January 26, 2015

WACHEZAJI WA CAMBRIDGE WAKISHANGILIA BAADA YA KUING'OA MANCHESTER UNITED.

Na Saleh Ally
SOKA raha sana, wakati mwingine utasikia viongozi wa michezo mingine wakilalamika kwamba waandishi au dunia inaupendelea sana mchezo huo.


Kulinganisha na michezo mingine sawa, lakini ubora na matokeo yake ni burudani ambayo ni nadra kuipata katika michezo mingine.

Mfano mzuri ni matokeo ya mechi za juzi za Kombe la FA ambazo zimemalizika kwa vigogo wa Ligi Kuu England kulamba vumbi kutoka kwa timu za ligi za madaraja ya chini.

Manchester United, wao wanalazimika kucheza mechi ya pili kwenye Uwanja wa Old Trafford baada ya sare ya bila kufungana dhidi ya timu ya Daraja la Nne ya Cambridge FC.

Siku hiyo, kocha Louis van Gaal alionekana ni tatizo kutokana na mfumo wake lakini saa chache baadaye timu zinazoshiriki Ligi Kuu England kama Chelsea, Manchester City, Swansea, Tottenham na Southampton zinazoonekana ni kubwa na zilizopewa nafasi ya kusonga mbele zikatolewa kwa kudhalilishwa na timu za madaraja ya chini.

Tena kipigo cha Chelsea ambao ni vinara wa Ligi Kuu England kimekuwa kivutio zaidi baada ya kufungwa mabao 4-2 na Bradford FC inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu England (League One).

Bradford wakiwa kwenye Uwanja wa Stamford Brigde, walitoka nyumba kwa mabao mawili na kufanikiwa kufunga manne, huku Chelsea ikiwa “Full Mziki”!

Mechi hiyo ikaingia kwenye somo kuwa ‘money can’t buy soccer’. Yaani uwezo wa fedha hauwezi kuununua mchezo wa soka kwa kuwa una asili yake sahihi na matokeo ya aina tatu, kushinda, kushindwa na sare lazima yajitokeze katika mechi.

Hili linathibitishwa na mengi sana. Mfano kikosi cha Chelsea ambacho kilianza katika mechi dhidi ya Bradford thamani yake inafikia pauni milioni 200 (zaidi ya Sh bilioni 540) na kilikuwa kikipambana dhidi ya kikosi chenye thamani ya pauni 7,500 (Sh milioni 20).

Pauni hizo 7,500 ni fedha zilizotokana na Bradford kulipa kumnunua mchezaji James Hanson alipojiunga na klabu hiyo lakini wachezaji wengine wote walioanza katika mechi hiyo dhidi ya Chelsea walijiunga wakiwa huru.

Wakati kikosi hicho cha kocha Phil Parkinson kikiwa na thamani ya pauni 7,500 tu, kikosi cha Jose Mourinho kiliingiza wachezaji wengine kutoka kwenye benchi wenye thamani ya pauni milioni 99 (zaidi ya Sh bilioni 267).

Hata wachezaji watatu kutoka kwenye benchi la Chelsea walikuwa wanazidi kwa zaidi ya mara kumi kwa thamani ya kikosi cha Bradford kilichowatoa shoo.

Matokeo hayo ya Bradford ni mfano wa kuonyesha kiasi gani, mchezo wa soka hauwezi kuwa bora pekee kwa mwenye fedha tu.

Hiyo inaonyesha kusajili wachezaji ghali pekee hakuwezi kuwa ndiyo ubora wa kikosi kwa asilimia mia badala yake uwezo wa kujituma, kipaji na kujitambua kunajenga kikosi imara pia.

Ukirudi katika kikosi cha Manchester United ambacho kinalazimika kucheza mechi nyingine Old Trafford dhidi ya Cambridge FC inayoshiriki Ligi Daraja la Nne England, utagundua pia majibu ni yaleyale, fedha haiwezi kuinunua soka.
 
WACHEZAJI WA CAMBRIDGE UNITED WALIOITOA JASHO MANCHESTER UNITED
Maana thamani ya kikosi cha Man United ni zaidi ya pauni milioni 200, lakini ilijikuta ikitoka sare na timu hiyo ya daraja la nne ambayo mshahara wa mchezaji wake mmoja Radamel Falcao ungeweza kuwalipa kwa mwezi wachezaji wote wa Cambridge FC.

Falcao analipwa pauni 265,000 (Sh milioni 730) kwa wiki, wakati wachezaji wa Cambridge FC hawawezi kufikia thamani ya fedha hizo hata kwa mwezi mzima iwapo watalipwa mshahara wao na kocha wao.

Achana na Falcao, jiulize kiasi gani Man United wanawazidi mishahara kama utachukua wachezaji wake wote? Lakini walishindwa kuwafunga.

Kwa hapa nyumbani pia linaweza kuwa funzo kwamba kutokana na utajiri wa Yanga, Simba na Azam FC haina maana kwamba lazima zitapata ushindi.

Soka si mchezo wa mwenye fedha pekee, ndiyo maana unapendwa na watu wengi kwa kuwa dunia ina watu wengi wasio na uwezo mkubwa ukilinganisha na wale wenye uwezo wa kifedha.

Angalia kikosi cha milioni 200 cha Chelsea dhidi ya kile cha Bradford cha pauni 7,500. Alama ya £ inamaanisha fedha ya pauni:

CHELSEA
Petr Cech: £7m
Andreas Christensen: Chipukizi
Kurt Zouma: £12m
Gary Cahill: £7m
Cesar Azpilicueta: £6.5m
Ramires: £20m
Oscar: £25m
John Obi Mikel: £4m
Mohamed Salah: £11m
Didier Drogba: Bure
Loic Remy: £8.5m

BENCHI:
Cesc Fabregas - £30m, Nathan Ake - bure, Eden Hazard - £32m, Thibaut Courtois - £5m, Willian - £32m, John Terry - bure, Ruben Loftus-Cheek - bure

Jumla: £200m

BRADFORD
Ben Williams: bure
Stephen Darby: bure
Rory Mcardle: bure
Andrew Davies: bure
James Meredith: bure
Billy Knott: bure
Gary Liddle: bure
Filipe Morais: bure
Andy Halliday: bure
James Hanson: £7,500
Jon Stead: mkopo

BENCHI:
Alan Sheehan - bure, Billy Clarke - bure, Francois Zoko - bure, Mark Yeates - bure, Jason Kennedy - bure, Christopher Routis - bure, Matthew Urwin - bure

Jumla: £7,500


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic