi alikutana na klabu, wakajadili na
kufikia uamuzi mzuri. Wakati pande hizo mbili zinakutana, TFF tayari ilitangaza
kumfungia Dk Ndumbaro kupitia kamati ya nidhamu.
Tena Dk Ndumbaro alifungiwa wakati serikali ikiwa
imeagiza wakutane na Nkamia akaonyesha masikitiko yake akisema Malinzi na TFF
walidharau wito wake wa kulimaliza suala hilo kwa kukaa.
Shauri la Dk Ndumbaro liliwasilishwa kwenye kamati ya
nidhamu, wakati ilionekana si sahihi, lingepelekwa kwenye kamati ya maadili. Ndani ya siku mbili lilishafikishwa na ndani
ya siku tano tayari ilijulikana Dk Ndumbaro amefungiwa miaka saba!
Adhabu yenyewe ni ya ajabu kabisa, inaonyesha imejaa
visasi, inaonyesha imetolewa kuwatuliza kila wanaoweza kukosoa na ajabu wadau
wa soka wako kimya wakiona ni kawaida. Dk Ndumbaro amekata rufaa, amelipa Sh
milioni moja kwa ajili ya rufaa hiyo, leo ni zaidi ya mwezi, kimya!
Kwa nini isisikilizwe, wakati TFF ilifanya mambo
harakaharaka na kumhukumu miaka saba ambayo Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji,
baadhi ya viongozi wa Simba na wadau wa soka wamekuwa wakiamini ni kubwa na
hailingani hata kidogo na linaloitwa ‘kosa’.
Kama kweli TFF ni taasisi ya Watanzania, taasisi
inayoweza kutenda haki, inayoongozwa na watu watenda haki na wasio na nia mbaya
na mpira wa Tanzania. Vipi rufaa ya Dk Ndumbaro haisikilizwi.
Kuna mdau mmoja aliniambia kuwa TFF inaweza kumfungulia
Dk Ndumbaro kesi nyingine, eti ya kutaka kumpindua Malinzi! Nikamwambia TFF
hawawezi kuwa na mawazo yasiyo na mashiko kama hayo, huenda alisikia tu mtaani
naye akaamini.
Hapa hoja ya msingi ni kwamba, TFF lazima waonyeshe ni
viongozi sahihi wanaoweza kufanya mambo yao kwa kufuata utaratibu na sheria na
si kuyapeleka kwa lengo la kuwakomoa wanaoweza kukosoa.
Mfano kwenye siasa, kila kukicha tunaona wanasiasa
mbalimbali wanapata nafasi ya kusema na kukosoa mambo fulani. Ndiyo maana
tunaweza kuona mambo yanayovumbuliwa ambayo si sahihi kwa afya ya nchi yetu,
hatua zinachukuliwa na mabadiliko yanatokea.
Sasa kama TFF kila atakayekosoa, basi anasimamishwa,
akipeleka rufaa haisikilizwi, pia inapaswa mipango ya kumuangamiza zaidi.
Halitakuwa jambo jema na wadau wa michezo wanapaswa kutokaa kimya.
Maana kama ataachiwa Dk Ndumbaro aangamizwe kimyakimya
bila ya watu kuzungumza lolote kwa kuona jambo la kawaida.
Tutaijengea TFF uwezo wa ‘kifalme’, haitakuwa
ikikosolewa na itataka iende inavyotaka yenyewe bila kushauriwa au kuambiwa.
Tutauua mpira wetu, kumbukeni TFF si ya Malinzi, ni yetu sote ndiyo maana ni
Shirikisho la Soka Tanzania si Shirikisho la nanii, wapiwapi. Amkeni jamani!







0 COMMENTS:
Post a Comment